Featured Post

HIZI NDIZO AINA ZA MBUZI WA MAZIWA




Na Daniel Mbega
Kwa vyovyote vile, baada ya Makala zilizotangulia za Namnaya kuanzisha mradi wa ufugaji wa mbuzi wa maziwa na Faida za Mbuzi wa Maziwa, inawezekana wewe au ndugu na jamaa yako mmevutiwa na kuhamasika na ufugaji wa mbuzi wa maziwa.
Ikiwa ndivyo, basi tunaweza kuendelea kuhabarishana mambo mbalimbali yanayohusiana na ufugaji huo kwa nia ya kuleta tija kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Tuchukulie tayari umekwisha hamasika na unataka kuanzisha mradi wa ufugaji mbuzi wa maziwa. Ni vyema basi tuangalia mambo mengine ya msingi, ambayo, hata kama bado hujashawishika, yanaweza kukuhamasisha ukaingia kwenye ujasiriamali huo.
Kama nilivyoeleza katika makala iliyotangulia, mbuzi hawa wana faida nyingi, lakini ili uweze kuwafuga kibiashara na kuongeza kipato kuna mambo ambayo unapaswa kuyafahamu, bila kujali ni aina gani ya mbuzi utakaowafuga.
Kuyafahamu mambo haya mapema kutaongeza hamasa kwako wewe au mwingine yeyote ambaye atapenda.

Uchaguzi wa Mbuzi wa Kufuga
Bila kujali ni aina gani ya mbuzi utakaowafuga, ni vizuri kutambua sifa zinazofaa za mbuzi wa kufugwa.
Lengo kubwa la kuchagua mbuzi wa kufuga ni kuboresha uzalishaji na kuendeleza kizazi bora. Kuna aina nyingi za mbuzi wanaoweza kufugwa kulingana na mazingira na mahitaji ya mfugaji.
Uchaguzi hufanyika kwa kuangalia umbile, uzalishaji na kumbukumbu za wazazi kama vile umbo kubwa, ukuaji wa haraka, uwezo wa kutunza vitoto na kutoa maziwa mengi.
Mbuzi majike wanaofaa kwa ajili ya kuzalisha maziwa wawe na sifa zifuatazo:
Historia ya kukua upesi, kuzaa (ikiwezekana mapacha) na kutunza vitoto vizuri
Umbo la mstatili linaloashiria utoaji wa nyama nyingi
Asiwe na ulemavu wa aina yoyote
Awe na miguu ya nyuma iliyo imara na iliyonyooka na yenye nafasi kwa ajili
ya kiwele; na
Awe na kiwele kikubwa na chuchu ndefu zilizokaa vizuri
Dume bora anatakiwa awe na sifa zifuatazo:
Miguu iliyonyooka, imara na yenye nguvu
Asiwe na ulemavu wa aina yoyote
Mwenye uwezo na nguvu ya kupanda; na
Mwenye kokwa mbili zilizo kaa vizuri na zinazolingana

Aina ya mbuzi wa maziwa
Baada ya kujua sifa hizo za jumla, sasa tuangalie aina za mbuzi wanaofaa kwa kufugaji kwa ajili ya maziwa.
Kuna aina tatu za mbuzi wa maziwa. Kwanza kuna wale wa kigeni wanaopatikana hapa nchini kama Toggenburg, Saanen, British Alpine, German Alpine, French Alpine, Nubian, Anglo Nubian, Angora na Oberhauzen. Hawa Anglo Nibian ni uzao wa mbuzi aina ya Nubian (ambao asili yao ni Sudan) na mbuzi kutoka Uingereza.
Kuna mbuzi aina ya Malya (Blended) ambao wamezalishwa katika Kituo cha Kilimo cha Malya mkoani Mwanza ambao wanafaa kwa ajili ya nyama na maziwa na pia wapo mbuzi chotara.
Hata hivyo, wapo pia mbuzi wa asili aina ya Small East African Goat na hutoa kiwango kidogo sana cha maziwa. Lakini mbuzi hawa wanaweza kuzalishwa na mbuzi wa kigeni ili kupata chotara wanaotoa maziwa mengi na wenye uwezo wa kustahimili magonjwa na hali ya hewa ya hapa nchini.
Aina hizi zote za mbuzi hustahimili aina tofauti ya hali ya hewa na huhitaji mazingira tofauti ya kuwafuga.
Ikiwa unataka kufuga mbuzi wa maziwa ni bora kutafuta ushauri kutoka kwa wataalam wa mifugo katika eneo lako ili wakufahamishe aina nzuri ya mbuzi wanaopatikana na mbinu nzuri za kuwazalisha zinazopatikana nchini ikiwa ni pamoja na wale wanaoendana na mazingira unayotaka kuwafugia.

