- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
RAIS MAGUFULI AMZAWADIA PETER TINO KIWANJA NA PESA SHILINGI MILIONI 5, AFUNGUA AKAUNTI CRDB NA KUZIWEKA
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa
Stars) Peter Tino akimshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kumzawadia shilingi Milioni 5 kwa kutambua mchango wake kwa Timu ya Taifa
ya mwaka 1980 ambapo goli lake liliiwezesha Tanzania kufuzu fainali ya Michuano
ya Soka Barani Afrika (AFCON) wakati Rais Magufuli alipokutana na kuwapongeza
wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ambao jana waliifunga Timu
ya Taifa ya Uganda (The Cranes) na kufanikiwa kufuzu kucheza fainali za AFCON
2019 zitakazofanyika baadaye mwezi Juni 2019 huko Misri.
Na Sultani Kipingo
Mchezaji
wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Peter Tino leo
amekabidhiwa shilingi Milioni 5 alizopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua mchango wake kwa Timu ya
Taifa ya mwaka 1980 ambayo ilifuzu kuingia fainali Michuano ya Soka Barani
Afrika (AFCON).
Mchezaji
Peter Tino ndiye aliyefunga goli lililoiwezesha Tanzania kuingia fainali
hizo na tangu mwaka huo wa 1980 Tanzania
haikuwahi kufanikiwa tena kuingia hatua hiyo mpaka mwaka 2019 ikiwa ni miaka 39
imepita.
Peter Tino
alialikwa Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 25 Machi, 2019 wakati Mhe. Rais
Magufuli alipokutana na kuwapongeza wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania
(Taifa Stars) ambao jana waliifunga Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) na
kufanikiwa kufuzu kucheza fainali za AFCON 2019 zitakazofanyika baadaye mwezi
Juni 2019 huko Misri.
Pamoja na
kupatiwa shilingi Milioni 5, Peter Tino pia ameunganishwa katika zawadi ya
kupatiwa kiwanja Jijini Dodoma kwa kila mchezaji wa Taifa Stars iliyotolewa na
Mhe. Rais Magufuli ambapo naye atapatiwa kiwanja cha kujenga nyumba.
Peter Tino
amezeweka pesa hizo katika akaunti yake ya Benki ya CRDB aliyoifungua mara tu
baada ya kutoka Ikulu na kukabidhiwa kadi yenye taarifa zake za benki (ATM).
“Hakika
Mungu ni mkubwa” amesema Peter Tino baada ya kupokea kadi yake ya Benki kwa
Meneja Biashara wa Tawi la CRDB la Azikiwe, Bw. George Yatera, akishuhudiwa na
Afisa kutoka kutoka TFF Bw. John Michael
Mashaka. “Hela hii sikuiota hata ndotoni na mradi Raisi wetu mpendwa John Pombe
Magufuli kanikumbuka hakika sintomwangusha. Yaani nitakwenda kumalizia kibanda
changu kule Morogoro,” aliongezea.
Afisa wa
Benki hiyo Bi. Gloria Kaale ndiye aliyemsajili mchezaji huyo ambaye wadogo
zake, Gebbo Peter na Emma Peter, nao walitikisa anga za soka nchini kwa nyakati
tofauti siku za nyuma kabla ya na wao kustaafu. Familia yao kwa sasa inaishi
Morogoro.
Kwa mujibu
wa kumbukumbu zilizopo, ilikuwa ni Agosti 26,1979 wakati timu ya soka ya Taifa,
Taifa Stars ilipokuwa ikirudiana na timu ya soka ya Taifa ya Zambia katika mechi
ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za
mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria.Pambano hilo lilichezwa mjini Ndola.
Mechi hiyo
ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Taifa Stars kwa vile ilikuwa ikihitaji sare ya
aina yeyote ili iweke historia ya kufuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya
kwanza , tangu ilipoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 1968. Katika mechi ya
kwanza iliyochezwa wiki mbili nyuma kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
Taifa Stars iliishinda Zambia bao 1-0. Bao hilo lilifungwa na kiungo Mohammed
Rishard Adolph.
