- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mwalimu Nyerere akihutubia katika uzinduzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam UDSM 1970
Na Daniel Mbega
“VIJANA
wetu lazima wapate elimu inayoendana na Afrika. Hii ina maana kwamba, elimu
ambayo siyo tu inatolewa Afrika lakini pia inayolenga kukidhi matakwa ya sasa
ya Afrika.” Hayo ni maneno aliyoyatoa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Oktoba 25, 1961 akizungumzia kuhusu elimu na
sheria.
Leo
tunapokumbuka miaka 14 ya kifo chake tunaona fahari kubwa kukumbuka maneno ya
busara ya Mwalimu Nyerere, ambaye siyo tu alisukumwa na taaluma yake ya ualimu,
bali nia yake ya dhati ya kuhakikisha kwamba elimu bora inatolewa kwa kila mtu.
Mwalimu
Nyerere aliamini kwamba, elimu pekee ndiyo ingeleta maendeleo ya Tanzania, na
hata Afrika kwa ujumla, na ndiyo maana hata katika hotuba zake nyingi
alisisitiza umuhimu wa watoto kufundishwa namna ya kujitegemea na siyo kufaulu
mitihani tu.
Mwalimu
aliamini kwamba elimu ni ule ujuzi ambao unamwezesha mtu kujitegemea katika
mazingira yanayomzunguka, na siyo fikra zile za kale za kuona kwamba eti mtu
mwenye elimu mahali pake pa kazi na ofisini tu.
Suala hili
mwalimu alijitahidi kulikemea kwa kutumia busara, akifafanua kwa hekima katika
hotuba zake mbili alizowahi kuzitoa mjini Tabora (Mei 4, 1967) na mjini Mbeya
(Mei 14, 1967) ambapo alisema shabaha ya elimu ya msingi lazima ibadilike.
Mwalimu
alisikitika sana kubaini kwamba miaka ya nyuma wakati nafasi za elimu
zilipokuwa chache watu waliona kuwa elimu ya msingi ilikuwa maandalizi siyo ya
maisha bali ya kuendelea zaidi kielimu na kupata kazi za ofisini.
Lakini
akasema kwa kuupanua mfumo wa elimu kwa wote (Universal Primary Education –
UPE), elimu ya msingi inaweza kuwa maandalizi ya maisha kijijini na siyo kazi
za maofisini tu.
“.. Elimu
ya primary kama mnavyojua walimu wenzangu, mimi sikuwahi kufundisha katika
primary kwa hiyo sijui matatizo yake ya kufundisha. Nimefundisha katika
sekondari tu na nimeanzia hapa hapa Tabora. Kwa hiyo najua matatizo ya
sekondari skuli lakini siyo haya ninataka kuzungumza; wala si matatizo ya
walimu ninataka kuzungumza; ni matatizo ya nchi,” alisema.
“Primary,
kama mnavyojua kwanza mpaka sasa ni nusu tu ya watoto wetu ambao wanapata
nafasi ya kusoma. Kabla ya uhuru tulikuwa tuna ngazi mbili za shule za primary.
Tunayo ile miaka minne ya kwanza, halafu wachache hupenya wakaingia katika
miaka minne mingine inayofuata ambayo tunaita middle school. Halafu wachache
hupenya wakaingia katika miaka miwili inayofuata iliyokuwa ya standard nine na
standard ten ya sekondari skuli. Halafu tena tunachuja chuja.
“Tulikuwa
na ngazi nyingi sana za kuchuja chuja. Sisi tukaahidi katika TANU. Tukaahidi
kwamba tutafanya mambo mawili. La kwanza, tutajitahidi kuondoa ngazi hii hapa baada ya miaka minne. Pili, kwamba primary nzima tutaifanya miaka minane.
Miaka minane ile tukaijaribu ikatushinda. Tukaona mirefu. Tukaipunguza
tukafanya kwamba elimu ya primary tutaifanya iwe miaka saba tu basi.
“Basi
ndivyo ilivyo sasa, na ndivyo tunavyojitahidi, na mwaka jana, nadhani, tukaanza
kupata mgogoro wetu wa kwanza kabisa walipomaliza watoto wengi, nadhani
wanakaribia 50,000 waliomaliza standard seven. Wachache wakaingia form one.
