- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Ndama Shabani Hussein, maarufu
kama Pedeshee Ndama Mtoto ya Ng’ombe
By Tausi Ally, Mwananchi
Dar es Salaam. Tuhuma za kughushi, kutakatisha fedha na
kujipatia Dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu zimemfanya
mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Ndama Shabani Hussein, maarufu
kama Pedeshee Ndama Mtoto ya Ng’ombe (44) kupandishwa kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mashtaka
hayo yanaangukia katika Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Akisoma
hati ya mashtaka jana Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa amedai mbele ya
Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa kuwa mshtakiwa huyo alifanya hivyo na
kujipatia Dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu kati ya Februari 26
na Machi 3, 2014.
Msigwa
amedai kuwa Februari 20, 2014 jijini Dar es Salaam, Ndama alighushi nyaraka ya
kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa
kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa
kusafirisha maboksi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yakiwa na thamani ya
Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL
Limited wakati akijua si kweli.
Mshtakiwa
huyo anadaiwa kuwa Machi 6, 2014 katika Jiji la Dar es Salaam, alighushi kwa
kutengeneza hati ya kibali (Certificate of Clearance) ya Umoja wa Mataifa ofisi
ya Dar es Salaam, akijaribu kuonesha kilogramu 207 za dhahabu toka nchini Congo
zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment
Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited,
zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.
Wakili
huyo wa Serikali ameendelea kudai kuwa Februari 20, 2014 mshtakiwa huyo
alighushi fomu ya forodha yenye namba za usajili R.28092 akionesha kampuni ya
Muru Platinum Tanzania Investment Company Limited imelipa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) Dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo
zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani
8,280,000 kutoka Congo kitu ambacho si kweli.
Pia,
mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014 katika jiji la
Dar es Salaam alijihusisha moja kwa moja na utakatishaji fedha kwa kufanya
miamala ya Dola za Marekani 540,390 kwa kuelekeza ziwekwe katika akaunti namba 9120000085152
iliyopo katika benki ya Stanbic yenye jina la Muru Platinum Tanzania Investment
Company Limited na kuzitoa taslimu wakati akijua fedha hizo zinatokana na zao
la uhalifu.
Baada ya
kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi
Mahakama Kuu.
Upande wa
mashtaka umedai upelelezi bado haujakamilika na mshtakiwa alipelekwa rumande
kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili ni miongoni mwa mashtaka
yasiyo na dhamana.
Kesi
imeahirishwa hadi Desemba 13, 2016 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama
upelelezi utakuwa umekamilika.
CHANZO –
MWANANCHI
Comments
Post a Comment