- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Diwani wa Kata ya Magulilwa wilayani Iringa, Ernest Kasike, akiwaonyesha waandishi wa Kwanza Jamii bwawa lililojengwa chini ya kiwango.
Na Daniel Mbega, Iringa
JUMLA ya ekari 400 zililengwa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Kata ya
Magulilwa zimekwama kwa miaka saba sasa kutokana na ufisadi uliofanyika wakati
wa ujenzi wa bwawa la maji.
Taarifa za uchunguzi zinaeleza kwamba, bwawa hilo lililojengwa katika
Kijiji cha Magulilwa mwaka 2009, lililenga kuwanufaisha wakazi 13,639 wa kata hiyo – wanaume 6,663 na wanawake 6,976 – wakazi wa vijiji
vitatu kati ya sita (6) vinavyounda kata hiyo, ambao walidhani mradi huo
ungewakomboa kiuchumi.
Vijijini
ambavyo vingenufaika moja kwa moja na mradi huo ni Magulilwa, Ng'enza na
Mlanda. Vijiji vingine vya kata hiyo ni Ndiwili, Negabihi na Msuluti.
“Ndoto hizo
za kilimo cha umwagiliaji zimetoweka, achilia mbali huduma nyingine za kijamii
ikiwemo josho la kuogeshea mifugo hapa kijijini, ambalo limejengwa lakini si
katika kiwango na ufanisi uliotakiwa,” anaeleza Isidory Mwakikoti, mkazi wa
kijiji hicho.
Mwakikoti anasema kwamba, kwa takriban miaka saba sasa, bwawa hilo limeshindwa
kufanya kazi baada ya kujengwa chini ya kiwango licha ya kugharimu Shs. 47
milioni.
Uchunguzi wa Fikra Pevu umebaini kwamba, fedha zilizotumika kwenye
ujenzi wa bwawa hilo zilitoka kwenye Mradi
Shirikishi wa Maendeleo ya Kilimo na Uwezeshaji (Padep – Participatory Agricultural Development and Empowerment
Project), Halmashauri ya Wilaya pamoja na nguvu ya wananchi.
Aidha, mradi
huo wa bwawa la Magulilwa ndio uliokuwa pekee kwa Mkoa wa Iringa kati ya miradi
69 ya malambo na visima iliyofadhiliwa na Padep nchi nzima tangu mwaka 2004
ambapo hadi mwaka 2007 yalikuwa yamegharimu jumla ya Shs. 3,003,785,439.
Mikoa mingine
na idadi ya malambo ikiwa kwenye mabano ni Arusha (5), Kilimanjaro (1), Manyara
(28), Tabora (2) na Singida (32).
“Usimamizi
mbovu ndio uliofanya bwawa hili lijengwe kienyeji na chini ya kiwango licha ya
kutumia fedha nyingi, lakini hili ndilo lingekuwa mkombozi mkubwa wa wananchi
wa Magulilwa kiuchumi kwa sababu kuna eneo kubwa la bonde kwa ajili ya kilimo
cha umwagiliaji,” alisema Ernest Kasike, Diwani wa Kata ya Magulilwa kupitia Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Diwani huyo alisema, hata miundombinu ya
bwawa hilo ikiwemo mifereji, ni mibovu hali ambayo inazua maswali mengi hasa
kuhusu suala la usimamizi wa miradi ya jamii pamoja na fedha za umma.
“Serikali imepanga kulijenga upya ingawa
bado upembuzi yakinifu haujafanyika ikiwa ni pamoja na kujua gharama za ujenzi
huo.
“Tumeambiwa kwamba inabidi wayakaushe
maji yote yaliyoko bwawani na kuanza ujenzi, lakini hawajasema gharama zake
zitakuwa kiasi gani,” alisema na kuongeza kwamba tayari bwawa hilo lilikuwa
limeanza kuzalisha samaki kwa wingi pamoja na kufuga bata maji.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Magulilwa,
Majeshi Richard Ndambo, alisema wanufaika wa mradi wa bwawa hilo ni wengi kwa
maana endapo litakamilika kuna ekari 400 zitakazotumika kwa kilimo cha
umwagiliaji.
