- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
KIKOSI cha
timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, Jumapili Oktoba 2,
2016 kitajitupa uwanjani mjini Brazzaville kupambana na wenyeji Congo katika
kutafuta nafasi ya kucheza fainali za 17 za vijana Afrika.
Timu hiyo
inaingia uwanjani ikiwa na ushindi wake wa mabao 3-2 ilioupata jijini Dar es
Salaam Septemba 18, 2018 ambao kama itaulinda, utakuwa mtaji mzuri wa kushiriki
kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya vijana ambayo itafanyika Aprili 2017 nchini
Madagascar.
Hata hivyo,
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, Serengeti Boys inakabiliwa na kumbukumbu mbili kubwa katika mashindano hayo.
Kwanza,
itakumbukwa kwamba, timu hiyo ilifuzu kwa fainali za mwaka 2005 kule Gambia,
lakini ikashindwa kushiriki baada ya kutolewa na Shirikisho la Soka Afrika
(CAF) kutokana na kumchezesha ‘kijeba’ beki Nurdin Bakari aliyekuwa akiitumikia
klabu ya Simba wakati huo.
Katika
raundi ya awali iliitoa Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1 – kwanza ikitoka sare ya
1-1 mjini Kigali kabla ya kushinda 1-0 jijini Dar es Salaam.
Kwenye raundi
ya kwanza iliifungashia virago Zambia kwa kushinda jumla ya mabao 4-1. Ilishinda
2-1 ugenini halafu ikashinda 2-0 nyumbani.
Katika raundi
ya pili ikaitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 4-1 pia – ilishinda 3-1 nyumbani na
kisha 1-0 ugenini, mechi ambazo Nurdin Bakari hakucheza kutokana na kutumia
kadi mbili za njano.
Wakati ikiwa
tayari imefuzu na kutarajiwa kupangwa katika Kundi B pamoja na Nigeria, Afrika
Kusini na Ivory Coast, huku maandalizi yakiendelea, hatimaye Januari 28, 2005
CAF ikaiondoa Tanzania kwenye fainali hizo kwa kumchezesha Nurdin Bakari dhidi
ya Rwanda na Zambia kutokana na kudanganya umri.
TFF ilieleza
kwenye taarifa za wachezaji kwamba Nurdin alizaliwa mwaka 1988, lakini katika
orodha iliyotumwa CAF na klabu yake ya Simba kwenye mashindano ya Ligi ya
Mabingwa, ilionyesha kwamba mchezaji huyo alizaliwa mwaka 1983!
Kwa maana
hiyo ukijeba wa Nurdin ukaikosesha Tanzania kushiriki fainali na nafasi yake
ikachukuliwa na Zimbabwe ambayo hata hivyo iligeuka kuwa daraja la timu
nyingine.
Jambo la
pili ni kwamba, Serengeti Boys inakumbuka pia ilivyozikosa fainali za mwaka
2013 kule Morocco baada ya Congo-Brazzaville hao hao kuwafungashia virago
katika raundi ya pili.
Baada ya
kusonga mbele kwa chee kufuatia Misri kujitoa katika raundi ya kwanza, Tanzania
ilikumbana na Congo-Brazzaville kwenye raundi ya pili na mechi yao ya kwanza
Novemba 16, 2012 ilishuhudia Serengeti ikishinda 1-0, lakini ziliporudiana
mjini Brazzaville Desemba 2, 2012 Serengeti wakakubali kipigo cha 2-0.
MaendeleoVijijini inajua kwamba, haya ni
majinamizi ambayo Serengeti inapaswa kukabiliana nayo kwa dhati kuhakikisha
inashinda na kufuzu kwa fainali hizo.
Serengeti inahitaji
ushindi ama sare ya aina yoyote ili iweze kufuzu kwa mara ya kwanza fainali
hizo ambazo kwa ujumla ndizo zimepata kuibua vipaji vya wachezaji wengi nyota
wa Afrika waliotamba na wanaoendelea kutamba katika ligi mbalimbali duniani.
Ushindi au
sare utasaidia kulinda matokeo yake ya kwanza ya ushindi wa 3-2, wakati Congo
wao wanahitaji ushindi hata wa bao 1-0 tu kutokana na kuwa na faida ya bao la
ugenini.
Ili kufuzu,
Serengeti wanatakiwa kutafuta mabao ya mapema, kuimarisha kiungo pamoja na
ngome ili kuvuruga mashambulizi ya wenyeji wao na kutoruhusu kupenya.
Jukumu hilo
linaweza kuwa limefanyiwa kazi vizuri na makocha wa timu hiyo ambao wameiongoza
vyema katika hatua za awali ambapo kwanza iliitoa Shelisheli kwa jumla ya mabao
9-0; kwanza ikiifunga 6-0 ugenini na kushinda 3-0 nyumbani, halafu ikaitoa Afrika
Kusini kwa jumla ya mabao 3-1; ikitoka sare 1-1 ugenini na kushinda 2-0
nyumbani.
Timu nyingine
ambazo zinawania nafasi saba ili kuungana na wenyeji Madagascar kwenye fainali
hizo ni Ghana, Ivory Coast, Niger, Gabon, Mali, Ethiopia, Senegal, Guinea,
Sudan, Cameroon, Angola na Comoro.
Katika mechi
zilizopita, Ghana iliifunga Ivory Coast 3-1; Niger ikaifunga Gabon 1-0; Mali
ikashinda 2-0 dhidi ya Ethiopia; Senegal ikafungwa nyumbani 1-0 na Guinea;
Sudan ikailima Cameroon 4-2; na Angola ikaichabanga Comoro 5-0.
Congo ni
wazoefu wa mashindano hayo, walikuwa mabingwa wa kwanza mwaka 1985 na wamerudia
nusu fainali mara mbili – mwaka 1991 na 2011 – na wameshiriki ubingwa wa dunia
wa vijana mara tatu.
Makala haya yameandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com, simu 0656-331974. Kama utayatumia kwa namna yoyote ile ni lazima utoe credit kwa mwandishi Daniel Mbega au MaendeleoVijijini Blog.
Comments
Post a Comment