- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Orchestra Maquis Original mwaka 1987 katika ukumbi wa Wapiwapi's Bar, Chang'ombe jijini Dar. Kutoka kulia ni: Mbuya Makonga "Adios", Dekula Kahanga "Vumbi", Mpoyo Kalenga na William Maselenge. Aliyechuchumaa ni Juma Choka. Picha kwa hisani ya wanamuzikiwatanzania.blogspot.com.
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
Wasifu
Jina kamili: Dekula Aloyce Obeid Kahanga
Kuzaliwa: Aprili 2, 1962
Mahali: Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Mtaalamu: Gitaa la solo, mtunzi, mwimbaji,
Bendi alizopitia: Kyalalo Band, Gramick
Jazz, Bavy National, Grand Mike Jazz, Chamwino Jazz, Marquis du Zaire, Makonde Group (Sweden).
Bendi ya sasa: Dekula Band (Sweden).
Dekula Aloyce Obeid Kahanga ‘Vumbi’ (alizaliwa Aprili 2, 1962 katika Kijiji cha Lumera, Wilaya
ya Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo). Ni mwanamuziki wa Congo
mwenye uraia wa Sweden ambaye alijipatia umaarufu mkubwa akiwa nchini Tanzania
wakati akipiga muziki na bendi ya Orchestra Marquis du Zaire. Dekula ni
mtaalamu wa kupiga gitaa hasa la solo na umahiri wake unasikika katika nyimbo
nyingi za Marquis kama Makumbele, Ngalula,
Tipwatipwa na kadhalika.
Ni baba wa
familia akiwa na mke na watoto watatu. Dekula ni mtoto wa kwanza kati ya watoto
kadhaa wa Mzee Aloyce Obeid Dekula, aliyekuwa mfanyakazi katika serikali ya
Zaire iliyokuwa ikiongozwa na rais Mobutu Seseseko.
Dekula ni
kati ya wanamuziki wachakarikaji ambaye amepata mafanikio makubwa hivi sasa
akiwa jijini Stockholm, Sweden pamoja na bendi yake anayoimiliki ya Dekula
Band.
Maisha ya awali
Akiwa huko
kwao wilaya ya Kivu, ‘Vumbi’ alikuwa msikilizaji mzuri wa Radio Tanzania Dar es
Salaam (RTD) ambayo ilikuwa ikisikika wakati huo na alizitamani sana nyimbo
zilizokuwa zikiporomoshwa na bendi za Morogoro Jazz, Jamhuri Jazz, Tabora Jazz,
Nyanyembe Jazz, NUTA Jazz, Mlimani Park, Maquis du Zaire na Orchestra
Safari Sound.
Awali baba
yake hakupenda apige gitaa, lakini kwa bahati nzuri alikulia kwa bibi yake
katika mji wa Uvira, Mkoa wa Kivu, ambako alipata wasaa mzuri wa kujifunza na
kutumia ala hiyo.
Huko alikuwa
na uhuru zaidi na akaanza kwa kutengeneza magitaa yake, ambapo yalikuwa
yakivunja kila mara baba yake alipokuwa akienda kumtembelea bibi yake.
Jirani na
alipokuwa akiishi kulikuwa na baa iliyoitwa Sikiya Sosi ambapo palikuwepo na
bendi iliyoitwa Gramick Jazz iliyokuwa ikitumbuiza hapo. Bendi hiyo ilipitiwa
na wanamuziki wengi ambao baadaye walikwenda Tanzania, akiwemo Ramazan Mtoro
Ongalla ‘Dk. Remmy’.
Dekula alikuwa
akisikiliza muziki uliokuwa ukipigwa katika baa hiyo na yeye akawa anafuatisha
kwenye gitaa la kutengeza mwenyewe la nyuzi tatu.
Bibi yake
akamnunulia gitaa dogo la nyuzi nne ambalo alikuwa anaenda nalo hadi shuleni,
ambako mwalimu wake siku nyingine alikuwa akimwita awatumbuize wanafunzi wenziwe.
