- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Ahmed Mohammed Kipande
Na Daniel Mbega
Ahmed
Mohammed Kipande (alizaliwa mwaka 1937, Kilwa Kivinje mkoani Lindi) alikuwa
mwanamuziki wa Tanzania na kiongozi wa bendi ya Kilwa Jazz. Ahmed Kipande
alishiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa maendeleo na kupigani Uhuru wa
Tanganyika akiwa na bendi yake ya Kilwa Jazz, ambayo siku Tanganyika ilipopata
Uhuru Desemba 9, 1961 ilitumbuiza wimbo wa kusifia nchi hiyo kupata Uhuru kutoka
kwa wakoloni. “Ewe Mola tunakuomba
uibariki Tanganyika yetu na jirani zetu,
Uhuru tumepata lakini, Nyoyo zinasikitika wenzetu wanateseka, Wakoloni wamewashika…” ni mashairi
yaliyokuwemo kwenye wimbo wa Uhuru.
Chini ya
uongozi wa Ahmedi Kipande, Kilwa Jazz ilishiriki pia kutoa burudani wakati
mikakati ya kufanya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye meneo ya makao makuu ya bendi
hiyo jijini Dar es Salaam mwaka 1964. Ahmed Kipande na bendi yake waliteuliwa
na serikali ya Tanganyika kwenda kushiriki sherehe za Uhuru wa Malawi mwaka
1963 na Uganda mwaka 1962.
Maisha yake ya awali
Ahmed
Mohammed Kipande alizaliwa mwaka 1937 huko Kilwa Kivinje mkoani Lindi. Miaka
michache baada ya kifo cha mama yake, Ahmed Kipande alifuatana na baba yake kwenda
Dar es Salaam na akaanza masomo katika shule ya Uhuru Wavulana ilikuwa maeneo
ya Kariakoo, Dar es Salaam.
Kikosi cha Kilwa Jazz.
Ahmed Kipande na 'midomo ya bata'
Katikati ya
miaka ya 1950 Kipande alianza kupiga muziki akitumia ala iitwayo Violin katika
bendi ya Tanganyika Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Zimbe Kidosi. Bendi hiyo
ilikuwa na makao makuu yake katika mtaa wa New Street ambao hivi sasa unaitwa
mtaa wa Lumumba.
Wanamuziki
wa miaka hiyo walianzisha bendi wakizipa majina ya maeneo yale wanakotoka,
hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa
Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika.
Ahmed
Kipande aliyekuwa ametoka Kilwa Kivinje mkoani Lindi naye akishirikiana na
mwanamuziki mwenzake aliyetajwa kwa jina moja la Shamte wakaamua kuanzisha
bendi ya watu kutoka Kusini ya Kilwa Jazz mwaka 1958. Kilwa Jazz ikaanza
kujizolea umaarufu kwa kutunga na kuimba nyimbo mbalimbali zikiwemo za siasa,
mapenzi na za uhamasishaji kupata Uhuru wa Tanganyika.
Alitunga
na kuimba nyimbo kama TANU Yajenga Nchi, Nchi
Yetu, Enyi Vijana Tujenga Yetu, Doli, It
can be done, play your party, Mapenzi Yananivunja Mgongo, Roza Waua, Nipate lau
nafasi, Nacheka cheka Kilwa leo na ule wa Maneno Hayafai.
Wimbo wa Nipate Lau Nafasi ulitungwa na Ahmed
Kipande baada ya kunakili wimbo wa Tabu
Ley na John Bokelo wa Mokolo Nakokufa,
hali kadhalika nyimbo za Nacheka cheka
Kilwa leo, Rose Waua na Maneno Hayafai
ambazo walizinakiri kutoka wimbo wa Course
au Povouir na Est ce Que za T.P.OK. Jazz.
