- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
JUMAMOSI Oktoba
Mosi, 2016 wakati mwanandinga maarufu wa Liberia, George Tawlon Manneh Oppong
Ousman Weah, atakata keki ya kutimiza miaka 50, Yanga na Simba watakuwa kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuchukuana katika mechi ya kwanza ya msimu
wa 2016/17 ikiwa ni mechi ya pili ndani ya utawala wa awamu ya tano chini ya
Rais Dk. John Pombe Magufuli.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, Weah, ambaye
ni Seneta wa Jimbo la Montserrado nchini Liberia kupitia chama cha Congress for
Democratic Change – CDC, ataungana na mwanasoka mwingine Julio Cesar Baptista wa
Brazil atayekuwa anatimiza miaka 35.
Lakini wanasoka
hao wataungana na Rais wa 39 wa Marekani, Jimmy Carter na Waziri Mkuu wa
Uingereza, Theresa May, kusherehekea siku ya kuzaliwa. Jimmy Carter atatimiza
miaka 92 wakati Theresa May atatimiza miaka 60.
Simba na
Yanga zitaingia uwanjani zikiwa katika hatua tofauti katika raundi hiyo ya
saba, kwani wakati Simba itaingia ikiwa kileleni mwa ligi hiyo kwa pointi zake
16 baada ya mechi sita, Yanga yenyewe inashika nafasi ya tatu kwa pointi 10
baada ya kushuka dimbani mara tano.
MaendeleoVijijini inajua kwamba, Simba
itaingia dimbani ikiendelea kusherehekea ushindi wake mnono wa mabao 4-0 dhidi
ya Maji Maji ya Songea Septemba 24, 2016 huku Yanga ikiwa na jeraha kubwa baada
ya kucharangwa panga moja katika Stand ya Shinyanga Jumapili, Septemba 25.
Baada ya
kuokota ‘almasi’ 2-0 pale Mwadui, Yanga ilikuwa na uhakika wa kuikaribia Simba
endapo ingeshinda kwenye Stand ya Shinyanga, lakini ikajikuta ikichapwa bao
hilo la pekee na kuzima ndoto zake.
Swali kubwa
lililopo ni kwamba, nani atakuwa mbabe katika utawala wa awamu ya tano wa Rais
Magufuli baina ya timu hizo mbili kongwe?
Tumeshuhudia
katika mechi ya mwisho ya msimu wa 2015/16 iliyofanyika Februari 20, 2016
wakati Yanga ilipoigaragaza Simba kwa mabao 2-0, lakini hiyo inaweza isiwe
kigezo cha kwamba Msimbazi wanaweza kuendelea kuomboleza na Jangwani wanafanya
sherehe.
Hii inatokana
na ukweli kwamba, mechi baina ya timu hizo mbili huwa haitabiriki hata kama
mojawapo ya timu hizo itakuwa inafanya vibaya kuliko nyingine.
Simba inaonekana
msimu huu imepania hasa baada ya kukosa ubingwa kwa misimu minne iliyopita
tangu ilipoibuka bingwa katika msimu wa 2011/2012.
Kejeli wanazozipata
kutoka kwa mahasimu wao ‘Wa Kimataifa’ zimeipa nguvu mpya Simba kurekebisha makossa
yake na sasa inaonekana imejiimarisha zaidi na dhamira yake ni kunyakua
ubingwa.
Katika kipindi
cha awamu ya nne, Simba iliitawala Yanga kwenye Ligi Kuu ikiwemo kuichakaza kwa
mabao 5-0 katika mechi ya marudiano ya msimu wa 2011/12, matokeo ambayo bado
yanaonyesha kovu kubwa kwa vijana hao wa Jangwani.
Kati ya
mechi 20 walizocheza wakati wa awamu ya Jakaya Kikwete, Simba walishinda mechi
sita wakati Yanga ilishinda mechi tano tu, huku timu hizo zikitoshana nguvu
mara tisa ingawa Yanga ndiyo iliyoongoza kwa kufunga jumla ya mabao 23 dhidi ya
21 ya watani wao wa jadi.
Yanga
itatokea Pemba safari hii ambako ilikwenda kutafuta ubani ili iweze kuendelea
kuiadhibu Simba kwa mara ya tatu mfululizo wakati Simba wao wako jijini Dar es
Salaam wakijiandaa vilivyo na mtanange huo.
