- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
NILIWAHI
kuandika wakati fulani kwamba “UKWELI WA MWANASIASA NI JINA LAKE TU” lakini wakatokea watu wengi kunikosoa, wakipinga uchambuzi wangu huo na wengine
wakinitisha kwa maneno kwa sababu tu nilikuwa nimekisema kile ambacho wao ama
wapendwa wao hawakupenda kisemwe hata kama kiko wazi.
Ilikuwa ni
wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu 2015 wakati nilipozichambua kauli
za mawaziri wakuu wa zamani – Edward Lowassa na Frederick Sumaye – waliokwenda kutafuta
hifadhi Chadema baada ya kuona ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hawana nafasi
ya kwenda Ikulu tena kama wakuu wa nchi.
Nilisema kwamba
wanasiasa hao wamefuzu katika sanaa. Bora Lowassa tunajua alisomea sanaa, lakini
Sumaye alisomea kilimo!
Baada ya
kukimbilia Chadema, kwa nyakati tofauti wanasiasa hao walitoa kauli
zilizodhihirisha kwamba ukiwa kwenye siasa lazima uwe mwongo, lakini wakasahau
kwamba, ukiwa muongo daima usiwe msahaulifu.
Kabla ya
kwenda Chadema na kuteuliwa kuwa mgombea urais, Lowassa alipata kumsifu Rais (mstaafu)
Jakaya Kikwete akisema: “Rais Kikwete ni Visionary Leader ana uwezo wa kuona
mbali”, lakini alipotua tu Chadema na kuvikwa joho la Ukawa, akasema: “Rafiki
yangu Jakaya Mrisho Kikwete ameuharibu uchumi wan chi hii”.
Yako mengi
aliyowahi kuyasema akiwa ndani ya CCM ikiwemo kuapa kwamba asingetoka ndani ya
chama hicho na ikiwa kuna mtu hamtaki, basi aondoke yeye.
Sumaye ndiye
aliyenishangaza kabisa na nitaendelea kumshangaa daima katika maisha yangu. Juni
2, 2008 alinukuliwa na gazeti la Tanzania
Daima akisema “Urais basi”, kwamba hakuwa na nia ya kuwania tena nafasi ya
urais hata itakapofika mwaka 2015, na badala yake anataka kuwa mtu wa msaada
kwa nchi za Afrika, ili ziweze kujikwamua katika lindi la umaskini. Maneno haya
aliyasema kwenye mkutano na waandishi wa habari pale kwenye Hoteli ya Protea,
zamani Court Yard, jijini Dar es Salaam.
Lakini
ghafla bin vuu akajitokeza kuwa miongoni mwamakada 42 wa CCM waliojitokeza
kutaka kupokea kijiti cha Jakaya Kikwete. Wakati akiwa na harakati za kuwania
urais, alipata kukaririwa akisema: “Endapo CCM itampitisha Lowassa kugombea
urais mimi nitahama chama.” CCM haikumpitisha Lowassa, wala yeye hakupitishwa.
Akabakia huko kwa muda na baada ya kutafakari akahama kumfuata Lowassa Chadema!
Tena basi akateuliwa kuwa Meneja wa Kampeni wa mtu aliyedai hafai kuwa rais
akiwa CCM!
Baada ya
kwenda Chadema, Sumaye huyo huyo katika uzinduzi wa kitaifa wa kampeni za
Ukawa, ndiye aliyempigia kampeni Lowassa akisema: “Lowassa anastahili urais
yeye ndiye Jemedari wetu”.
Kwa miaka
kadhaa sasa, Chadema imejipambanua kwamba ni chama kinachopinga ufisadi na
kiliweza kujijengea sifa na kuaminiwa na wananchi kwa msimamo huo, huku
kikiendesha kampeni nchi nzima kupinga ufisadi pamoja na suala la kusamehe kodi
ambalo lilikuwa linaikosesha serikali mapato makubwa.
Waliahidi kwamba,
mara watakapoingia madarakani – kama wangefanikiwa – wangeanza kusafisha
mafisadi wote na kuhakikisha kodi inakusanywa ili nchi isiwe tegemezi.
Kwa bahati
mbaya kura za Lowassa ‘hazikutosha’, hivyo CCM imeendelea kushika hatamu ya
uongozi wa taifa hili chini ya Rais John Pombe Joseph Magufuli, ambaye naye kwa
kiasi kikubwa katika kampeni zake aliahidi kupambana na ufisadi, kubana
matumizi na kuigeuza nchi kuwa ya uchumi wa viwanda, huku akienda mbali Zaidi kwa
kusema kwamba angeanzisha mahakama ya kuwashughulikia majizi na mafisadi.
Baada tu ya
kuingia madarakani akaanzisha ‘Operesheni ya Kutumbua Majipu’ kwa kusafisha
uozo wote uliokuwa ukipigiwa kelele ambao uliota mizizi kuanzia kwenye rushwa,
ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka pamoja na uzembe na kufanya kazi kwa
mazowea.
Tulishuhudia
namna serikali ilivyofanikiwa kukusanya trilioni kadhaa kwa miezi mitano ya
mwanzo na inaendelea na kasi hiyo hiyo, huku Rais Magufuli akifanya kile
ambacho hakikutarajiwa kwa kuwakamata wafanyabiashara wote wakubwa ambao
walikwepa kodi wakati wa awamu ya nne na wakalipa.
Watendaji wa
serikali wengi wakaondolewa na baadhi yao kesi zao ziko mahakamani kutokana na
kutumia madaraka yao vibaya yaliyoikosesha serikali mapato huku wananchi
wakiendelea kuogelea kwenye tope la umaskini.