Mwaka 1973,
Kilwa Jazz ilialikwa na kutumbuiza katika utangulizi wa onyesho la gwiji la
muziki wa dansi Afrika, Franco Makiandi na bendi ya T.P.OK. Jazz lililofanya
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Luambo Makiadi baada ya
kuzisikiliza nyimbo hizo alimfuata Ahmed Kipande na kumpongeza kwa umahiri wake
mkubwa wa ‘kokopi na kupesti’ pasipo kukosea.
Kilwa Jazz na usafiri wao
Makao
makuu ya Kilwa Jazz yalikuwa katika kona ya mitaa ya Muhoro na Jangwani ambako
siku moja katika mwaka 1964 ilipiga muziki nje ya ofisi yao na kuwashangaza
watu kuona bendi ikipiga muziki mchana. Lakini wakati ikipiga dansi hilo nje
mchana kweupe, mipango kamambe ilikuwa ikipangwa katika maeneo hayo kwa
viongozi wanamapinduzi siku chache kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika
Januari 12. Viongozi walikuwa wakipanga mikakati ya mapinduzi yaliyouondoa
utawala wa Kisultani mwaka 1964 huko Zanzibar. Bendi ya Kilwa Jazz baadaye
haikueleweka na jamii. Wengine wakafika mbali wakizusha maneno kwamba ni bendi
ya serikali ‘eti’ ilikuwa ikialikwa kutoa burudani katika sherehe nyingi za
kitaifa.
Kilwa Jazz
pia ilialikwa kutoa burudani katika sherehe za ndoa ya Oscar Kambona, wakati
huo Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Tanganyika. Katika sherehe hiyo,
Ahmed Kipande alionyesha kipaji chake kwamba si cha kubahatisha. Alitunga wimbo
wa papo kwa papo wa kuwasifia wanandoa hao Oscar Kambona na mkewe. Yaelezwa
kwamba Kambona aliinuka kutoka kwenye kiti cha maharusi na kwenda kumkumbatika
Kipande kisha akamtunza kwa pesa.
Bendi hiyo
ya Kilwa Jazz ilikuwa chini ya udhamini mkubwa wa Mzee Nangwanda Lawi Sijaona,
ambaye anaelezewa kuwa alitoa mchango mkubwa wa hali na mali. Kilwa Jazz
ilikuwa na wanamuziki wenye vipaji tofauti. Walikuwepo ambao walikuwa wakipiga
ala za muziki zaidi ya moja pamoja na kuimba.
Ahmed
Kipande alikuwa kiongozi, mtunzi wa nyimbo, alikuwa akiimba pia alikuwa hodari
wa kupuliza ‘mdomo wa bata’ Saxophone. Duncan Njilima, Zuberi Makata na Hassan
Shabani ‘Kichwa’ (kaka mkubwa wa Ahmed Kipande) wote walikuwa na uwezo wa
kupiga gita la solo. Kwa upande wa saxophone walikuwepo akina Kisi Rajabu, Juma
Town na Abbas. Waimbaji alikuwa yeye Ahmed Kipande, Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’
na Kassimu Mapili. Gita la kati lilikuwa likiungurumishwa na Abdul Mngatwa
wakati drums zilikuwa zikicharangwa na Said na Abdallah Kanjo.
Upigaji
wao wa muziki ulikuwa ukiwakuna vilivyo viongozi wengi wa siasa na serikali,
ilifikia kiongozi mkubwa wa nchi wakati huo, Mzee Rashid Mfaume Kawawa alitoa
ofa ya suti kwa wanamuziki wote wa Kilwa Jazz.
Katika
maisha yake, Ahmed Kipande alifanikiwa kupata watoto sita.
Ahmed Mohammed
Kipande afariki dunia Aprili 27, 1987 baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa
kiharusi kwa kipindi kirefu. Alizikwa kwenye makaburi ya Tandika Maguruwe,
mkoani Dar es Salaam, Aprili 28, 1987.
Imeandaliwa
na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Ukinakili tafadhali taja chanzo hiki.
Comments
Post a Comment