- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri Ummy Mwalimu
TAMKO LA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO MHE. UMMY MWALIMU (MB) KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA
SIKU YA UKOMA DUNIANI TAREHE 29/01/2017
Ndugu wanahabari na wananchi
“Siku ya Ukoma Duniani” huadhimishwa kila mwaka,
Jumapili ya mwisho wa mwezi Januari. Mwaka huu maadhimisho yanafanyika tarehe 29
Januari 2017. Siku hii iliasisiwa na
mwandishi wa habari mfaransa, Raoul Follereau aliyetumia muda wake mwingi
kuzunguka dunia kueleza hali duni ya maisha ya watu walioathirika na ugonjwa wa
ukoma.
Lengo kuu la
kuadhimisha siku hii ni kuukumbusha umma wa watanzania kuwa sote tunao wajibu
wa kushiriki kikamilifu katika vita ya kupambana na ugonjwa wa ukoma nchini.
Siku hii ni muhimu kwa jamii kukaa kitako na kutafakari madhara na shida
zinazotokana na maradhi ya ukoma. Tatizo kubwa la ugonjwa huu ni kuvishambulia
viungo vya mwili wa binadamu na kusababisha kukatika viungo na hivyo kupelekea ulemavu
wa kudumu ambao ndio hasa huutambulisha ugonjwa huu kuliko hata dalili zake.
Ndugu
wananchi na wanahabari
Maadhimisho ya Siku
ya Ukoma Duniani yanatupa fursa kama nchi kujitathmini na kuangalia harakati
zetu katika kuutokomeza kabisa ugonjwa wa ukoma katika Taifa letu. Kimsingi, napenda
kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kuwa ukoma
bado upo hapa nchini kwetu na hivyo basi tuna wajibu wa kukabiliana nao. Takwimu
zinatuonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutokomeza ugonjwa
huu kutoka kiwango cha utokomezaji cha watu 0.9
kati ya watu 10,000 mwaka 2006 na kufikia kiwango cha watu 0.4 kati ya watu 10,000 mwaka 2015. Kwa
maana nyingine katika kila watanzania
10,000 kiwango cha watu wenye ugonjwa wa ukoma sasa ni watu 0.4 mwaka 2015
kutoka wastani wa wagonjwa 0.9 katika watu 10,000 mwaka 2015. Haya ni mafanikio
makubwa sana kwa sababu kiwango cha kimataifa cha utokomezaji ukoma
kinatakiwa kuwa chini ya mgonjwa 1
katika watu 10,000.
Ndugu
wananchi na wanahabari
Japokuwa mwelekeo
wetu kama nchi unaonyesha tunapiga hatua nzuri, bado kuna wilaya na mikoa ambayo bado tatizo la ukoma lipo juu na watu wengi
wanazidi kuathirika. Mikoa na wilaya ambazo bado zina wagonjwa wengi wa
ukoma ni Lindi (Lindi Manispaa, Liwale, Lindi
na Ruangwa), Morogoro (Halmashauri ya Ulanga, Kilombero na Mvomero), Dar es
Salaam (Manispaa ya Temeke na Kigamboni), Tanga ( Halmashauri za Muheza,
Mkinga na Pangani), Mtwara (Halmashauri
ya Nanyumbu na Newala), Rukwa (Halmashauri ya Nkasi), Pwani (Halmashauri ya
Rufiji na Mkuranga), Geita (Halmashauri ya mji Geita na Halmashauri ya Chato),
Tabora (Halmashauri ya Sikonge), Mwanza (Halmashauri ya Kwimba na Misungwi), na Ruvuma (Halmashauri ya Songea na Namtumbo).
Mikoa na halmashauri hizi haina budi kuongeza juhudi za ziada na kuhakikisha wanatokomeza
ugonjwa wa ukoma kabla ya mwaka 2030 kama yalivyo malengo ya maendeleo endelevu
ya dunia. Endapo tutaongeza jitihada katika maeneo haya, sina shaka kuwa nchi
yetu itatokomeza kabisa ugonjwa wa ukoma hata kabla ya mwaka 2030.
Ndugu
wananchi na wanahabari
Ugonjwa wa ukoma unatibika na kupona kabisa. Mgonjwa akijitokeza
na kugunduliwa mapema hupona vizuri bila madhara yoyote. Lakini, iwapo mgonjwa atachelewa
kujitokeza na kupata matibabu mapema, atakuwa katika hatari kubwa ya kupata
madhara ikiwa ni pamoja na ulemavu wa kudumu. Hivyo katika siku hii ya
maadhimisho ya siku ya Ukoma Duniani nitoe rai kwa watu wote wanaougua ukoma
nchini kwenda katika vituo vya tiba ili kupata huduma ya tiba.
Katika miaka 10
iliyopita, ugonjwa wa ukoma peke yake umeongeza idadi ya watu wenye ulemavu wa
kudumu zaidi ya 2,800 hapa nchini na kwa mwaka 2015 tu, walemavu wapya wapatao
300 waligunduliwa miongoni mwa wagonjwa wapya wa ukoma, kati ya hao watoto
walikuwa 26. Ulemavu unaotokana na ukoma unazuilika na hakuna sababu ya
kuendelea kuona idadi kubwa ya nguvu kazi yetu inakuwa tegemezi na mzigo mkubwa
kwa jamii yetu kwa sababu ya Ukoma. Tunapoadhimisha Siku ya Ukoma duniani,
napenda kutoa rai kwa jamii kushiriki katika kuwabaini wagonjwa wa ugonjwa na
kuwahimiza kwenda kwenye vituo vya tiba ili kuepusha ulemavu wa kudumu hasa
miongoni mwa watoto.
Ugonjwa wa ukoma
huchukua miaka mingi, hadi mpaka miaka 30 kati ya maambukizi hadi ugonjwa
unapojitokeza na kuonyesha dalili. Hivyo tuonapo dalili za ugonjwa huu miongoni
mwa watoto ni dhahiri ya kuwa ni maambukizi ya hivi karibuni na kuwa maambukizi
bado yanaendelea katika jamii. Hali itakuwa mbaya zaidi kama mtoto
hatagunduliwa mapema kabla ya kupata madhara ya ulemavu. Kazi kubwa iliyombele
yetu sasa ni kuwaepusha watoto na ulemavu unaotokana na ukoma. Katika muktadha
huu, Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tuepuke ulemavu unaotokana na ukoma
miongoni mwa watoto”.
Kauli mbiu hii
inatutaka wagonjwa wa ukoma hasa watoto wagunduliwe mapema kabla ya kupata
ulemavu na hasa pale zinapojitokeza dalili za mwanzo za ugonjwa huu. Hivyo
basi, kila mmoja wetu katika maeneo ya mijini au vijijini nchini Tanzania, tujenge
tabia ya kuwachunguza watoto wetu kama wana dalili za ugonjwa huu au la. Na endapo
tutabaini dalili za ugonjwa huu miongoni mwa watoto basi tuhakikishe
tunawapeleke katika vituo vya kutoa tiba maramoja ili kuwezesha ugonjwa kugunduliwa mapema kabla ya mtoto kupata
ulemavu na hasa pale zinapojitokeza dalili za mwanzo za ugonjwa wa ukoma.
Ndugu
wananchi na wanahabari
Ukoma huenezwa kwa
njia ya hewa toka kwa mtu anayeugua na ambaye hajaanza matibabu. Dalili za ukoma ni pamoja na baka au
mabaka yenye rangi ya shaba mwilini.
Mabaka haya hayaumi wala
hayawashi bali hupoteza hisia unapoyagusa na yanaweza kujitokeza mahala
popote mwilini, kuanzia kichwani hadi miguuni. Napenda kutoa wito kwa kila
mtu na familia kujijengea tabia ya kujichunguza kila wakati na pale utakapoona
dalili hizo nenda kituo cha huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi, ushauri na
tiba.
Matibabu ya ukoma yanatolewa bila
malipo yoyote katika vituo vyote vya huduma, vya serikali na pia vya binafsi. Serikali itahakikisha zipo dawa za
kutosha na zinazopatikana kwa wakati wote na kwa kila mgonjwa wa ukoma mahali
popote nchini. Tutaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa umma na kwa watoa
huduma hususani katika maeneo ambayo bado ukoma ni tatizo kubwa.
Ningependa kutoa wito kwa halmashauri zote ambazo
bado hazijafikia viwango vya utokomezaji wa ugonjwa wa ukoma kuweka katika
mipango kazi yao huduma za uchunguzi wa ukoma ngazi ya kaya na hasa kuwafanyia
uchunguzi wa mara kwa mara watu wanaoishi na wagonjwa wa ukoma.
Vile vile, naziagiza halmashauri zote nchini
kuhakikisha zinawabaini walemavu wote, hasa wale wenye ulemavu unaotokana na
ukoma na kuwaweka katika mpango wa matibabu ili kuzuia madhara zaidi yanayoweza
kujitokeza baada ya kumaliza matibabu na kupona ukoma.
Aidha naziagiza halmashauri zote nchini kuendesha
uchunguzi wa ugonjwa wa ukoma kila wanapoendesha kampeni yoyote ya upimaji wa
afya za wananchi katika maeneo yao. Mathalani, wakifanya kampeni ya upimaji wa
mabusha, kichocho, kisukari au magonjwa mengineyo, wawapime pia na ukoma. Kwa
njia hii, tutaweza kuwafikia watu wengi zaidi na kuwaokoa kwa kuwagundua na
kuwaponyesha mapema na hivyo basi kulipunguza tatizo la ulemevu huu kama siyo
kulikomesha kabisa.
Ndugu
wananchi na wanahabari
Mwisho napenda kuwashukuru wadau wote ambao
wamekuwa wakitusaidia katika kudhibiti ukoma nchini wakiwemo Shirika la Afya
Duniani (WHO), Shirika la Ukoma la Ujerumani (GLRA), Shirika la Madawa la
NORVATIS, na Mhe. Yohaei Sasakawa, balozi wa amani wa Umoja wa Mataifa katika
harakati za kutokomeza ugonjwa wa ukoma.
Pia natoa shukrani za pekee kwa mke wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mama Janeth Magufuli kwa misaada ya hali
na mali anayoitoa kwa walemavu walioathirika na ukoma katika makazi ya
wasiojiweza sehemu mbalimbali nchini. Vile vile, natoa shukurani kwenu wanahabari
kwa elimu mnayoitoa kwa wananchi kuhusu masuala mbali mbali ya uboreshaji wa
afya ya watanzania, nawaomba muendelee na juhudi hizo na mshiriki pia kikamilifu
kuuelimisha umma juu ya ugonjwa wa ukoma. Tulipofikia siyo pabaya lakini bado
tunahitaji kuweka juhudi kubwa zaidi ili kuumaliza ukoma na athari zake zote
katika jamii na hasa ulemavu ambao kwa namna yoyote ile unazuilika.
Ukoma unatibika na mgonjwa kupona kabisa. Tujitokeze
mapema wakati tukibaini dalili za awali ili tuchunguzwe, tutibiwe na kujiepusha
kabisa na balaa la ulemavu usio wa lazima.
“Tuepuke
ulemavu unaotokana na ukoma miongoni mwa watoto”.
27/01/2017
Comments
Post a Comment