Kwa hiyo
kelele hizo hazikuwa za Chadema tu, bali hata Dk. Magufuli aliziona akiwa CCM
na ndiyo maana alipopata dhamana ya kuwatumikia Watanzania akaamua kupambana
nazo kwa vitendo bila kumuonea haya yeyote.
Lakini pamoja
na jitihada hizo ambazo zilikuwa kero kubwa kwa wananchi na mtaji wa kisiasa wa
wapinzani, Chadema wanazibeza na ikafikia mahali viongozi na baadhi ya mawakili
wa chama hicho wakaanza kuwatetea wale wote ‘waliotumbuliwa’ na kufikia hatua
ya kuahidi kwamba wangeweza kwenda kuwatetea mahakamani.
Kwa maana
nyingine, Chadema wanaonekana kukerwa na utendaji uliotukuka wa Rais Magufuli
ambaye ameimarisha nidhamu ya kazi na kuhakikisha rasilimali za Watanzania
haziendi mifukoni mwa wachache.
Hapa ndipo
panapoanzia figisu zote zinazofanywa sasa na Chadema kiasi cha kuanza kumwita
Rais Magufuli ni dikteta bila kubainisha udikteta wake ni kwa vile amepambana
na ufisadi au kwa sababu amekubalika kwa wananchi kiasi kwamba wapinzani hawana
hoja ya msingi ya kuikosoa serikali.
Kitendo cha
Chadema kupinga kila jambo linalofanywa na serikali ni ukaidi ambao hauna maana
yoyote wala tija kwa taifa na kwa hatua yao ya sasa ya kuitisha maandamano ya
kupinga hicho wanachokiita ‘ufisadi’ ni kumjaribu Rais Magufuli kama ‘atawafanya
nini’.
Hapa niseme
tu kwamba, Chadema wanapima homa kwa
viganja, jambo ambalo ni la hatari. Huwezi kusema mtu ana homa kwa sababu
tu kwa kutumia kiganja unaona joto la mwili limepanda, utakuwa unakosea.
Wakati wa
utawala wa Jakaya Kikwete, ni Chadema hao hao waliomkosoa rais kwamba ‘anacheka
cheka’ na wengine wakamwita ‘Marco Polo’ au ‘Vasco da Gama’ kutokana na
kusafiri sana ughaibuni.
Leo amekuja
mtawala anayefanya kazi kwa vitendo wanamwita dikteta, kwa sababu tu ameweza
kupambana na changamoto nyingi zilizoiyumbisha serikali huko nyuma. Sasa wanataka
nini?
Kama mtawala
aliyepita alikuwa anacheka na wakamkejeli walivyotaka, sasa huyu amenuna,
hacheki wala nini, yeye anapiga kazi tu!
Chadema wamekuwa
kama ‘mtoto wa kufikia’ ambaye hata ujitahidi kumtunza namna gani, hawezi
kuridhika na atafanya visa vingi tu kumgombanisha baba na mama!
Tena hawana
tofauti na ‘ndugu wa mume’ ambao watamkosoa mke wa ndugu yao hasa ikitokea
kwamba ‘hakuwa chaguo lao’, na siyo ajabu wakamwambia ndugu yao ‘mwache
mwanamke huyu hakufai, mchoyo, au hata mchawi!’
Ndivyo
wanavyofanya Chadema kwa serikali ya awamu hii kwa sababu wao walikuwa na
matumaini kwa asilimia 200 kwamba wangeingia Magogoni baada ya kumpata ‘mchezaji’
Lowassa katika timu yao na kutumia msururu wa wafuasi wa mwanasiasa huyo
aliotoka nao CCM.
Kwa kuwa
ushindi wa Dk. Magufuli umewanyima fursa ya kuwa mawaziri, ma-RC, ma-DC, mabalozi
na kadhalika, sasa wanafanya kila namna kumtoa kasoro ili aonekane hafai, jambo
ambalo lina malengo hasi kwa taifa letu.
Kukwamisha jitihada
za serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ni kosa kubwa na kukaidi
mamlaka iliyopo ni kosa pia kwa sababu hata vitabu vya dini vinatuagiza
tuheshimu mamlaka za dunia kwa sababu “Mamlaka zote zimewekwa na Mungu”, hata
kama ulikwenda kupanga foleni kupiga kura.
Moma ni
nyoka mpole sana, lakini akiamua kushambulia hagongi kama nyoka wenyine, bali
anang’ata na kuondoka na nyama na sumu yake ni kali kiasi kwamba pale alipopang’ata
huvimba na kubadilika rangi – matokeo yake ni kifo.
Rais
Magufuli alishaonya kwamba watu wasimjaribu kwa sababu kamwe yeye hajaribiwi,
maana yake ni kwamba Chadema wasithubutu kumjaribu kwa sababu atakapochukua
hatua itakuwa ni hatari.
Hivi siyo
vitisho wala siyo udikteta, kwa sababu wakati mwingine kiongozi inabidi ufanye
lile linalofaa kwa maendeleo ya taifa lako na kitendo cha kuzuia mikutana na
maandamano ni katika kuwafanya wananchi waendelee na shughuli zao za uchumi
badala ya kuchelewa siasa – tena zile za kupinga maendeleo.
Wakati mwingine
kuna haja ya kuwapuuza wanasiasa wa aina hii kwa sababu kwa kiasi kikubwa
wanachelewesha maendeleo.
Ni maoni yang
utu.
0656-331974
Comments
Post a Comment