Baadaye
akakutana na jamaa aliyekuwa akipiga katika bendi iliyokuwa ikimilikiwa na
mapadri, Dekula akawa anamnunulia sigara huyu jamaa, naye akaanza kumfundisha
chords mbalimbali za kupiga gitaa.
Aliendelea
vizuri hatimaye akajiunga na bendi hiyo ya mapadri iliyoitwa Kyalalo Band akiwa
mpiga rhythm.
Wanamuziki
wa Kyalalo hawakuruhusiwa kujiunga na bendi zilizokuwa zinapiga muziki kwenye baa
wala bendi yenyewe kwenda kupiga kwenye baa. Kulikuwa na ukumbi mkubwa wa
kanisa na hapo ndipo walipofanya mazoezi na maonyesho.
Alipata
elimu ya sekondari katika shule mbili tofauti za Bukavu na Uvira huko Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo. Alihitimu kidato cha nne mwaka 1979.
Aanza rasmi muziki
Mwaka 1980,
safari yake katika muziki ilianza kwa kujiunga na bendi ya Grand Mike Jazz.
Kama ni kuanza rasmi muziki wa ushindani, basi ilikuwa mwaka 1983 wakati Dekula
alipojiunga na bendi Orchestre Bavy National kama mpiga rhythm. Bendi hiyo
ilikuwa ikipiga muziki pale pale Sikia Sosi Bar mjini Uvira, mkoani Kivu. Bendi
hiyo iliongozwa na Packot ambaye pia alikuwa mpiga solo, Maboko alikuwa akipiga
gitaa la bass, Merry-Djo alikuwa akipiga drums na waimbaji walikuwa Djo Mali na
Simplice Mofeza.
Akiwa hapo
akakutana na mwimbaji Issa Nundu ambaye alikuwa anafanya kazi hospitali na
jioni kujiunga na bendi. Baadaye Kyanga Songa ambaye kazi yake ilikuwa Bwana
Shamba naye akajiunga nao.
Katika
kipindi hicho wakazi wa Kongo ya Mashariki, ambako kunazungumzwa Kiswahili,
walikuwa wakisikiliza na kuzijua bendi nyingi kutoka Afrika Mashariki. Bendi
kama Tabora Jazz, Mangelepa, Simba wa Nyika, Mlimani Park zilisikilizwa sana,
na wimbo kama Kassim ulikuwa maarufu
wakati huo na hivyo ikawa ndoto ya Vumbi kuwa lazima siku moja aende huko
unakotoka muziki mtamu ili naye aweze kushiriki.
Kutoka
kulia mstari wa nyuma ni Dekula (Rythm), Packot (Solo na Kiongozi),
Maboko (Besi), Merry-Djo (Drums). Kutoka kulia mstari wa mbele, waimbaji
ni Djo-Mali,Issa Nundu na Simplice Mofeza. Hii ilikuwa mwaka 1983
katika ukumbi wa "Sikia Sosi Bar" mjini Uvira, Kivu katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo.
Katika
kipindi hicho Kyanga Songa na Issa Nundu waliondoka kwenye bendi ya Bavy
National na kwenda nchini Tanzania. Bendi ikatetereka sana, lakini Vumbi naye
wakati huo akawa na hamu ya kwenda Afrika Mashariki.
Bahati nzuri
mtu mmoja Alida Shanga akamfuata akiwa ametumwa na Mzee John Luanda aliyekuwa
anamiliki Chamwino Jazz kwenda Zaire kutafuta wanamuziki. Akawachukua yeye
Dekula, waimbaji akina Sisko Lunanga, Fanfan Bwami, Baposta na mwenzao mmoja
Baposta Kilosho ambaye hatimaye alirudi Congo.
Wakatua Tandale
jijini Dar es Salaam, na siku hiyo waliyofika tu wakaanza mazoezi. Wakiwa
vijana bado yeye na wenzie watatu walikuja wakiwa na staili ya kuimba na steji
show ambayo wakati huo iliitwa sarakasi, na pia wao ndio walioanzisha mtindo wa
kurap katikati ya nyimbo.
