- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ruangwa
mkoani Lindi pamoja na Wakuu wa Vyombo vilivyo chini ya Wizara yake mkoani
humo. Katika mzungumzo hayo, Masauni
aliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuanzisha Kituo cha Zimamoto wilayani
hapo kuanzia mwezi Aprili mwaka huu pamoja maandilizi ya Ujenzi wa Kituo kipya
cha Polisi wilayani humo. Picha zote na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuanzisha kituo
cha zimamoto Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Masauni alisema Aprili Mosi mwaka huu
Jeshi hilo litakuwa na ofisi wilayani humo ili askari wa Jeshi hilo waanze
kutoa huduma sehemu mbalimbali ya Wilaya hiyo ambayo ni muhimu kituo hicho
kuwepo kutokana na uwepo na machimbo ya madini ya dhahabu pamoja na mji kuendelea
kukua kwa kasi.
“Tumekubaliana vizuri baada ya Kamanda
wa Zimamoto mkoa kuwa ifikapo tarehe moja askari wa zimamoto watakuwepo hapa
Ruangwa rasmi kwa ajili ya kuanza kazi, na watapewa ofisi na halmashauri ya
Wilaya, hivyo utaratibu wa kupata vifaa vya awali uanze mara moja kama
tulivyokubaliana,” alisema Masauni.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi hilo
Mkoa wa Lindi, Christina Sunga alimuhakikishia Naibu Waziri pamoja na Watendaji
wa Wilaya hiyo, agizo hilo atalifanyia kazi haraka iwezekanavyo na mpaka
ifikapo Aprili mosi mwaka huu tayari askari wawili watakuwa wameripoti mjini
Ruangwa.
“Uwepo wa askari hawa kutarahisisha kwa
kiasi kikubwa kutoa elimu kwa umma jinsi ya kuzima moto pamoja na kupambana na
uzimaji moto, licha ya kuwa tunakuwa na vifaa vya awali vya uzimaji moto mpaka
hapo tutakapopata gari kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uzimaji moto na
utoaji elimu zaidi,” alisema Sunga na kuongeza;
“Tunashukuru Halmashauri ya Wilaya ya
Ruangwa kwa kutupa ofisi kwa ajili ya askari wa zimamoto lakini pia kutuwezesha
kupata vifaa hivyo vya awali vya uzimaji wa moto.”
Aidha, Masauni alimuagiza Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Lindi, (RPC) Renatha Mzinga kuandaa mchoro pamoja na gharama ya
ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi cha Wilaya ya Ruangwa ili ujenzi huo uanze.
“Nimekagua eneo la ujenzi wa kituo
kipya cha polisi, eneo zuri na linafaa kwa ujenzi wa kituo kikubwa cha polisi,
maandalizi tayari yameanza na hivi karibuni RPC atakamilisha mchoro pamoja na
gharama ya ujenzi wa kituo hicho hapa Ruangwa,” alisema Masauni.
Pia Masauni amesema Wizara yake
itahakikisha inawajengea ofisi Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(Nida) pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani humo ambapo kwasasa
ofisi hizo zipo katika jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni akimpa maelekezo Fundi Mkuu wa ujenzi wa Gereza Ruangwa (kushoto)
wakati Naibu Waziri huyo alipofanya ziara ya kukagua ujenzi huo unaoendelea
mjini Ruangwa. Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Lindi, Tusekile
Mwaisabila. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ruangwa, Joseph
Kiyengi wakati alipokuwa akionyesha eneo litakalojengwa Kituo kipya cha Polisi
wilayani humo. Maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho yameshaanza. Katika ziara
yake Masauni pia aliagiza uanzishwaji wa Kituo cha Zimamoto wilayani humo
haraka iwezekanavyo. Katikati ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Twaha Mpembenwe.
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi
Hamad Masauni (katikati) akimsikiliza Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya
Ruangwa, Joseph Kiyengi alipokuwa anatoa taarifa yake katika Kikao cha Wajumbe wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ruangwa ambacho kilijumuisha Wakuu wa
Vyombo vilivyo chini ya Wizara hiyo mkoani Lindi. Katika mzungumzo hayo, Masauni aliagiza Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji kuanzisha Kituo cha Zimamoto wilayani hapo kuanzia mwezi
Aprili mwaka huu pamoja maandilizi ya Ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi wilayani
humo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi.
Comments
Post a Comment