Matokeo yao yaliyopita, ambayo MaendeleoVijijini inayo,
ni kama yafuatavyo:
Mwaka 2006
Katika msimu
huo mechi zote mbili timu hizo zilitoka suluhu. Kwanza Machi 25 na hata
ziliporudiana Oktoba 29. Yanga ikaibuka bingwa kwa pointi zake 70 wakati Simba
ilishika nafasi ya pili kwa pointi 62.
Ligi Ndogo
2007
Kutokana na
mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa ligi, kwamba inabidi ianze mwezi Agosti,
mwaka 2007 TFF ililazimika kuendesha ligi ndogo ili kuwapata wawakilishi wa
Tanzania kwenye michuano ya kimataifa 2008.
Simba na
Yanga zilikwepana kwa kupangwa tofauti katika hatua ya makundi ambayo yalikuwa
Arusha, Dodoma na Morogoro n ahata katika hatua ya Sita Bora, bado zilipangwa
tofauti.
Yanga
iliongoza kundi la Arusha na Simba ikaongoza kundi la Morogoro, hivyo
zikakutana fainali Julai 8, 2007 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro mbele ya
watazamaji 9,758.
Mechi hiyo
iliyochezeshwa na Victor Mwandike ilishuhudia Simba ikipata bao la kuongoza
dakika ya pili tu ya mchezo kwa mkwaju wa penalty ya Mkenya Moses Odhiambo,
lakini Yanga ikasawazisha katika dakika ya 56 kupitia kwa Said Maulid, matokeo
ambayo yalidumu hadi katika muda wa nyongeza hivyo kulazimisha kupigwa mikwaju
ya penalty, ambapo Simba ilipata penalty 4 na Yanga ikapata 3, hivyo Msimbazi
wakawa mabingwa.
Msimu wa 2007/08
Katika msimu
huo, Simba iliifunga Yanga katika mechi ya kwanza Oktoba 24, 2007 kwa bao la
Ulimboka Mwakingwe katika dakika ya 32 na ziliporudiana Aprili 27, 2008
zikatoka suluhu.
Hata hivyo,
msimu huo Yanga iliibuka bingwa kwa kufikisha pointi 49 wakati Simba ilishika
nafasi ya tatu kwa pointi zake 42. Prisons ya Mbeya ndiyo iliyoshika nafasi ya
pili baada ya kukusanya pointi 45.
Msimu wa 2008/09
Mechi ya
kwanza ya watani wa jadi Oktoba 26, 2008 ilishuhudia Ben Mwalala akiipatia
Yanga bao pekee la ushindi dakika ya 16 na ziliporudiana Aprili 19, 2009 zikatoka
sare ya 2-2.
Yanga ilitwaa
ubingwa msimu huo, lakini ilikuwa imefungiwa na TFF kushiriki michuano yote ya
kimataifa kutokana na kitendo chake cha kugombea mechi yake na Simba ya
kutafuta mshindi wa tatu wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 2008.
Msimu wa 2009/10
Bao la
dakika ya 25 la Mussa Hassan Mgosi liliipatia ushindi Simba Oktoba 31, 2009, na
ziliporudiana Aprili 18, 2010, Yanga ikalala tena kwa mabao 4-3. Mabao ya Simba
yalifungwa na Uhuru Selemani (dk. 3), Mgosi (dk. 53 na 73), na Hilary Echesa
(dk. 90+) wakati ya Yanga yalifungwa na Athumani Idd ‘Chuji’ (dk. 31), Jerry
Tegete (dk. 67 na 88pen.).
Msimu huo
Simba ndio walioibuka mabingwa kwa kufikisha pointi 62 dhidi ya 49 za Yanga
iliyoshika nafasi ya pili.
Msimu wa 2010/11
Jerry Tegete
aliipatia Yanga bao pekee na la ushindi katika dakika ya 79 kwenye mchezo wao
wa kwanza Oktoba 16, 2010, lakini ziliporudiana Machi 5, 2011 zikafungana 1-1
huku Stephano Mwasika akiipatia Yanga bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalty dakika
ya 56 na Mgosi akaisawazishia Simba dakika ya 74.
Msimu huo
Simba ilinyang’anywa ubingwa na Yanga kwa tofauti ya wastani wa mabao, kwani
timu zote zilikuwa na pointi 49. Hata hivyo, Yanga ilifunga mabao 32 na kufungwa
7 hivyo kuwa na tofauti ya mabao 25, wakati Simba ilifunga mabao 40 na kufungwa
17, kwa hiyo ikawa na tofauti ya mabao 23!
