- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mzee
Kungubaya akiwa na gitaa la galatone enzi hizo. Picha kwa hisani ya Kijiwe cha
Kitime.
Na Daniel Mbega
Wakati umewadiwa
Wa salamu za
wagonjwa
Hospitalini
Leo tunawapa pole
x2
Ajuaye Bwana Mungu
Kwa mzima kuwa mfu
Mgonjwa kuwa
salama
Leo tunawapa pole
x2
Kipindi chenu
kinawapa pole
Wote tunawapa pole
Mungu awajalieni
pole x2
Tunawapa pole x2.
SWADAKTA kabisa.
Hapana shaka yoyote kwamba, mashairi haya si mageni masikioni mwa Watanzania
walio wengi, kwani ndiyo hufungua na kufunga kipindi cha saa nzima cha Ugua
Pole, kilichobeba jina la wimbo huo, kinachosikika Redio Tanzania Dar es Salaam
(RTD) kila siku ya Jumapili kuanzia saa 4.02 asubuhi hadi saa 5.00.
Lakini pamoja na
kufahamika kwa mashairi hayo hata kwa vijana wa kizazi cha leo, ni dhahiri kwamba
si wengi wanaomfahamu mtunzi wa wimbo huo unaoendelea kutamba redioni mpaka
leo.
Huyu si mwingine
bali ni Omar Kungubaya, mkongwe wa muziki aliyedumu katika fani hiyo kwa zaidi
ya miaka 50.
Kwa wale vijana wa
zamani, yaani wa miaka ile ya '47, enzi ambazo nyimbo kama za 'Nina Mpenzi wangu Kibamba' zilikuwa zikitamba sana katika
majukwaa ya muziki, basi watakuwa na kumbukumbu tosha ya mwanamuziki huyo
mkongwe, ambaye hata hivyo, kama walivyo wengi wao, hakunufaika na lolote
katika muziki.
Wapenzi wengi wa
muziki wa dansi walishafikiria kwamba huenda mzee huyu alikwisharejesha namba
kwa Mungu kutokana na ukimya wake wa muda mrefu katika majukwaa makubwa ya
muziki, tofauti na wakongwe wengine ambao wanaendelea kuimba katika bendi
zinazofufuliwa na kisha kuzikwa tena kutokana na kushindwa ushindani wa
kibiashara.
Sijui kwa sasa
mahali aliko, lakini nakumbuka nilikutana naye mwaka 2002 katika ukumbi wa
Container Bar, Maili Moja Kibaha na kufanya mazungumzo naye, wakati akiishi
Kibamba. Kama yu hai, basi wakati huu atakuwa na miaka 74.
Hata hivyo, staili
aliyokuwa akiitumia wakati nakutana naye ni tofauti na ile ya zamani ya kuwa na
bendi, kwani kila siku za wiki endi alikuwa anazunguka kwenye kumbi mbalimbali,
baa na hata vilabu vya pombe za kienyeji akiwa na 'bunduki' yake, yaani gitaa
aina ya galatone akiwaburudisha wateja waliokaa kwenye
meza kwa ajili ya kustarehe.
Kwa upande wao,
wateja nao huamua kumtuza chochote, lakini ilimuwia vigumu kuweza kuwashawishi
ili wampatie fedha kutokana na nyimbo anazoimba.
Hali hiyo
ilimfanya mwanamuziki huyo mkongwe awe akizunguka mpaka kwenye vilabu vya
uchochoroni, hususan huko Kibaha-Maili Moja, ambako nilikutana naye.
Kwa ujumla, staili
hiyo, inayojulikana zaidi kama 'Chuna Buzi', haikuwa ikimnufaishi chochote
zaidi ya kumuwezesha kupata angalau senti kidogo kwa ajili ya mkate wake wa
kila siku tofauti kabisa na mchango wake alioutoa katika jamii.
ALITOKA WAPI?
Mzee Kungubaya ni
matunda mengine ya hazina isiyokwisha kutoka mkoa wa Morogoro, ambao umejaa
vipaji vya kila aina. Alizaliwa mwaka 1939 katika Kijiji cha Mgaza Vigolegole,
Morogoro, ambapo alipata elimu yake ya msingi (darasa la nane) Msamvu Middle
School mwaka 1955.
Alishindwa
kuendelea na masomo ya darasa la tisa kutokana na wazazi wake kushindwa
kumlipia karo.
Historia yake
kimuziki inaanzia mwaka huo wa 1955 akiwa shuleni Msamvu, ambapo wakati huo
alikuwa na umri wa miaka 16 tu, na aliweza kuchaguliwa kuwa kiongozi wa bendi
ya shule na mara baada ya kumaliza shule akajiunga rasmi na bendi ya Cuban
Marimba iliyokuwa chini ya Salim Abdallah Yazidu 'Say'.
Itakumbukwa
kwamba, bendi hiyo iliyokuwa na maskani yake Nunge Welfare (sasa eneo hilo
linajulikana kama Mji Mpya), Morogoro ilikuwa tishio kwa bendi nyingi za Dar es
Salaam na ndiyo iliyoibua vipaji vya wanamuziki wengi. Kwa sasa bendi hiyo
imetoweka katika ulimwengu wa muziki.
