- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Shaaban Dede 'Super Motisha' a.k.a Kamchape enzi za uhai wake akiwa na Msondo Music Band.
“NANI kauona mwaka! Nani kauona mwaka! Ni
majaliwa yake Mungu eeeh, kuuona mwaka!...”
Haya ni mashairi
ya wimbo wa ‘Nani Kauona Mwaka’ uliotungwa na Shaaban Dede ‘Kamchape’ na
akauimba akiwa na bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra mwanzoni mwa miaka ya
2000.
Naam. Dede au
‘Super Motisha’ hatunaye tena. Mwanamuziki huyo mkongwe aliyejaaliwa kipaji cha
utunzi na uimbaji, amefariki dunia leo Alhamisi saa 2:00 asubuhi, Julai 6, 2017
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Dede, ambaye
anafahamika kwa utunzi wa tungo nyingi zilizosheheni ladha nzuri na maudhui
bora kwa jamii, alikuwa amelazwa kwa wiki mbili kwenye Wadi ya Mwaisela Namba 5
kutokana na kusumbuliwa na tatizo la mishipa ya damu.
Kifo cha
mwanamuziki huyo ambaye alikuwa akiitumikia Msongo Music Band kimewashtua
mashabiki wengi wa muziki nchini Tanzania, hasa baada ya kuelezwa hivi karibuni
kwamba hali yake ilikuwa ikiendelea vyema.
Hili ni pigo kwa
tasnia ya muziki wa dansi Tanzania, kwani Dede ni miongoni mwa wanamuziki
wakongwe waliosalia ambao walikuwa bado wanaendelea na muziki wa jukwaani.
Dede alizaliwa
Kanyigo, Bukoba mwaka 1954 ambapo alianza kuupenda muziki tangu akiwa mdogo kwa
vile wajomba zake walikuwa na bendi iliyofahamika kama Ryco Jazz.
Hata hivyo,
bendi yake ya kwanza kujiunga nayo ilikuwa ikimilikiwa na Chama cha TANU na
ilikuwa na maskani yake Biharamulo.
Mwaka 1974
alijiunga na Bendi ya Polisi Bukoba ambayo hakudumu nayo sana kwani mwaka 1975 alikwenda
kujiunga na Tabora Jazz ‘Wana Segere Matata’ iliyokuwa ikiongozwa na Shem
Ibrahim Kalenga.
Ni huko ndiko
alikoanza kufahamika na kutokana na umahiri wake katika uimbaji, hatimaye bendi
ya Dodoma International ikamnyakua mwaka 1976 ambako alidumu kwa miaka mitatu.
Shaaban Dede (kushoto) enzi zake akiwa na Hassan Rehani Bitchuka katika bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra.
Mnamo mwaka 1979
alijiunga na bendi ya Juwata Jazz ‘Wana Msondo Ngoma’ (sasa Msondo Music Band
ambayo alikuwa akiitumikia hadi mauti yalipomfika). Ikumbukwe kwamba, wakati
anakwenda Juwata, bendi hiyo ilikuwa imeondokewa na wanamuziki wake kadhaa
mahiri wakiwemo Muhidin Maalim Gurumo na mpiga solo Abel Baltazar ambao
walikwenda kuanzisha Mlimani Park Orchestra pale Mwenge Survey kabla bendi hiyo
haijachukuliwa na STC na baadaye DDC.
Baada ya kutamba
na wimbo wa Fatuma, alidumu na Juwata
hadi mwaka 1982 alipohamia Mlimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde Ngoma ya Ukae’,
lakini akakaa kwa mwaka mmoja tu kabla ya Shirika la Bima la Taifa
halijamchukua na kujinga na Bima Lee Orchestra ‘Wana Magnet Tingisha – Magnet
Ndele’ pamoja na akina Max Bushoke. Huko aliibuka na wimbo wa Shangwe ya Harusi.
Baadaye alikaa
kwa muda mfupi na bendi ya International Orchestra Safari Sound (OSS) “Wana
Ndekule’ iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabishara Hugo Kisima, ambapo alikuwa na
wamamuziki kama Maalim Gurumo, Hassan Rehani Bitchuka na mpiga solo Abel
Baltazar. Pamoja na kushiriki nyimbo nyingi, lakini aliibuka na wimbo wa Nyumba ya Mgumba haina Matanga.
Mnamo mwaka 1987
Wakati Bitchuka aliporejea Sikinde, Dede alirudi tena Juwata ‘Msondo Ngoma’
ambako lakini alikaa kidogo tu na kurejea tena Sikinde baada ya kufanyiwa
vitendo visivyo vya kiungwana na wanamuziki wenzake.
Ni hapo
aliporejea Sikinde ndipo akatunga wimbo wa ‘Talaka Rejea’ akilalamikia kitendo
hicho, ambapo anasema kwenye wimbo huo:
“Ulinitaliki kwa talaka rejeaaa....
Bila aibu ulininyang'anya nguo mbele za
watuuu...
Huku ukitoa kashfa, nikajifunze kwa
wazazi wangu...
Leo unaniambia nirejee kwako,
ulivyonidhalilisha umesahau...
Mtu anapochukiaaa, moyo kuurudisha
furahani ni vigumuuu...
Ukweli nasemaaaa, ni heri nipate tabu
kuliko kurejea kwakoooo...”
Kwa hakika,
tangu aliporejea Sikinde, Dede, akiwa na wanamuziki wengine mahiri kama Francis
‘Nasir’ Lubua, Hassan Kunyata, Hussein Jumbe Totoro ‘Mzee wa Dodo’ na wengineo
waliweza kuiimarisha bendi hiyo na kuleta ushindani mkubwa dhidi ya wapinzani
wapo Msondo.
Ushindani huo
ulifanya muziki wa dansi ukue na kuimarika kiasi kwamba kumbi za DDC na Amana
zilikuwa hazikauki mashabiki kila bendi hizo zilipokuwa zikitumbuiza.
Mnamo mwaka
2011, Dede akaamua kujiunga tena na Msondo ikiwa ni mara yake ya tatu, na
safari hii aliweza kufanya kazi nzuri akishirikiana na wanamuziki wengine
wakongwe wakiwemo akina Said Mabera.
Mwenyezi Mungu
aiweke roho ya marehemu Dede mahali pema. AMEN!


Comments
Post a Comment