Msimu wa 2011/12
Pengine
ulikuwa msimu mbaya kwa Yanga, kwa sababu licha ya kupoteza ubingwa wake,
lakini ilikubali kipigo cha mabao 5-0 katika mechi yao ya marudiano na Simba Mei
6, 2012 ambayo ilijawa na hujuma kubwa.
Katika mechi
ya kwanza Oktoba 29, 2011 Yanga ilikuwa imeifunga Simba bao 1-0 kupitia kwa
Mnyasa Davis Mwape dakika ya 75.
Msimu huo
Simba ndio waliotwaa ubingwa kwa kufikisha pointi 62, Azam wakashika nafasi ya
pili kwa pointi 56 na Yanga wakashika nafasi ya tatu kwa pointi 49.
Msimu wa 2012/13
Oktoba 3,
2012 Yanga ilinusurika kufungwa baada ya kusawazisha dakika ya 64 kupitia kwa
Said Bahanuzi. Simba walipata bao la kuongoza dakika ya tatu kupitia kwa Amri
Kiemba.
Ziliporudiana
Mei 18, 2013 Yanga ikaibuka na ushindi wa 2-0 na msimu huo ikatwaa ubingwa kwa
kufikisha pointi 60 wakati Simba ilishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 45.
Azam walishika nafasi ya pili kwa mara nyingine tena wakiwa na pointi 54.
Msimu wa 2013/14
Huu ulikuwa
msimu was are baina ya timu hizo. Kwanza zilifungana 3-3 Oktoba 20, 2013, na
ziliporudiana Aprili 19, 2014 zikafungana 1-1. Safari hii Azam ndio waliokuwa
mabingwa kwa kufikisha pointi 62 wakati Yanga ilishika nafasi ya pili kwa
pointi 56. Simba ilikuwa ya nne kwa kukusanya pointi 38 wakati Mbeya City
ilishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 49 katika msimu wake wa kwanza.
Msimu wa 2014/15
Oktoba 18,
2014 timu hizo zilitoka suluhu, lakini ziliporudiana Machi 8, 2015 Yanga
ikafungwa bao la kizembe mno na Emanuel Okwi ambalo linaendelea kubaki katika
kumbukumbu hadi leo. Yanga ilitwaa ubingwa na Azama ikashika nafsi ya pili huku
Simba ikishika nafasi ya tatu.
Msimu wa 2015/16
Kwanza
Septemba 26, 2015 Yanga iliitandika Simba 2-0, halafu ziliporudiana Februari
20, 2016 ikatoka kipigo kama hicho na ikatwaa ubingwa ikifuatiwa na Azam huku
kwa mara nyingine Simba ikishika nafasi ya tatu.
Msimu wa 2016/17
ndio umeanza, tusubiri tuone itakavyokuwa katika mechi ya Jumamosi.
Mechi
nyingine za Ligi Kuu zitakazochezwa Jumamosi na Jumapili ni kama ifuatavyo:
Oktoba 1,
2016: Yanga vs Simba
Oktoba 2,
2016: Azam vs Ruvu Shooting
Oktoba 2,
2016: Kagera Sugar vs Prisons
Oktoba 2,
2016: Majimaji vs Stand United
Oktoba 2,
2016: Mbao vs JKT Ruvu Stars
Oktoba 2,
2016: Mbeya City vs Mwadui
Oktoba 2,
2016: Mtibwa Sugar vs African Lyon
Oktoba 2,
2016: Toto Africans vs Ndanda
Msimamo wa
Ligi Kuu
1. Simba 6 5 1 0 12:2 16
2. Stand U. 6 3 3 0 6:3 12
3. Yanga 5 3 1 1 8:1 10
4. Azam 6 3 1 2 8:5 10
5. Mtibwa 6 3 1 2 7:6 10
6. Kagera 6 2 3 1 4:3 9
7. Prisons 6 2 3 1 3:2 9
8. Mbeya
City 6 2 2 2 7:6 8
9. Mbao 7 2 2 3 9:10 8
10. Ruvu
Shoot. 6 2 2 2 5:7 8
11. Ndanda 7 2 2 3 6:9 8
12. African
Lyon 6 1 3 2 4:7 6
13. Ruvu
Stars 5 1 2 2 3:3 5
14. Toto
Africans 6 1 2 3 1:3 5
15. Mwadui 6 1 2 3 3:6 5
16. Majimaji 6 0 0 6 2:15 0
Makala haya yameandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com, simu 0656-331974. Kama utayatumia kwa namna yoyote ile ni lazima utoe credit kwa mwandishi Daniel Mbega au MaendeleoVijijini Blog.
Comments
Post a Comment