- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
BERNARD Rabiu Saanane, au Ben Saanane,
mwanaharakati chipukizi wa kisiasa, ametoweka tangu Novemba 18, 2016 na
hajulikani aliko.
Kwa jinsi mwanasiasa huyo chipukizi alivyo mahiri
wa ‘kukesha’ kwenye mitandao ya kijamii, kwa vyovyote vile mpaka sasa angekuwa
amejibu mwenyewe kwamba yuko wapi – awe mapumzikoni au kazini.
Hata baada ya familia yake kuamua kufungua
kesi ya ‘kupotea’ kwa ndugu yao katika Kituo cha Polisi Tabata jijini Dar es
Salaam Desemba 5, 2016 na kupewa RB namba TBT/RB/8150/2016, bado viongozi wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho Ben ni kiongozi na Katibu
Myeka wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, hakikuweza kutoa tamkoa
lolote.
Katika mazingira ambayo yanayonyesha kwamba
huenda viongozi wa Chadema walikuwa ‘wakitafuta uongo’ wa kuwaeleza Watanzania,
hawakuweza kusema lolote hadi Jumatano, Desemba 14, 2016 – yaani siku 9 tangu
familia ilipotoa taarifa polisi – ndipo wakatoa tamko.
Tamkoa la Chadema, ambalo lilitanguliwa na
tamko la wanaharakati wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG) lililotolewa
na mwenyekiti wake Malisa Godlisten (mfuasi wa Chadema pia), linatia walakini
kwa sababu halijajibu hoja za msingi na linaonekana kama kuna maigizo ya wazi.
UTG iliipa Chadema saa 72 kutoa taarifa za
kupotea kwa Saanane aliyeondoka nyumbani kwake Novemba 18, 2016 na mpaka sasa hajaonekana
wala taarifa zake kutolewa sehemu yoyote.
Katika tamko lao, badala ya kujibu hoja za
msingi kutokana na mijadala inayoendelea, Chadema wanaitaka eti Serikali kutumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kumtafuta Ben Saanane.
Katika kile ambacho kinaonekana kupotosha ukweli, Mwanasheria Mkuu
wa Chadema, Tundu Lissu alisema ati katika siku za karibuni, Saanane amekuwa
akiongoza kampeni kwenye mitandao ya kijamii, kuhusu kuhakikiwa kwa shahada za
uzamivu (PhD) kwa baadhi ya viongozi kwamba huenda ikawa ndiyo chanzo cha
kutoweka kwake.
Lissu akasema ati wakati fulani (bila kutaja ni lini – pengine
huenda miaka 10 iliyopita) Saanane alitumiwa ujumbe wa maneno kupitia simu yake
ya kiganjani akitishiwa kuacha kuikosoa Serikali.
“Nanukuu maneno aliyotumiwa: “Ben Saanane unachokitafuta ndani ya
Serikali hii utakipata, kwa elimu na uwezo wako hatukutarajia ungefikia hatua
ya ajabu kwa namna ulivyofikia, hujiulizi kwanini upo huru hadi muda huu.
“You are too young to die. Tunajua utaandika na hili, andika
lakini the next post hutaandika ukiwa na uhuru wa kutosha, andika but your days
are numbered.
“Unajua kuna rafiki yako alipuuza na hutaki kuandika kuhusu yeye,
labda kwa kuwa alitangulia, andika Ben, andika sana, ongea, sema lakini
utajikuta mwenyewe na chatu,” alinukuu Lissu.
Kuhusu taarifa ambayo imesambaa katika mitandao ya kijamii kuwa
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anajua aliko Saanane, Lissu alisema:
“Mara ya mwisho Ben amewasiliana na mwenyekiti Novemba 14 mwaka huu akiwa
Dodoma na huwa hawaongozani, bali Ben anafanyia kazi zake makao makuu ya
chama.”
Kitu pekee ambacho Lissu, Mbowe na Chadema hawakijui ni kwamba,
kupotea kwa Ben Saanane siyo suala la itikadi wala kisiasa, bali ni suala la
kitaifa na linawahusu Watanzania wote bila kujali ni wafuasi wa chama gani cha
siasa wala imani gani ya dini.
Kueleza kirahisi rahisi tu kwamba Serikali ndiyo yenye wajibu wa
kulinda hata mipaka ya nchi ni kukwepa hoja kwa mkusudi kabisa wakati
wanafahamu fika wanacheza na uhai wa mtu.
Binafsi sijaridhika na tamko la Tundu Lissu wala ujumbe huo wa
maandishi kwenye simu ambao unaweza pia ukawa wa kutungwa ili kuirushia serikali
lawama kwamba inahusika na utekaji wa watu na kuua wananchi wake, jambo ambalo
halipo.
Chadema na Lissu wanashindwa kusema ukweli
kwamba suala la kutoweka kwa Saanane, ambaye mwaka 2015 aligombea ubunge kule
Rombo na kushindwa vibaya kwenye kura za maoni za chama hicho na Joseph
Selasini, ni la kimkakati zaidi ndani ya chama kama ambavyo taarifa mbalimbali
zimekuwa zikitarai kwenye mitandao ya kijamii.