Aina hizi ndizo bora
Kufuga mbuzi huanza na kuchagua ni jamii gani unayoitaka kwa sababu kuna jamii zaidi ya 200 ambazo zimeendelezwa duniani kote, ingawa siyo zote zinazopatikana Tanzania ama Afrika. Uamuzi wako utategemea utashi wako kama unawataka mbuzi kwa ajili ya maziwa, nyama, nyuzi au mapambo.
Mbuzi wa maziwa ni wale ambao wanazalisha maziwa mengi kuliko wanayoweza kuwanyonyesha watoto wao.
Kununua mbuzi wa maziwa atakayekidhi mahitaji yako linaweza kuwa jambo gumu. Huwezi tu kukurupuka na kununua mbuzi kwenye mnada wa Vingunguti au Pugu, na kama unataka mbuzi mwenye afya, uzao bora na maziwa mengi huwezi kuchagua mwenye mkia ulionona. Kitu cha kwanza ambacho unapaswa kukifanya ni kuamua aina gani ya mbuzi anayefaa.
Kuna aina sita bora za mbuzi wa maziwa wa kisasa ambao wanafaa kwa ufugaji:

Nubia
Mbuzi hawa asili yao ni Nubia (Sudan) na ndio maarufu kwa ufugaji kwa ajili ya maziwa. Utawatambua mbuzi hawa kutokana na masikio yao marefu, yaliyoanguka na bua ya Kirumi.
Japokuwa mbuzi aina ya Nubia hawatoi maziwa mengi kama jamii nyingine, lakini wanafahamika kutokana na maziwa yao kuwa na mafuta mengi.
Kwa vile asili yao ni Afrika, mbuzi jamii ya Nubia wanastahimili mazingira ya joto, lakini wanaweza kumudu mazingira yoyote. Mbuzi jamii ya Nubia wanaweza wakawa weupe, kahawia na wekundu kwa weusi. Wengine wanaweza kuwa na mchanganyiko wa rangi hizo.

Saanen
Mbuzi wa Saanen (inatamkwa sah-nen) wote ni weupe na masikio yao yamesimama na nyuso ambazo ni kinyume na zile za Nubia. Kwa wastani, mbuzi jamii ya Saanen wanatoa maziwa mengi zaidi. Wafugaji wengi wa mbuzi wa maziwa wanapendelea jamii hii. Mbuzi hawa asili yao ni Uswisi na tabia zao ni za Kiswisi: kazi yao ni kutoa maziwa tu.

Hawa ni jamii pia ambayo asili yake ni Uswisi. Utawatambua kwa rangi yao ya kahawia, nyuso nyeupe na mabaka. Ni wazalishaji wazuri wa maziwa.

Zamani walikuwa wamegawanywa katika makundi ya Ufaransa na Uswisi, lakini jamii ile ya Uswisi kwa sasa inaitwa Oberhasli. Mbuzi jamii ya Alpines wana masikio yaliyonyooka na wanapatikana kwa rangi mbalimbali kuanzia weupe hadi weusi. Wengine wana mabaka ya rangi ya udongo au meusi kichwani.

LaManchas
Mbuzi jamii ya LaManchas mara nyingi wanawavutia watu kutokana na masikio yao yasiyo ya kawaida. Masikio yao ni mafupi mno na usije ukashangaa watu wanaokuja kwako kukutembelea wakakuuliza “Kwanini uliwakata maskini?” Lakini ukweli ni kwamba, hivyo ndivyo walivyozaliwa.
Lakini wewe hukamuia masikio … na kwa jamii ya mbuzi wa maziwa, hawa ndio bora zaidi. Wakati mbuzi wengine wana mabaka kwenye masikio, LaManchas wana mabaka kwenye mikia.

Oberhasli
Jamii hii, ambayo ni maarufu sana kwao Uswisi, inafahamika kutokana na umbile lake. Ina rangi ya udongo na mabaka meusi, ingawa baadhi ya majike ni meusi tii. Ni wazuri kwa uzalishaji wa maziwa ambayo ndani yake yana mafuta asilimia 3.6.

Hata hivyo, kuna aina nyingine ya mbuzi wa maziwa. Kuna wale wanaoitwa African Pygmy (au Pygmy) na Nigerian Dwarf ambao hufugwa kama wanyama marafiki kuliko uzalishaji wa maziwa, ingawa baadhi yao, hasa Nigeria Dwarf, wanazalisha maziwa.
Mbuzi jamii ya Kinder ilikuwa ni mzao chotara wa bebeeru la Pygmy na jike la Nubia. Mbuzi hao chotara ni wakubwa kuliko Pygmy na Nigerian Dwarf, lakini siyo wakubwa kama jamii nyingine. Hawa pia wanatoa maziwa mengi kuliko wale wadogo.
Pia kuna jamii nyingine kama Angora na Tennessee Fainting au Wooden Leg, na kwa sasa mbuzi jamii ya Boer (Kaburu). Lakini hao wanafungwa kwa ajili ya nyuzi au nyama, na mara chache sana wanafikiriwa kwa ajili ya maziwa.
Jamii gani ni bora zaidi? Swali hilo halina jibu. Kila jamii ina wafuasi wake kulingana na ubora na mazingira, na kwa kadiri ya uzalishaji wa maziwa ulivyo, kunaweza kukawepo na tofauti kubwa ndani ya jamii moja kuliko jamii kwa jamii.
Wafugaji wengi huanza na mbuzi wenye asili mchanganyiko ambao wanapatikana kwa urahisi.
Hata hivyo, ni vyema kuwaona maofisa mifugo waliopo jirani nawe ili wakuelekeze jamii bora ya kufuga kulingana na ubora na mazingira uliyopo.

Baada ya kuzijua jamii bora za mbuzi wa maziwa, sasa tutaichambua jamii moja baada ya nyingine ili kama imetokea unataka kuwafuga, ama unawafuga tayari, uweze kuwaelewa tabia na uwezo wao pamoja na ustahimilivu wa magonjwa.
Ikiwa una maoni au ushauri, usisite kunipigia au kunitumia ujumbe wa simu au whatsapp kupitia namba 0656 331974 au nitumie barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.


Comments