Alisema ekari hizo ni kati ya ekari 600
zinazofaa kwa umwagiliaji katika kata nzima, ambapo kwa sasa zinazolimwa ni
karibu 200 tu.
“Tunaamini kama bwawa hili litakapokamilika
na kuanza kutumika wananchi wengi wa kata hii watanufaika na watakuwa na kilimo
endelevu cha masika na kiangazi, kwa sababu maeneo ni mengi yanayofaa kwa
kilimo hicho,” alisema.
Hata hivyo, wananchi wengi wanaendelea
kulima nyanya, maharage, pilipili hoho, bamia na njegere kwenye eneo lisilozidi
ekari 50 katika bonde hilo wakitegemea zaidi unyevunyevu.
“Kama maji yangekuwepo hali singekuwa
hivi, naamini mazao yangestawi vizuri kwa sababu wangeyamwagilia,” anasema Ndambo.
Ndambo anasema, kukamilika kwa bwawa hilo
kungewanufaisha pia wafugaji, kwani wangeyatumia maji hayo pia kwa ajili ya
josho lao la kuogeshea mifugo lililoko kijijini hapo.
Kwa sasa, anasema, wanapata maji kwa
shida kwani wanalazimika kujaza maji kwa kuteka kwa ndoo kutoka umbali mrefu.
Miundombinu duni ya kilimo cha
umwagiliaji inakwamisha kwa kiasi kikubwa uzalishaji huku wananchi wengi
wakitegemea zaidi visima vya kienyeji.
Diwani Kasike alisema kwamba, ni muhimu kuhakikisha
miundombinu bora inajengwa kwenye bonde linalotegemea uwepo wa bwawa hilo na
hata bonde lililo kando kando ya Mto Ruaha.
Ofisa Mifugo na Kilimo wa Kata ya
Maguliwa, Shaaban Ngwenga, alisema wananchi wa kata hiyo wanalima zaidi mahindi
na maharage huku mahindi yakipewa kipaumbele zaidi ambayo hulima kwa ajili ya chakula
na biashara, hususan mahindi mabichi, maarufu kama ‘gobo’.
“Tumepanga program ya kila mkulima awe na
ekari tatu, ili ekari mbili azitumie kwa gobo na moja kwa ajili ya chakula,”
anasema Ngwenga.
Miradi ya
umwagiliaji
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuna miradi
mbalimbali ya kilimo cha umwagiliaji ambapo mmojawapo ni mradi wa Bwawa la Maji
la Mkungugu ambalo limekuwa mkombozi kwa wananchi wa Kijiji cha Mkungugu na
vijiji vya Kising’a na Uhominyi katika Kata ya Kising’a, katika Tarafa ya
Ismani.
Tarafa ya Isimani kwa miaka mingi inakabiliwa na
ukame hata wakati wa masika kwa kukosa mvua za kutosha, hivyo kusababisha
wananchi wengi kukabiliwa na njaa kila mwaka kutokana na kutegemea kilimo cha
msimu ambacho nacho kimekuwa cha mashaka.
Kilimo cha umwagiliaji kinaweza kutoa taswira mpya
ya ukombozi wa kiuchumi kutokana na kuwepo kwa bwawa hilo, ambalo inaelezwa
kwamba limegharimu kiasi cha Shs. 1.2 bilioni hadi kukamilika.
Mbali ya kilimo, lakini kujengwa kwa bwawa hilo
kutaondoa shida ya maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo huku pia likitumika
kwa shughuli za uvuvi na samaki.
“Tumeanza kuvua samaki ingawa siyo wengi, lakini si
haba, wanapatikana wa kitoweo,” anasema Simon Muhema, mvuvi ambaye pia ni mwenyekiti
wa Kamati ya Maji ya Kijiji.
Muhema anasema, kuwepo kwa bwawa hilo kumemfanya
arejee kijijini hapo baada ya kutumia muda mwingi akivua samaki katika Bwawa la
Mtera, ambako ameshuhudia wenzake wengi wakipoteza maisha na viungo kutokana na
kujeruhiwa na mamba bwawani humo.
“Muda mwingi nimekuwa nikivua Mtera, lakini matukio
ya mamba kujeruhi na hata kuua wavuvi yamenifanya nije nipumzike huku nyumbani.