Katika mahojiano
maalum, Mzee Kungubaya alimtaja Kibwana Katashingo, aliyekuwa dereva wa
marehemu Salim Abdallah na pia mpiga drum wa bendi hiyo, kwamba ndiye aliyekuwa
mwalimu wake wa kwanza katika muziki wakati alipojiunga na Cuban Marimba,
ambapo yeye Kungubaya alikuwa akipiga gitaa la galatone lenye nyuzi sita.
Mwaka 1960
Kungubaya alichanja mbuga na kuelekea Nairobi, Kenya kwa kile alichosema
alikwenda kujiendeleza kimuziki.
"Huko nilipokelewa
na wanamuziki wakongwe wakiwemo akina John Ondolo Chacha, John Mwale na David
Amunga, ambao wote walikuwa wakikung'uta magiaa ya galatone kwenye vilabu mbalimbali jijini humo.
"Hata hivyo,
mwaka uliofuata nilirejea Morogoro na kujiungan na bendi ya Kilosa Jazz
iliyokuwa ikiundwa na akina Yahya Abbas na marehemu Abel Baltazar. Nilidumu na
bendi hiyo hadi mwaka 1963," alieleza Kungubaya.
Alisema kwamba,
aliamua kurejea tena Cuban Marimba, ambapo viongozi wa bendi hiyo wakampeleka
kwa Mzee Mwaipungu aliyekuwa akiongoza bendi nyingine iliyokuwa tawi la Cuban
Marimba, lakini mwaka 1969 akaondoka.
Safari hii aliamua
kuyaweka kando masuala ya muziki na kuwa 'cashier' katika vituo vya kuuza
mafuta vya Capital Esso Services kilichopo Mtaa wa India na baadaye kituo cha
Agip Centre cha Mwembesongo. Hii ilikuwa mwaka 1970.
Alieleza kwamba,
mwaka 1971 akaamua kurejea tena masuala ya muziki, ambapo mara hii alikuwa
akijitegemea mwenyewe. Kama ilivyo ilivyokuwa wakati nakutana naye, alikuwa
akipiga gitaa moja tu lagalatone, ambapo alihamia Dar es Salaam na
kuanza kutumbuiza katika baa moja iliyokuwa ikimilikiwa na Mama Hamm huko
Tandale, Manzese.
Penzi, anasema,
halina mipaka na halichagui fukara wala tajiri. Kwanini? Anasema kwamba, bosi
wake huyo 'alimzimia' na kuanguka kwenye penzi.
"Hivyo
nikaamua kumuoa mama huyo, ambaye hadi anafariki mwaka 1995 hatukubahatika
kupata mtoto. Lakini mwaka 1974 tulinunua shamba kijijini Kwembe, na kuanzia
hapo mpaka anafariki tulikuwa kijijini na ndiko ninakoishi mpaka sasa,"
alibainisha.
Mzee Kungubaya
alisema kwamba, kabla mkewe huyo hajafariki alimpa ruksa ya kuoa mwanamke
mwingine, ameoa, na wamebahatika kupata watoto watatu, ingawa mmoja alifariki.
ANAFANYA NINI
SASA?
"Kama
ujuavyo, hivi sasa nimekuwa mwanakijiji. Shughuli zangu ni za kilimo ingawa kwa
kweli sina mtaji wa kutosha na mara nyingi natumia jembe la mkono,"
alisema.
Alisema ingawa
yuko kijijini, lakini muziki kwa vile uko kwenye damu yake hawezi kuuacha,
ndiyo sababu kila siku ya Ijumaa hadi Jumapili jioni alikuwa akionekana katika
baa mbalimbali huko Kibaha-Maili Moja, akiwatumbuiza watu kwa kutumia gitaa
lake la galatone alilolinunua miaka ya 1970.
Mara nyingi
ungemkuta akiimba nyimbo nyingi zilizopata kutamba miaka ya 1960 hadi 1970,
hususan nyimbo kama Mtoto si Nguo na Ndugu
sikilizeni navunja vunja vikombe zilizoimbwa
na Heorge Mukabi wa Kenya, na Wanawake
wa Tanzania na Maneno madogo madogo kwa mabibi na
mabwanazilizoimbwa na marehemu Salim Abdallah kule Cuban Marimba.
Wakati wa enzi
zake alitunga nyimbo nyingi sana, lakini alisema kwamba, katika miaka 47 akiwa
kwenye jukwaa la muziki hakunufaika na chochote zaidi ya kuishia kutumbuiza
vilabuni!
Hata hivyo,
aliitaka serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuwajali wasanii wa zamani kwa
kuwaenzi na ikibidi iwekwe siku maalum ya kuwakumbuka wakongwe wa zamani na
kazi zao.
Aidha, alisema kwa
kuwa Sheria ya Haki Miliki imekwisha pitishwa na serikali, basi ni vyema hata
wasanii wa zamani wafikiriwe kupewe chochote na Radio Tanzania kutokana na kazi
zao zilizohifadhiwa huko, ambazo sasa RTD (TBC Taifa) imekuwa ikiziuza.
Comments
Post a Comment