Wengine hawakupata nafasi kuingia form one. Tukapata kelele za wazee. Tulipata
kelele nyingi sana mwaka jana. Na mwaka huu tumepata zingine, na nadhani
tutaendelea kupata kwa watoto kukosa nafasi ya kuingia form one.
“Na wazee
wanasema:- “Mwanangu mimi hakushindwa; mbona kakosa nafasi ya kuingia katika
form one? Na wengine wale tunajibu hivi hivi. Tunasema:- Mtoto ameshindwa, huyu
ameshindwa, huyo ameshindwa.” Na washindwaji hawa ni 90 kwa 100 ya watoto
wote… waliofaulu ni wale 10 kwa 100… ndio lugha tunayoitumia. Kusema kweli
tunaitumia mpaka sasa. tunajaribu kuifuta ile lugha lakini tunaitumia mpaka
sasa.”
Mwalimu
alisema kwamba walikuwa wanaogopa kutokana na wingi wa watoto wanaomaliza shule
halafu hawana mahali pa kwenda, yaani wanakosa nafasi za kwenda sekondari
wakati huo, kutokana na uhaba wa shule za sekondari uliokuwepo.
“Wazee
wanauliza; “Mwanangu nitamfanyaje? Sasa mtoto wangu ameshindwa kwenda darasa la
nane, form one. Mimi nitamfanyaje mwanangu?” miezi ya nyuma nilipopita katika
mzunguko ule nilioutaja hapa nilikuwa Musoma, wazee wangu kule wakataka
kunikabidhi watoto wao. Wanasema:- “Nenda nao huko huko Dar es Salaam. Mimi
nitawafanyaje watoto hawa. Wameshindwa! Nenda nao huko wewe utajua la kufanya.”
Nenda nao watoto wenu? Mimi watoto wote hawa wa standard seven nitawabeba! Wa
Tanzania nzima nitakwenda nao wapi? Mzee anaulia: Sasa mtoto huyu ana miaka 13
tu, 14 tu, mnasema eti alime? Atalimaje mtoto wa miaka 13 tu, 14 tu, atawezaje
kulima?
“Swali
hilo anayejiuliza si swali la kweli. Upande mmoja si swali la kweli hata
kidogo. Ni swali la mazowea tu. Anasahau mzee huyu huyu, ama mwalimu, wakati
mwingine mtu mwenye akili nzuri kabisa anakuuliza swali hili… anasema umri wake
mdogo mno hawezi kulima. Upande mmoja ni kweli, watoto hawa wana umri mdogo
lakini si umri unaoleta problem. Tatizo ni kwamba wamesoma watoto hawa. Maana
swali hili haliulizwi kwa mtoto mwenye umri kama huo ambaye hakusoma.
Haliulizwi. Wanasaga watoto wale nyumbani, wanaleta kuni… wanalima… wanachunga
ng’ombe… wanavuna. Haliulizwi swali hili juu ya watoto ambao hawakupata nafasi
ya kwenda shule. Wao wanasema atalimaje na mwanangu kasoma? Kusoma huko kwa
kulima ni kusoma gani? Maana nia ya kusoma, madhumuni ya kusoma ni kuepuka
jembe. Anasoma mtu aepukane na maisha haya ya vijijini ya majembe majembe haya.
“Elimu
ilikuwa ni utaratibu wa kuhama vijijini… ukianza kumsomesha mtoto unajua safari
yake ya kuhama imeanza. Ilikuwa inaanza hivi unaiona. Na hasa kwa sababu shule
tulikuwa hatuna nyingi, watu waliweza kujua kwamba anakwenda huyu sasa. Halafu
baada ya hapo tena nimefanya safari na kumaliza standard four. Kwangu standard
five nimekuja Tabora. Kutoka Musoma unakwenda kuifuata standard five Tabora.
Ndio unakwenda hivyo!
“Unahama.
