- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
KIASI cha Dola za Marekani bilioni moja kimetengwa kwa ajili
ya kuimarisha zao la muhogo nchini kupitia mkataba wa kibiashara baina ya
Serikali ya Tanzania na kampuni ya Tanzania Agricultural Export Processing Zone
Limited and Epoch Agriculture (TAEPZ) kutoka China.
Akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano hayo jijini
Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji anayeshughulikia viwanda Dk. Adelhelm Meru, alisema huu ni wakati wa
wakulima kunufaika na Kilimo cha muhogo baada ya kulima kimazoea.
Alisema, kwa muda mrefu Watanzania wamekua wakilima muhogo
kwa ajili ya chakula tu huku wakisafirisha muhogo ghafi hali inayokosesha
serikali mapato na kunufaisha mataifa ya nje kupitia zao hilo lenye manufaa
mengi.
“Lengo la serikali kuwa na uchumi wa viwanda linaanza
kutimia, huu ni uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo cha biashara. Kutakuwa
na shamba kubwa la mihogo, kutajengwa viwanda mbalimbali vya kuzalisha unga wa
mihogo, makopa, chakula cha mifugo, sukari ya viwandani na mbolea.
“Hii fursa tusiiache,
kama mlikua mkilima mihogo kwa kiwango kidogo ongezeni mashamba kwa sababu soko
la uhakika lipo, pia tunashauri mnunue hisa katika kampuni hii ili ikiwezekana
tuimiliki kwa kiwango kikubwa,” alisema Dk. Meru.
Vilevile alipongeza urafiki wa kibiashara baina ya Tanzania
na China na kumshukuru balozi wa China nchini, Balozi Lu Youqing kutokana na
juhudi za kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kati kwa kuleta wawekezaji
wengi kila mwaka.
Aliongeza kuwa mradi huu utasaidia wakulima wa mihogo kuongeza
ufanisi na kuhakikisha wanapata mbegu bora ili kufikia kiwango kinachotakiwa
katika kipindi cha miaka mitano ya majaribio, pia kutakuwepo na mafunzo juu ya
ulimaji bora wa zao hili pamoja na namna ya kusindika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta
Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye amewataka wakulima kugeukia Kilimo cha
muhogo kwa sababu wawekezaji hawa wanahitaji tani milioni tano kwa mwaka.
“Takwimu zinaonyesha Tanzania tunazalisha tani milioni tano
za mihogo mibichi kwa mwaka, Kampuni ya TAEPZ inahitaji tani milioni 2.5 za
muhogo mkavu (makopa), maana yake ikiwa mibichi kutoka shambani inakua na uzito
mara mbili.
“Tumeamua kuwaita
wawekezaji kwa sababu tuliwahi kupewa fursa ya kusafirisha tumbaku na nyama
kwenda China, lakini tulishindwa kutimiza vigezo kutokana na kila mmoja
kusafirisha kwa namna yake bila kuzingatia ubora , naamini katika hili
tutafanikiwa kutimiza malengo tuliyojiwekea,” alisema Simbeye.
Balozi wa China nchini Dk. Lu Youqing, akizungumza katika
mkutano huo alisema, “naamini mkataba huu utaleta tija kwa Watanzania, kwa
sababu muhogo ni zao muhimu wa raia wa China na lina faida kubwa. Rais Dk. John
Magufuli wakati wa kampeni za urais pia aliwahi kugusia ushurikiano katika
mazao ya chakula.
“Hata Waziri wa Mambo
ya Nje Jamhuri ya Watu wa China, WANG Yi alipokuja nchini mapema mwezi huu
alitilia mkazo kuhusiana na kusafirisha mazao ya biashara China. Kwa hiyo ili
kuboresha uhusiano wetu ulioasisiwa na Mwenyekiti Mao Tse Tung na Mwalimu
Julius Nyerere, serikali yetu itawekeza zaidi ili kukuza uchumi wa Tanzania.”
Alibainisha kuwa kwa sasa Tanzania ndiyo nchi inayoongoza
Afrika kuwa na uwekezaji mkubwa kutoka China ambapo kiasi cha Dola za Marekani
Bil 6.62 kimewekezwa nchini katika miradi mbalimbali. Hivyo, hata katika
usafirishaji mihogo China watahakikisha Tanzania inazipita Nigeria na Ghana
ambazo ndizo zinazoongoza kwa kusafirisha zao hilo kwa sasa.
Akitoa sababu za kuichagua Tanzania katika mradi huo,
mwenyekiti wa TAEPZ, Dior Feng alisema ni kutokana na ardhi yenye rutuba na
wananchi wengi kujishughulisha na Kilimo cha mihogo lakini hawana soko la
uhakika, hivyo wakipewa maelekezo wanaweza kufikia kiwango kinachohitajika.
“Tanzania kuna fursa nyingi za Kilimo, katika awamu ya
kwanza ya mradi huu tutaanzisha kiwanda za kusindika mihongo katika mikoa
mitatu ambayo ni Lindi, Pwani na Mtwara, ingawa baadaye tutaongeza mikoa
mingine mradi utakapoonyesha mafanikio.
“Tuna imani na kasi ya awamu hii na ndiyo maana tumekubali
kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kwa sababu serikali itatusaidia kuhakikisha
mradi unafanikiwa kwa kiwango kikubwa,” alisema Feng.
Kwa muda mrefu sasa Tanzania imekuwa na urafiki mzuri na
China katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, nishati na uchumi, hivyo hii
ni fursa ya kipekee kwa wakulima kunufaika na zao la muhogo.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
anayeshughulikia viwanda Dk. Adelhelm Meru (kushoto), akiwa na Mwenyekiti wa TAEPZ,
Dior Feng wakati wa kutia saini makubaliano ya mradi wa zao la muhogo nchini
utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 1. Waliosimama kutoka kushoto ni balozi
wa China nchini, Dk. Lu Youqing na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta
Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye. Mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
anayeshughulikia viwanda Dk. Adelhelm Meru (kushoto), akibadilishana nyaraka na
Mwenyekiti wa TAEPZ, Dior Feng baada ya kusaini mradi wa zao la muhogo nchini
utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 1. Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni
balozi wa China nchini, Dk. Lu Youqing na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye. Mwishoni mwa wiki jijini Dar es
Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
anayeshughulikia viwanda Dk. Adelhelm Meru, akizungumza katika hafla ya utiaji
saini makubaliano ya mradi wa kusindika muhogo nchini utakaogharimu Dola za
Marekani bilioni 1, wengine katika picha ni Mwenyekiti wa TAEPZ, Dior Feng na
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Godfrey Simbeye.
Mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment