- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni (kushoto) akizungumza na mamia ya Wananchi wa Kijiji cha Bungu, Wilaya
ya Kibiti, mkoani Pwani. Masauni alifanya ziara katika Wilaya hiyo kwa lengo
kuangalia hali ya usalama wa Wilaya ya Rufiji, Kibiti na Mkuranga ambapo
alizungumza na askari polisi wanaolinda usalama katika maeneo hayo na baadaye
alizungumza na wananchi na kuwaomba kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi bila
woga ili waweze kuwasambaratisha wahalifu katika maeneo hayo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni (wapili kulia) akimsikiliza Mkazi wa Kijiji cha Bungu, Wilaya ya
Kibiti, mkoani Pwani, Ayubu Mketo alipokuwa anamuuliza swali kuhusiana na hali
ya usalama katika eneo lao la Bungu. Hata hivyo, Masauni aliwahakikishia
usalama wananchi wa Wilaya hiyo pamoja na ya Rufiji na Mkuranga, kuwa askari
wake wameweka kambi kwa ajili ya kupambana na wahalifu pamoja na kuwalinda
wananchi wa maeneo hayo. Masauni alifanya ziara katika maeneo hayo ambapo
alizungumza na polisi pamoja na wananchi kuhusu kushirikiana na Jeshi la Polisi
bila woga ili Jeshi hilo liweze kupambana na wahalifu kikamilifu. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Na Felix
Mwagara/MOHA
NAIBU
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amewataka wananchi wa
Wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani kuwapa taarifa za matukio ya
uhalifu Jeshi la Polisi bila woga wowote ili Jeshi hilo liweze kuwasambaratisha
wahalifu katika maeneo hayo.
Masauni
alisema Jeshi hilo ili liweze kufanikiwa katika mapambano yake na wahalifu
katika maeneo hilo, nguvu ya wananchi inahitajika sana katika utoaji wa taarifa
ya matukio hayo.
Akizungumza
na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Bungu wilayani Kibiti, Masauni alisema Jeshi
lake limejipanga kikamilifu kwa kupambana na wahalifu na litahakikisha wahalifu
hao wanakamatwa wote ili wakazi wa maeneo hayo kuendelea kufanya shughuli zao
za kuijenga nchi kama kawaida bila wasiwasi wowote.
Aliongeza
kuwa, ili jeshi hilo lifanikiwe zaidi katika mapambano hayo linahitaji msaada
wa kupata taarifa ya wahalifu hao kwa kuwa baadhi ya wananchi wanawajua
wahalifu hao lakini wanaogopa kutoa taarifa kwa polisi wakiwa na wasiwasi wa
kuja kuvamiwa endapo ikijulikana.
Masauni
aliwahakikishia usalama endapo watatoa ushirikiano kwa Jeshi hilo kwani umakini
utakuwepo na hakuna mwalifu atakaye jua kuwa Jeshi hilo limepewa taarifa
zozote, kwani kitendo cha kuto kuripoti taarifa ya wahusika hao ni hatari kwa
usalama wa wananchi hao kwani huwezi kujua majambazi hayo yanaweza yakaja siku
yoyote kuwavamia wananchi hata kama hawakuhusika kutoa taarifa zozote hivyo
njia ya busara kushirikiana na polisi ili Jeshi hilo liweze kufanya kazi yake
ya kupambana nao na kuleta usalama zaidi.
“Nchi
yetu ni ya amani, na Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuleta maendeleo kwa
wananchi wake, kama mnavyoona viwanda vinajengwa, na pia mnaendelea kufanya
shughuli zenu kwa amani kabisa, sasa ili amani hii iweze kudumu, mnatakiwa
kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pale ambapo mnakuwa na taarifa na
wasiwasi na mtu yeyote katika maeneo yenu ambaye hana nia nzuri na usalama wenu,”
alisema Masauni.
Alisema
Jeshi la Polisi halipaswi kuogopwa na raia mwema, Jeshi hilo ni rafiki kwa kila
Mtanzania mwema ambaye ana uzalendo wa dhati na nchi yake, Jeshi ni rafiki ya
wananchi, hivyo wananchi wanapaswa kuwa karibu na Jeshi kwa kuwa hao ndio
walinzi wa wananchi pamoja na mali zao.
Aidha,
Masauni aliwataka wananchi wa maeneo hayo kufuata sheria ili waweze kuishi kwa
amani na ushirikiano na endapo watafanya makosa basi jeshi hilo litawakamata
wale wote watakaovunja utaratibu mzuri wa kuishi ikiwemo wale wanaoendesha
bodaboda bila kofia ngumu.
“Jeshi
halionei mtu, na endapo mtaonewa tafadhali nipeni taarifa kwa njia ya simu au
mpigieni msaidizi wangu, na pia mnaweza mkawasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Pwani, ili shida zenu, kero, malalamiko yote ambayo yapo kinyume na sheria
wanayoyafanya baadhi ya polisi wetu wasiokuwa waaminifu tuyajue na kuyafanyia
kazi kwa dakika chache,” alisema Masauni.
Kabla ya
kufunga mkutano huo na kuendelea na ziara yake katika mikoa ya Lindi na Mtwara,
Masauni alitoa namba zake za simu ya mkononi kwa wananchi hao pamoja na ya
msaidizi wake, pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani pamoja na wa Wilaya nao
walitoa namba zao kwa ajili ya mawasiliano na wananchi hao.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni akizungumza na askari Polisi wanaolinda usalama katika Wilaya ya
Kibiti, Rufiji na Mkuranga ambao wameweka Kambi katika Wilaya ya Kibiti kwa
lengo la kupambana na wahalifu katika Wilaya hizo. Masauni pia alizungumza na
mamia ya wananchi wa Kijiji cha Bungu na kuwahakikishia usalama wao na pia
aliwataka kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili waweze kuwasambaratisha
wahalifu hao kwa uharaka zaidi. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni
(kushoto), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani (RPC), Onesmo
Lyanga wakiwasili Kituo cha Polisi Bungu, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
Masauni alifanya ziara katika Kituo hicho na alizungumza na askari Polisi
wanaolinda amani katika eneo hilo na pia alizungumza na wananchi ambapo aliwataka watoe
ushirikiano kwa Jeshi hilo katika mapambano ya kuwasambaratisha wahalifu
mbalimbali waliopo Wilaya ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani humo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
************************************
************************************
Comments
Post a Comment