- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Elisabeth Finant
Kuzaliwa: Novemba 9, 1954
Mahali: Kisangani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Kufariki: Septemba 9, 1994, Paris, Ufaransa
Elisabeth Jean
Finant (alizaliwa Novemba 9, 1954 mjini Kisangani, Mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo) alikuwa mwanamuziki wa Congo (zamani ikijulikana kama
Zaire) ambaye alifahamika zaidi kwa jina la Abeti Masikini.
Maisha yake ya awali
Elisabeth
Finat au Abeti Masikini alitokea katia familia tajiri yenye watoto nane. Baba
yake mzazi mzee Jean Finant, alikuwa chotara wa mchanganyioko wa Mkongo na Mbelgiji.
Mwaka
1961, Abeti Masikini alipatwa na pigo baada ya baba yake kuuawa kikatili mjini
Mbuji Mayi kutokana na matatizo ya kisiasa.
Mzee Finant alikuwa mwanachama wa
cha MLC, kilichokuwa kikiongozwa na hayati Patrice Emery Lumumba, Waziri Mkuu
wa kwanza wa Congo Leopoldville ambayo ndiyo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
ya sasa. Ndiye shujaa wa uhuru wa nchi hiyo.
Hali hiyo
ikamfanya mama yake Abeti Masikini kuchukua uamuzi wa kuhamia katika Jiji la
Kinshasa ili apate kujihifadhi akiwa na wanawe.
Wakiwa Kinshasa, mama yake
alimchukua Abeti Masikini na kumrejesha darasani kwenye shule iliyokuwa
ikijulikana kwa jina la Lycee Ycee Sacre Ceur, ambayo kwa sasa inaitwa
Bosongani.
Baada ya
kumaliza shule ya sekondari, Abeti Masikini aliajiriwa kama Katibu kwenye Ofisi
ya Waziri wa Utamaduni.
Hata hivyo, kwa mshangao wa ndugu zake na familia
nzima, Abeti Masikini aliamua kujiuzuru kazi hiyo na kuwaeleza nduguze kwamba mawazo
yake yalikuwa kwenye fani ya muziki, na ndio wakati alipojipachika jina la
‘Betty’ likiwa kifupi cha Elisabeth, ingawa mashabiki wake wakaamua kumwita
Abeti.
Mwaka 1971,
chini ya usimamizi wa mwanamuziki Gerard Madiata, palitokea mashindano ya
kumtafuta mwanamuziki chipukizi. Betty akaamua kushiriki kwenye mashindano
hayo, ambayo kwa bahati mbaya hakufanikiwa kufaulu.
Hilo halikumkatisha tamaa
kwani ilionekana kama hamu yake ya muziki iliongezeka Zaidi licha ya umri wake
kuwa mdogo wa miaka 17 wakati huo.
Ili aruhusiwe
kutumbuiza akiwa mnenguaji wa kujitegemea, ilibidi ajiongezee miaka mitatu
zaidi, ambapo alisema yeye alikuwa na miaka 20.
Akiwa anasaidiwa na kaka yake
Jean Aboumba Masikini aliyekuwa mpiga gitaa mahiri wa solo, Abeti akawa kila
siku anafanya onyesho kwenye vilabu vidogo vidogo jijini Kinshasa.
Mwaka huo
wa 1971, Abeti Masikini alikutana na Gerard Akueson jijini Kinshasa, raia wa Togo.
Hapo ndipo fani yake ya muziki ilipoanza rasmi. Gerard Akueson ndiye akawa
meneja wake mkuu tangu mwaka 1972. A
beti na Akueson wakaanzisha uhusiano wa mapenzi ingawa ndoa yao walifunga mwaka 1989 jijini Paris, Ufaransa ambaye walibahatika kupata watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume.
beti na Akueson wakaanzisha uhusiano wa mapenzi ingawa ndoa yao walifunga mwaka 1989 jijini Paris, Ufaransa ambaye walibahatika kupata watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume.
Mwaka 1973
mumewe huyo alimshauri wahamie katika nchi za Afrika Magharibi kwa matarajio ya
kupata mafanikio zaidi. Wakiwa huko alipata mashabiki wengi sana kwenye nchi za
Benin, Cote D’Ivoire, Togo, Niger, Nigeria, Guinea na Ghana.
Baada ya
miaka kadhaa akiwa kwenye nchi hizo, Abeti Masikini aliamua kurudi Congo.
Aliporejea mapokezi hayakuwa mazuri kwa kuwa watu wengi walikuwa hawamfahamu
kabisa. Kilichomponza zaidi ni kwamba, katika kipindi chote hicho hakuwahi
kurekodi hata albamu moja na kuiweka sokoni.
Changamoto
nyingine ilikuwa ushindani uliokuwepo hasa wa bendi kubwa kama T.P. O.K. Jazz,
Afrisa International, Zaiko Langa Langa, na nyinginezo na suala jingine ni
kwamba, wanamuziki wanawake, hususan wa kujitegemea, walikuwa hawajapata nafasi
ya kutosha wakati huo.
Lakini licha
ya kutofahamika kwake, aliamua kufanya onyesho kubwa katikati ya Jiji la Kinshasa
kwenye ukumbi wa CINE Palldium, lakini katika mshangao mkubwa aliambulia watu
12 pekee ambao ndio waliojitokeza kumuangalia. Tukio hilo halikumkatisha tamaa Abeti,
aliendelea kufanya kazi kwa bidii ili malengo yake yakamilike.
