- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Jovina Bujulu-
MAELEZO
Serikali
imewataka wachapishaji wote nchini waliojiandikisha kwa Msajili wa Makampuni (BRELA)
na Mamlaka ya Mapato (TRA), kufika
katika ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ili wajiorodheshe na
watambuliwe na Serikali na wananchi kabla ya Machi 30 mwaka huu.
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mpiga
Chapa Mkuu wa Serikali ndugu Cassian Chibogoyo alipokuwa akizungumzia kuwepo
kwa wimbi kubwa la wachapishaji hewa nchini.
Chibogoyo
amesema kuwa hatua hiyo inafuatia uwepo wa utitiri wa wachapishaji ambao
hawatambuliki na Serikali, kwa sababu baada ya kujiandikisha kwa mamlaka husika
kama kampuni, utawakuta wana mitambo ya uchapishaji ambayo mara nyingi
wanaitumia kuchapisha nyaraka bandia za Serikali bila kuwa na kibali kutoka
katika mamlaka yenye dhamana ya uchapishaji.
“Kwa sasa tumeanzisha utaratibu maalum wa
kuwatambua wachapishaji ambapo wanatakiwa kujiorodhesha kwa Mpiga Chapa Mkuu wa
Serikali, hii ni kutokana na kuwepo kwa uchapaji holela na bandia wa nyaraka za
Serikali” alisema Chibogoyo.
Aliongeza
kuwa chini ya utaratibu uliowekwa sasa wachapishaji wanatakiwa kuwasilisha
nyaraka halali za kampuni, shughuli wanazofanya, historia ya kampuni na mahali
kampuni inapofanyia kazi zake.
Adha,
Chibogoyo alisema kuwa faida za wachapishaji kujiandikisha ni pamoja na
kutambuliwa kisheria na Serikali ili hata wanaposhutumiwa waweze kulindwa na
Serikali, kukumbushana majukumu yao , wigo wao wa kazi, na pia wataelimishwa
kuhusu nyaraka wanazopashwa kuchapisha maana si kila nyaraka wanapashwa
kuzichapisha.
Zaidi
ya hayo, Chibogoyo alitaja madhara ya kuchapisha nyaraka bandia kuwa ni pamoja
na kuikosesha Serikali mapato kutokana na uchapishaji wa stakabadhi mbalimbali
bandia, uvamizi wa mawasiliano ya Serikali uchapishaji wa vyeti vya usajili wa
makampuni, na uchapishaji bandia wa vyeti vya elimu ambavyo hupelekea mtu
kuajiriwa kwa kazi ambayo hana ujuzi nayo.
Akizungumzia
hatua ambao zinaweza kuchukuliwa dhidi ya wachapishaji wa nyaraka bandia, Chibogoyo
alisema kuwa ni pamoja na kutaifisha mitambo ya wahusika.
Akizungumza
suala hilo hivi karibuni katika kipindi cha “Tujikumbushe”, Chibogoyo alisema
kuwa makosa ya uhalifu wa nyaraka bandia yanaangukia katika sheria za ushahidi,
sheria ya makosa ya jinai, sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 1970, pamoja na
sheria ya nembo na alama za Taifa.
Mpiga
Chapa huyo Mkuu wa Serikali alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali
kupambana na vita hii kwa kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi ili
kutokomeza janga hilo.
“Tunawaomba
wananchi tuwe na mshikamano katika kufichua janga hili la uchapishaji holela na
bandia kwani ni janga la kitaifa, linagusa maslahi ya nchi na wananchi,
nalifananisha na ujambazi wa hali ya juu” alisisitiza Chibogoyo.
Baadhi
ya nyaraka ambazo zimekuwa zikighushiwa mara kwa mara ni pamoja na vyeti vya
elimu katika ngazi mbalimbali, risiti za serikali, vyeti vya kuzaliwa na ndoa,
kadi za magari na pikipiki, mihuri na nembo ya Taifa.
MWISHO.

Comments
Post a Comment