Ukimya na usiri huu unaleta tafsiri hasi
katika jamii hasa katika kipindi ambacho Chadema, baada ya kushindwa kwa ‘Operesheni
Ukuta’, sasa inataka kuja na ‘Operesheni Kata Funua’ ambayo tunaambiwa ni
Saanane ndiye aliyeiandaa kabla ya kupewa ‘likizo’ na Mbowe kwa ‘kazi nzuri’
aliyoifanya.
Kwa msingi huo basi, Chadema, au viongozi
wa Chadema, wanataka kutumia kutoweka kwa Saanane kama ‘kick’ yao ya kuianzisha
‘Operesheni Kata Funua’ kwa kusingizia kwamba kupotea kwake ni hujuma za
Serikali ya Chama cha Mapinduzi – CCM, wakati siyo kweli.
Pengine wanataka kutumia hiyo kama njia ya
kutafuta huruma ya Watanzania ili wawaunge mkono watakapoanzisha operesheni yao
baada ya ‘ukuta wao kubomoka’. Hakuna anayejua.
Kwa kuwa hakuna anayejua kilichomo katika
mkakati wa Operesheni Kata Funua zaidi ya Saanane mwenyewe na viongozi wa juu
wa Chadema, basi ni vigumu kueleza kama hata kutoweka kwake ni sehemu ya
kufanikisha mkakati huo ama ndio ufunguo wa kuanzisha operesheni hiyo. Hakuna ajuaye.
Kama hayo hayako kwenye mikakati hiyo, basi
ni wakati wa wao kusema wazi aliko Saanane, vinginevyo jamii itaamini kwamba
chama hicho ni cha kuteka na kuwatesa wanachama na wafuasi wake kama ilivyopata
kutokea kwa aliyekuwa mlinzi binafsi wa Katibu Mkuu, Khalid Kagenzi, mwaka 2015
Watu hawatawaelewa kwa sababu watakumbushia
pia ajali ya utata ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Chacha Zakayo
Wangwe, iliyotokea mwaka 2008.
Na hawatawaelewa kutokana na mwenendo wa
uongozi wa mwenyekiti wa chama hicho, Mbowe, kuwaona wale wote wenye mtazamo
chanya na wanaokubalika ni adui zake.
Hakuna anayeweza kuwaelewa kwa sababu kati
ya yanayosemwa kwenye mitandao ya kijamii, yapo mengi yana ukweli kwa asilimia
kubwa.
Ben Saanane ameandaa operesheni nyingi
ndani ya Chadema, ambapo ukiachilia mbali ‘Operesheni Kata Funua’ ambayo
haijaanza, lakini pia aliratibu na kusimamia mkakati wa siri juu ya Zitto Kabwe
mwaka 2013 pamoja na Operesheni Ukuta.
Chadema waseme kuhusu madai kwamba, mnamo
Agosti Mosi, 2016 Saanane alipewa jukumu maalum la kumuandama Rais John Magufuli
kwenye mitandao ya kijamii. Je, hii haikuwa mkakati wao mahsusi wa kutimiza
malengo yao kwamba ikitokea jambo lolote likampata Saanane, basi jamii ielewe
ni kwa sababu ya maandiko yake kwenye mitandao ya kijamii?
Tamko la Lissu linakinzana na taarifa
zilizosambaa kwamba kabla ya kutoweka kwake, Saanane alikuwa amepewa likizo ya
wiki moja na bosi wake, Mbowe, hivyo hata kama waliwasiliana Novemba 14,
ilikuwa ni katika kipindi ambacho alikuwa likizo kabla ya kuianza safari yake
ya kwenda Afrika Kusini ‘kupumzika’ na kwamba katika kipindi hicho cha likizo
ya wiki moja alikuwa ameagizwa na Mbowe kutowasiliana na watu wengine ili apate
muda wa kutosha wa kukamilisha andiko la ‘Operesheni Kata Funua’.
Inaelezwa kwamba kumbe hata gharama gharama
zote za safari kwenda huko Afrika Kusini zililipwa na Mbowe.
Wakati Saanane anaandaliwa safari kwenda Afrika
ya Kusini, Mbowe na baadhi ya viongozi akiwemo John Mrema wakaandaa safari ya
kwenda Uingereza.
Lakini wakati familia ya Saanane ikiwa
haijui aliko ndugu yao, Novemba 26, 2016 akajitokeza mwanachama wa Chadema,
Hilda Newton, kupitia ukurasa wake wa Facebook akiwajibu wale wote waliokuwa
wanamtumia ujumbe kumuuliza alipo Ben Saanane, yeye akawajibu kwamba Saanane yuko
Afrika Kusini na kwamba atarejea siku chache zijazo.
Haijafahamika nani alimtuma Hilda kutoa
taarifa hiyo japokuwa habari nyingine zinadai kuwa ni maelekezo kutoka ngazi za
juu za Chadema.
Hapa kuna walakini na Chadema waseme
ukweli, vinginevyo Watanzania watawahukumu kwa hili.
Comments
Post a Comment