Hatua ya
kwanza aliyoifanya ni kufanya mazoezi kwa bidi ili kuboresha sauti yake. Baada
ya kufanya mazoezi makubwa hatimaye mwaka 1973 alifyatua album yake ya kwanza iliyokwenda
kwa jina la Pierre Cardin ikiwa na
nyimbo kadhaa zikiwemo Mutoto wangu,
Bibile, Aziza, Miwela na Safariet
Papy yaka. Album hiyo haikupokelewa vilivyo na wakazi wa jiji la Kinsahasa.
Machoni mwao walimchukulia Abeti kama mgeni huku mashabiki wengine wakimlaumu
kutokana na tabia yake ya kuimba nyimbo zake nyingi kwa lugha ya Kiswahili
badala ya Kilingala ama Kifaransa kama walivyofanya wanamuziki wengi.
Changamoto
hizo zikamfanya aunde kundi lake alilolipa jina la Les Redoutables ambalo
lilikuwa na wanenguaji wengi warembo na mahiri waliojulikana kama ‘Les
Tigresses’. Ni wanenguaji hao waliofanya watu wengi waanze kuvutiwa naye.
Maonyesho
yake katika Jiji la Kinshasa yakawa gumzo mitaani. Kazi alizokuwa akizifanya
meneja wake ambaye ndiye mumewe, zikazaa matunda mema. Alifanikiwa kupata
mkataba uliompeleka kwenda kufanya onyesho katika ukumbi maarufu wa Olympia
katika Jiji la Paris, Ufaransa.
Mwaka1973
akiwa njiani kuelekea Paris kwenye onyesho hilo, alitua kwanza katika Jiji la
Dakar nchini Senegal. Huko alifanya onyesho ambalo pia rais wa nchi hiyo wakati
huo Leopold Seadar Senghor alihudhuria. Pesa zilizopatikana katika onyesho hilo
alizitoa kama msaada wake kwa watu walioathiriwa kwa ukame nchini Senegal. Alipotua
jijini Paris Februari 2, 1973 aliporomosha onyesho kabambe lililowavutia hasa
mashabiki Wazungu kwenye ukumbi wa Olympia.
Abeti Masikini
alifanikiwa kufanya onyesho jingine Juni 6, 1974 kwenye ukumbi wa Carnegie, jijini
New York, Marekani.
Umaarufu
wake ulizidi kuongezeka pale alipopewa fursa ya kutumbuiza kwa pamoja katika
jukwaa moja na wanamuziki mahiri duniani kama James Brown, Miriam Makeba, Tabu
Ley na Franco Luambo Makiadi, kabla ya pambano la masumbwi la kihistoria kati
ya Mohammed Alli ‘Cassius Clay’ na George Foreman kwenye Uwanja wa Mei 26 jijini
Kinshasa, Congo, pambano ambalo linafahamika zaidi kama ‘Rumble in the Jungle’.
Albam yake
ya pili aliifyatua mwaka 1975 ikiwa na jina la La Voix Du Zaire. Nyimbo zilizokuwa zimesheheni katika albam hiyo
ni Likayabo, Yamba yamba, Kiliki, Bamba,
Nalikupenda na Ngoyaye.
Mwaka huo
huo Abeti alipokea mwaliko kutoka kwa Bruno Coquatrix aliyekuwa mmiliki wa
ukumbi wa Olympia wa jijini Paris. Akaenda kwa mara nyingine tena kufanya maonyesho
kwa siku mbili mfululizo. Ni wakati huo alipopachikwa jina la utani la ‘Tigeress
mwenye kucha za dhahabu’
Mwaka 1976
ulikuwa mbaya kimaslahi kwa Abeti Masikini. Alimpata mpinzani wa uhakika katika
muziki aliyejulikana kwa majina ya M’pongo Love, aliyekuja juu kuliko yeye. M’pongo
akaongoza Hit Parade kwenye radio ya taifa ya Zaire. Wimbo wake Pas Possible ulimfanya M’pongo kupendwa
mno na mashabiki.
Pamoja na
yote hayo, mwaka 1977 Abeti na M’pongo walifanya kitu ambacho hakikutarajiwa na
wengi. Walifanya onyesho kubwa kwa pamoja kwenye ukumbi wa ‘Cine Palldium’
katika Jiji la Kinshasa na kuacha simulizi kubwa. Kila mmoja aliimba kwa namna yake.
Wakaweka misingi mizuri ya kupendana kwa wanamuziki wa kike wa kizazi kijacho.
Historia
ya Abeti Masikini itaendelea kukumbukwa daima kwa kuwa yeye ni darasa tosha. Wanamuziki
wengi maarufu wamepitia kwenye bendi yake wakiwemo akina M’bilia Bel, aliyekuwa
mnenguaji toka 1976 hadi 1981, Lokua
Kanza aliyekuwa mpiga gitaa mwaka 1980 hadi 1981, Abby Surya aliyekuwa mnenguaji
mwaka 1984 hadi 1986 na Malage De Lugendo aliyekuwa mwimbaji.
Wengine walikuwa
wanenguaji Joƫlle Esso, Tshala Muana mwaka 1978 hadi 1979, Yondo Sister mwaka
1986 na Lambio Lambio ‘Komba Bellow’ mtaalamu wa kupiga kinanda.
Abeti Masikini
ni mmoja kati ya wanamuziki wa kike barani Afrika waliofanikiwa kujiwekea jina
kimataifa.
Alidhihirisha uwezo wa kipaji chake na kufahamika nchini Congo
ambako muziki umetawalia na wanaume.
Abeti pia
alikuwa mstari wa mbele kupigania haki za wanawake.
Alifariki
dunia Septemba 9, 1994 jijini Paris, Ufaransa, takriban miezi miwili kabla ya
kutimiza miaka 40.
Comments
Post a Comment