Katika bendi
ya Chamwino wakati huo wapiga magitaa walikuwa Vumbi Dekula, Kazembe wa Kazembe
(huyu alikuwa Msukuma ambaye aliishi kwa muda Congo na alikuwa mpiga gitaa
hodari sana), na Mzee Albert, na baadaye wakamchukua Muhidin Kisukari ambaye
alikuwa mpiga bass wa Dk. Remmy.
Rekodi yao ya
kwanza ilimuacha aliyekuwa mtangazaji maarufu nchini, ‘Uncle J’ Julius
Nyaisanga akishangaa vituko vya vijana hao.
Mwaka 1983
alikutana na mwanamuziki Tshimbwiza Tchinsensi Nguza Mbangu ‘Viking’, maarufu
Babu Seya, katika ofisi za Ubalozi wa Congo nchini Tanzania. Nguza wakati huo
alikuwa mpiga gita la solo pia alikuwa mmoja kati ya wanahisa wa Orchestra Marquis
Company (OMACO) na mmoja kati ya viongozi wa bendi ya Orchestra Marquis du
Zaire. Katika maongezi yao, Nguza alimpa mwaliko yeye na wenzake kwenda
kuburudisha kwenye ukumbi wa White House, uliokuwa maeneo ya Ubungo jijini Dar
es Salaam.
Dekula
alikubali mwaliko huo na Weekend moja walifika na kupewa nafasi ya kuburudisha
kwa muda mfupi.
Walipopanda
jukwaani waliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi wa muziki waliokuwa wamefurika
ukumbini humo pamoja na wanamuziki wa bendi hiyo ya Marquis du Zaire. Wakati
huo walikuwa wakipiga nyimbo za kukopi, kama Mario, Maze na kadhalika.
Walipopanda jukwaani wakazipiga hizo na watu wakafurahi sana na kuwatuza fedha
nyingi, wakachanganyikiwa maana bendi yao ya Chamwino ilikuwa haina mshahara na
si mara moja walitembea kwa miguu kutoka Buguruni hadi Tandale kwa kukosa mapato.
Japo wakati
huo walikuwa wadogo kwa umri na hata umbo (walifika mahala marehemu Ndala Kasheba
alikuwa anawaita ‘Vimario’) upigaji wao ulikuwa mzuri sana. Nguza Vicking aliwashauri
wawe wanakwenda kupiga kabla Marquis hawajaanza maonyesho. Hivyo wakaamua
kuacha Chamwino na wakawa wanasindikizana na Marquis. Jambo hilo lilimuudhi
aliyewaleta na siku moja wakiwa kwenye ukumbi wa Silent Inn, maofisa wa
Uhamiaji walikwenda kuwachukua wakalazwa Kituo Kikuu cha Polisi kabla ya
kupelekwa mahabusu katika Gereza la Keko.
Wakiwa huko mahabusu
wakamwandikia Mzee Luanda kuwa wanarudi Chamwino, basi wakaachiwa na kurudi
kusuka upya Chamwino Jazz. Hata hivyo, hawakukaa muda mrefu Mzee Makassy akaja
kuwaomba waingie katika bendi yake. Wenzake Sisco Lunanga na Bwami Fanfan wakaenda
kuimarisha safu ya uimbaji ya Orchestra Makkasy, yeye akabaki Chamwino.
Baadaye viongozi
wa Marquis du Zaire akina Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Mutombo Lufungula
‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’ walimtaka aandike barua ya kuomba kujiunga na
bendi yao kwa mkataba usio na mshahara. Alitakiwa na bendi hiyo ili kuziba
nafasi ya Nguza ambaye alikuwa tayari ameanza mgomo baridi. Vumbi alikubali na
ndio ukawa mwanzo wa kujiunga rasmi na Marquis kama mpiga gitaa la solo nambari
mbili (second solo). Aliwakuta wanamuziki kama Maneno Uvuruge, Omari Makuka,
Keppy Kiombile, Ilunga Lubaba, William Maselenge, Mbuya Makonga ‘Adios’, Mpoyo
Kalenga, Juma Choka na wakongwe wengine.