Na kusema kweli wengine hatujarudi tena. Tumekwenda moja kwa moja. Sasa ikawa
ndio mazowea kwamba mtoto akishapata nafasi ya kusoma, kusoma ni kutokana na
kilimo. Anakuwa kalani na kalamu anaiweka hapa kichwani. Lazima awe ana kalamu
msomaji huyu na shughuli zake hazitokani na kilimo kilimo. Hata unaporudi
nyumbani… wanakufanyia kazi wale wa nyumbani. Shughuli hizi za kufagia fagia au
kazi za mikono wenyewe nyumbani wanakufanyia. Wanasema huyu kasoma! Mpaka wewe
mwenyewe uwe mtundu kidogo useme nitafanya. Uweze kushika ufagio ufagie mahala,
au uchukue vyombo usafishe, au uchukue debe uende kuchota maji… kwa sababu watu
wa nyumbani hawakutazamii uchote maji. Binti aliyesoma debe kichwani si mahala
pake.
“Haya ndio
mawazo yetu. Na hii ni kwa sababu siku zile elimu ndivyo ilivyokuwa. Ilikuwa ni
kitu cha bahati bahati. Anakipata mtu mmoja kwa bahati, na makusudi yake ni
hayo, unampata mtu akawatumikie wakoloni wanaomtaka kwa shughuli fulani fulani…
Elimu haikuwa ni haki ya kila mtu. Elimu ikishakuwa ni haki ya kila mtu, lazima
iwe si elimu ya kuhamisha mtu. Lazima iwe elimu ya kumwezesha mtu yule mahali
pake alipo, maisha yake yanakuwa mazuri zaidi.”
Ingawa
maneno haya aliyasema Mwalimu Nyerere miaka 49 iliyopita, lakini bado yangali
vichwani mwa watu wengi, kwa sababu tunashuhudia kwamba hata kiwango cha elimu
kinachotolewa sasa shuleni hakikidhi haja kwa mtoto kujitegemea hapo baadaye.
Maadamu
tumekusudia kuwafundisha na kuwaelimisha watoto wetu, ni lazima tuondokane na
mawazo kwamba elimu ni ya kuwahamisha wasomi kutoka vijijini.
Lazima tufike mahali tuone kwamba shule zetu
zinatoa elimu bora ya kumwandaa mtoto kujitegemea, hata kama hakupata nafasi ya
kuendelea na masomo ya juu.
Tukiweka
mazingira mazuri ya elimu, tukajenga shule nzuri, madawati ya kutosha, walimu
bora wa kutosha, nyumba bora za walimu, tutapeleka na huduma muhimu za kijamii
huko vijijini, na kubadilisha mitaala yetu ya elimu kuwa ya kumfanya mtoto
ajifunze elimu bora ya kujitegemea, hakika tutakuwa tumetimiza malengo ya
Mwalimu Nyerere ya Elimu ni Kazi.
Lakini pia
Mwalimu Nyerere alikumbusha kwamba hata msomi anaihitaji jamii ili aitumikie.“Watu
wanadhani jamii tu ndiyo inayohitaji wasomi ili wapate maendeleo na neema. Hii
inawafanya wasomi kujiona, kuringa, na kuibeza jamii. Ukweli ni kwamba, ni
msomi ndiye ambaye kwanza kabisa anaihitaji jamii. Bila hivyo kisomo chake
atakipeleka wapi na atakitumiaje. Tunapaswa kuwa sehemu ya jamii, tunatakiwa
kufanya kazi kutoka ndani ya jamii na siyo kujitenga kama miungu ya kale.”
Hii
ilikuwa ni kauli yake aliyoitoa kwenye Chuo Kikuu cha Liberia, Monrovia
Februari 29, 1969 akielezea nafasi ya wasomi katika jamii. Kwa maana hiyo,
pamoja na kuhimiza umuhimu wa elimu, ni vizuri wasomi wetu watambue kwamba
wanahitaji jamii ili waitumie elimu yao ipasavyo. Huwezi kuwa na leseni bila
gari!
Kila kitu
kinawezekana tukiwa na malengo, na tukisimama imara kwa pamoja kushirikiana na
wadau kuhakikisha tunayatimiza kwa vitendo malengo tuliyojiwekea, na kisha kutathmini
kama tumefanikiwa au la.

Comments
Post a Comment