Nashukuru wakati nakuja na serikali nayo imetujengea bwawa hili,” anasema.
Mradi mwingine ni ule wa Skimu ya Umwagiliaji Mlambalasi katika Kijiji cha Kiwere
wilayani humo, inayofadhiliwa na serikali na tayari imekwisha onyesha ukombozi
kwa wananchi wa maeneo hayo tangu mwaka 2013 ulipokamilika, ambapo
unawanufaisha wakulima kutoka kaya 1,000.
Mradi huo wa umwagiliaji kwenye eneo la
hekta 500 (takriban ekari 1,250), ambao ni sehemu ya utekelezaji wa kauli mbiu
ya serikali ya ‘Kilimo Kwanza’, ni wa pili katika Kijiji cha Kiwere, ambapo wa
kwanza uliopo pembezoni mwa kijiji hiyo umekwishazaa matunda hasa kwa kilimo
cha nyanya, mpunga, mahindi na bamia.
Ofisa Msimamizi wa Mradi, Joseph Hango, alisema
ujenzi wa mfereji wa skimu hiyo wenye urefu wa kilometa 6.5, ukitokea katika
Mto Ruaha, uligharimu Shs. 700 milioni.
“Awamu ya kwanza zilitumika karibu Shs. 400
milioni na awamu ya pili zilitumika Shs. 300 milioni ambazo zote zilitolewa na
Serikali Kuu,” alisema Hango.
Hango anaongeza kwamba, endapo hekta zote
500 za umwagiliaji zitalimwa mpunga, kuna matarajio ya kuvuna wastani wa tani
2,500 kwa awamu moja, hivyo kuondoa tatizo la njaa.
Mfereji huo wenye ukubwa wa meta moja una
uwezo wa kupitisha meta moja ya ujazo ya maji kwa sekunde (sawa na lita 1,000
kwa sekunde), kiwango ambacho kitatosha kumwagilia hekta 500 kwa uhakika.
Taarifa zinaeleza kwamba, mpango uliopo wa serikali
ni kuhakikisha mfereji huo unajengwa hadi katika eneo la Muhunga, kiasi cha
kilometa 18 kutoka yalipo maingilio ya mfereji huo kwenye Mto Ruaha.
Hata hivyo, mradi wa bwawa
la umwagiliaji katika Kata ya Mgama ambao ulipaswa wakulima takriban 3,000 wa
vijiji vya Ibumila na Mgama umekwama baada ya kujengwa chini ya kiwango.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Mgama, John Kitime, anasema ujenzi wa bwawa hilo ulianza mwaka
2012 ulikuwa ukamilike mwaka 2015, lakini kwa kuwa ulijengwa chini ya kiwango
ukingo wote wenye urefu wa meta 200 ukasombwa na maji.
Mradi huo
ulikuwa unajengwa na kampuni ya GNMS Contractors Co. Limited ya mjini Iringa, inayomilikiwa
na William Mungai.
Ofisa
Mtendaji wa Kata ya Mgama, William Msofu, alisema kukamilika kwa bwawa hilo kungeongeza
tija kutokana na kilimo cha umwagiliaji hasa kwa mazao ya mboga mboga.
Alisema
mashamba mengi ambayo yamekuwa yakitegemea mvua za masika yangebadilika na kuwa
ya umwagiliaji katika majira yote ya mwaka, kwani uhakika wa kupatikana kwa
maji ungekuwepo.
“Wakulima
wengi wa Mgama wanalima nyanya, lakini wanategemea zaidi mvua za masika, ikiwa
bwawa litakamilika, basi kilimo chao kitakuwa endelevu katika majira yote ya
mwaka.
Usalama wa chakula
Idadi kubwa ya wakazi wa Wilaya ya Iringa
Vijijini, hususan Tarafa ya Isimani, kwa miaka mingi wamekuwa wakikumbwa na
uhaba wa chakula kutokana na ukosefu wa mbinu bora za kilimo pamoja na ukame.
Serikali
inaendelea na utaratibu wa kugharimia miradi ya Umwagiliaji kupitia Programu ya
Kilimo Endelevu (ASDP) ambapo miradi inaibuliwa na kuwekwa katika Mipango ya
Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADP) na kuombewa fedha katika Mfuko wa
Maendeleo ya Umwagiliaji ngazi ya Wilaya (DIDF) kwa miradi midogo na ngazi ya
Taifa (NEDF) kwa miradi mikubwa.
Kwa upande mwingine, Mfuko wa Maendeleo ya Hifadhi ya Jamii (Tasaf) nao
umejitahidi kutatua kero ya maji kwenye Tarafa ya Ismani ambapo kwa mwaka 2011 ulitenga
Shs. 102 milioni ili
kujenga mabwawa matatu katika vijiji vitatu vya Kata ya Nyang'oro kwa lengo la
kuwawezesha wananchi katika vijiji husika kupata maji kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani, kunywesha mifugo, umwagiliaji wa bustani na kusaidia katika ujenzi wa
nyumba bora na kuwaondolea kero ya usumbufu wa kufuata maji umbali mrefu.
Mratibu wa
Tasaf katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Christopher Kajange
alikaririwa mwaka 2013 akivitaja vijiji ambavyo vingenufaika na kuchimbiwa
mabwawa katika tarafa ya Isimani kuwa ni Mangawe, Ikengeza na Mawindi.
Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Iringa, Lucy
Nyalu, alisema, program za umwagiliaji zinaendeshwa wilayani humo na kwa sasa
kuna skimu 30 za jadi, miongoni mwazo 13 zimekarabatiwa yakiwemo mabwawa.
Alizitaja baadhi ya skimu hizo kuwa ni
Tanangozi na Igingilanyi kwenye umwagiliaji wa matone, Mlenge, Magozi, Kiwere,
Mlambalasi, Cherehani-Mkoga, Ipwasi-Ndorobo, Tungamalenga, Wangama na
Ilolompya, wakati ambapo mabwawa yaliyojengwa na yanayoendelea kujengwa ni
Mkungugu, Mgama, Ulongambi, Ikengeza, Nyang’oro na Malengamakali.
Mradi wa umwagiliaji wa Igingilanyi umetumia kiasi
cha Shs. 1 bilioni ambapo jumla ya hekta 15 zinalimwa mazao mbalimbali.
Nyalu alisema, miradi ya Idodi na Nyang’oro
ni ya uchimbaji mabwawa, ambapo jumla ya Shs. 6.5 bilioni zilikuwa zinahitaji kuweza
kuikamilisha.
“Jumla ya hekta 43,000.7 zimeainishwa kama
maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji lakini kwa sasa tuna eneo la hekta 21,000 tu
linalotumika ambalo linawanufaisha wakulima zaidi ya 40,000. Changamoto kubwa
inayotukabili ni fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya
umwagiliaji,” aliongeza Nyalu.
Mwaka 2011, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ilitenga Shs. 24 bilioni kwa ajili ya miradi ya
maendeleo, ikiwa ni pamoja na kugharimia ujenzi wa skimu za umwagiliaji
katika Vijiji vya Kiwere,
Tungamalenga, Ipwasi-Ndorobo na Cherehani-Mkoga.
Mkurugenzi wa zamani wa Halmashauri ya Iringa Vijijini,
Pudenciana Kisaka, alikaririwa wakati huo akisema miradi iliyoibuliwa na
wananchi na kusaidiwa fedha na Tasaf ni ujenzi wa mifereji mitatu katika Kata
ya Idodi, Kijiji cha Mfyome na Kata ya Kiwere.
“Mifereji mitatu ya Kata ya Idodi imejengwa katika vijiji vitatu ambapo ujenzi wake umegharimu jumla ya Shs. 107,537,008,” alisema.
“Mifereji mitatu ya Kata ya Idodi imejengwa katika vijiji vitatu ambapo ujenzi wake umegharimu jumla ya Shs. 107,537,008,” alisema.
Alifafanua kwamba, katika Kijiji cha Mahuninga mfereji uligharimu
Shs. 35,762,568, katika Kijiji cha Makifu ujenzi wa mfereji uligharimu Shs.
35,982,522 na katika Kijiji cha Idodi ujenzi uligharimu Shs. 35,793,918.
0656-331974
CHANZO: FIKRAP
Comments
Post a Comment