Siku moja
bendi ilikuwa inapiga maeneo ya Ukonga. Kwa kawaida Mzee Lubaba alikuwa anapiga
kuanzia saa tatu mpaka saa sita usiku, kisha Nguza Viking akiingia na
kuendelea. Siku moja Nguza hakuonekana ukumbini na ndipo Vumbi akaweza kupiga
nyimbo zote za Nguza, kesho yake akaambiwa afike ofisini akasainishwa rasmi
mkataba wa kuwa mwanamuziki kamili wa Marquis.
Vumbi
anaikumbuka siku mmoja wakipiga muziki katika ukumbi wa Temeke Stereo, alimuona
Nguza akiwa amejibanza pembeni mwa ukuta ukumbini humo huku akisikiliza midundo
inavyounguruma.
“Nilipomuona,
nikaingiwa na hofu kubwa nikijihisi kama ninamvunjia heshima Nguza. Nikaomba nimpishe
ili ashike nafasi yake.” Dekula anakumbuka.
Lakini viongozi
wake akiwemo Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’ na Ilunga Lubaba walimwamuru aendelee
kushika ‘mpini’. Amri hiyo, ilikuwa kama fisi aliyeachiwa bucha kuilinda.
Alizicharaza kwa umahiri mkubwa nyimbo zote zilizokuwa zikipigwa na Field
Marshal Nguza zikiwemo za Makumbele,
Ngalula, Seya, Malokelee, Karubandika, Mage, Dora Mtoto wa Dodoma, Clara, Mwana
Yoka ya Bato te, Nimepigwa Ngwala na nyingine nyingi pasipo kutofautisha
kati yake na Nguza.
Aliachiwa
kulivurumisha gita hadi mwisho wa onyesho hata mpiga solo Ilunga Lubaba
hakutaka kuligusa siku hiyo. Baada ya hapo kwa adabu zote alikwenda kumsalimia
Nguza pale alipo naye hakusita kumpa hongera kwa kazi nzuri.
Mgogoro kati
ya uongozi wa Marquis du Zaire na Nguza ‘Vicking’ ziliendelea hatimaye
aliondoka rasmi na kwenda kuanzisha bendi yake ya Orchestra Sambulumaa akiwa na
wanamuziki wengine akiwemo mwanaye Nguza Mbangu lakini bendi hiyo ikafa na
ndipo alipoanzisha bendi yake ya Achigo Band iliyokuwa ikipiga kwenye ukumbi wa
Motel Tiger, Mbezi Beach, ambayo ilikuwa na wanawe akina Papii Kocha lakini
ikasambaratika tangu mwaka 2004 wakati yeye na wanawe walipohukumiwa kifungo
cha maisha jela kwa makosa ya ubakaji.
Baada ya kuondoka
kwa Nguza walirekodi ule wimbo maarufu wa Makumbele.
Solo ya wimbo huo ilikuwa awali ikipigwa na Mzee Lubaba, lakini afya ya mzee
Lubaba ilianza kuzorota naye akawa anawafundisha nyimbo zake wanamuziki wengine.
Wimbo wa Makumbele alifundishwa
Makuka na akawa anaupiga katika maonyesho mbalimbali, lakini wakati wa kutaka
kurekodi kamati ya uongozi ya Marquis iliamua Vumbi aufanyie mazoezi na
aurekodi.
Kurekodi kwa
album ya Makumbele ilitokana na
safari ndefu ya bendi ambayo ilichukua miezi mitatu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,
hivyo waliporejea Dar wakakuta sifa ya bendi imepungua.
Kwa hiyo basi,
walirekodi album ya Makumbele
iliyokuwa na nyimbo kama Tipwatipwa, Ngalula na Makumbele, sifa ya bendi ikarudi juu tena kwa mara nyingine.
Ni wakati huo
ambapo bendi ilihamia katika ukumbi wa Lang’ata, Kinondoni jijini Dar es Salaam
ikitokea ukumbi wa White House.
Dekula Kahanga akionyesha umahiri wa kucharaza gitaa la solo huko Ughaibuni.
Dekula Kahanga akiwa na farasi.
Miaka ya
1989 na 1990 Dekula alikuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa Marquis Original,
jina lililozaliwa kutoka Marquis du Zaire baada ya kuhamia katika ukumbi wa Lang’ata
Kinondoni. Mtunzi na mwimbaji Marquis Original Tshimanga Kalala Assosa, alikuwa
akipaza sauti ya kumpandisha mori kwa kumuita mara kwa mara “Vumbiii! Vumbiii! Vumbiii!”
kama kibwagizo wakati wa chorus kwenye wimbo wa Ngalula.
Vumbi wakati
huo alikuwa na umri ambao unamruhusu kuhangaika kutafuta maisha yenye maslahi
mazuri. Hivyo uamuzi mgumu ukaanzia hapo Lang’ata baada ya kuamua kuiacha Marquis
Original, iliyompa jina na akaondoka na kutua katika jiji la Stockholm nchini
Sweden ambako hakujua atakuwa mgeni wa nani huko ughaibuni.
Akiwa
Stockholm, Vumbi alianza kuchacharika mitaani akitafuta bendi ya kupiga, hatimaye
akakutana na mwanamuzi kutoka Uganda, aitwaye Sammy Kasule. Mwaka 1993 wakaamua
kuanzisha bendi yao ikiitwa Makonde Group.
Baada ya
mihangaiko mingi, hatimaye alifanikiwa kuanzisha bendi yake ya Dekula Band,
ambayo kwa sasa ina mkataba wa kupiga mara mbili kwa mwezi katika ukumbi wa
Lala Vin, jijini Stockholm.
Mwaka 1999,
Dekula alifyatua album iitwayo Bolingo Ekeseni iliyosheheni nyimbo za ‘Dunia kuna mambo’ na ‘Mpenzi Asha’.
Dekula Band
ina wanamuziki mahiri kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo akina Luhembwe
Mwanahita ‘Bobo Sukari’ ambaye ni mwimbaji na mcheza show kutoka Congo ambaye
alipigia bendi kadhaa nchini Tanzania, Sammy
Kasule, huyo ni injinia pia huimba, kupiga gita la besi, drums na
kinanda. Wengine ni Joe Gerald Nadibanga, ambaye huimba, kupiga konga na
kucheza show, Christina Frank na Marceline Kouakoua. Mwenyewe Dekula
hulicharaza gila la solo na rhythm pamoja na Arne Winald ambaye ni mbonyezaji
wa kinanda.
Safu hiyo
kwa pamoja huufanya muziki wao kukubalika kimataifa hadi kupata mialiko lukuki
ndani na nje ya Sweden zikiwemo nchi za Ulaya, Asia, Marekani, Japan, Falme za
Kiarabu na Afrika.
“Hakuna kitu
muhimu kama kuwa na uhusiano mwema na watu kutoka nchi mbalimbali ninazotembelea.
Nimefikia kuweza kuongea kwa ufasaha lugha tano tofauti za Kiswahili,
Kiingereza, Kifaransa, Lingala na Kiswidi,” alisema Dekula.
Dekula
Kahanga anajivunia kwamba yeye ni mwanamuziki wa kwanza kutoka Afrika aishiye Sweden
kufyatua album. Alitoa album iitwayo ‘Dekula
Sultan Qaboos’ yenye nyimbo za Sultan
Qaboos, Mon Amour, Babylon, Mayanga (aliutunga akiwa na Marquis), Rozina, Mambo leo na Nostalgie nyimbo ambazo zinapigwa katika
vituo vingi vya redio duniani.
Ili kupata unafuu
wa maisha nchini Sweden, Dekula alilazimika kuomba uraia wa nchi hiyo baada ya
kufuata taratibu zote. Alichukua uamuzi mgumu mwingine wa kuukana uraia wa nchi
yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ili kupata uraia wa nchi hiyo. Hivi
sasa yeye na wanamuziki wenzake wa bendi hiyo ni raia halali wa Sweden.







Comments
Post a Comment