Ushindi
huo ulipatikana kwa mbinde kiasi kwamba mashabiki wengi hawakuwa na imani iwapo
Taifa Stars ingeshinda ama kupata sare katika mechi ya marudiano. Na hivyo ndivyo
ilivyokuwa kwani Wazambia walifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika za mapema
na kudumu nalo kwa takriban dakika 86.
Zikiwa
zimesalia dakika tatu pambano hilo kumalizika, mshambuliaji mrefu mwenye kasi
na mashuti makali, Peter Tino alibadili sura ya mchezo na kufanya kile
kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa mchezo huo nchini.
Ilipigwa
kona kwenye lango la Taifa Stars, kipa Juma Pondamali akaupangua mpira kwa
ngumi, ukamkuta kiungo Leodegar Tenga, aliyetoa pasi ndefu kwa kiungo mwenzake,
Hussein Ngulungu, ambaye naye alitoa pasi ndefu kwa Tino.
Akiwa
amezungukwa na mabeki watatu wa Zambia, Tino alilazimika kupiga hesabu za
haraka haraka. Aliwachomoka mbio mabeki nao na kukimbia na mpira kwa kasi.
Alipofika nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia, alifumua shuti kali la mguu
wa kulia, lililompita kipa Shileshi wa Zambia na mpira kutinga wavuni.Bao hilo
lilipatikana baada ya pasi tatu.
Katika
mechi hiyo, Taifa Stars iliwakilishwa na kipa Juma Pondamali, mabeki ni Leopard
Tasso, Mohammed Kajole/Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, viungo ni Leodegar
Tenga, Hussein Ngulungu na washambulaji ni Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed
Salim na Thuweni Ally.
Kikosi
hicho kilikuwa chini ya Kocha Slowmir Work kutoka Poland, akisaidiwa na Wazawa
Joel Bendera na Ray Gama (ambao kwa sasa wote ni marehemu), ndicho
kilichoiwakilisha Tanzania katika fainali za kombe hilo zilizofanyika nchini
Nigeria.
Katika
fainali hizo, Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na wenyeji Nigeria katika mechi
ya ufunguzi, ilitoka sare ya mabao 2-2 na Ivory Coast kabla ya kuchapwa mabao
2-1 na Misri na kutolewa hatua ya makundi.
Hiyo
ilikuwa ni miaka 39 iliyopita ambapo hivi sasa, baada ya kuichapa Uganda mabao
3-0 Jumapili, kila Mtanzania ameweka matumaini kwenye kikosi hicho kipya
kilicho chini ya kocha kutoka Nigeria, Emmanuel Amunike.
Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania
(Taifa Stars) Peter Tino leo akikamilisha kufungua akaunti ili aweke shilingi Milioni
5 alizopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kutambua mchango wake kwa Timu ya Taifa ya mwaka 1980 ambapo goli
lake liliiwezesha Tanzania kufuzu fainali ya Michuano ya Soka Barani Afrika (AFCON).
Wanaoshuhudia ni Meneja Biashara wa Tawi la CRDB la Azikiwe, Bw. George Yatera
na Afisa kutoka kutoka TFF Bw. John
Michael Mashaka. Kushoto ni Afisa wa Benki hiyo Bi. Gloria Kaale ambaye ndiye
aliyemfungulia akaunti nyota huyo wa zamani.
Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania
(Taifa Stars) Peter Tino akielekezwa na
Meneja Biashara wa Tawi la CRDB la Azikiwe, Bw. George Yatera namna na kutumia kadi yake ya ATM baada ya kukamilisha kufungua akaunti ili
aweke shilingi Milioni 5 alizopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua mchango wake kwa Timu ya Taifa ya
mwaka 1980 ambapo goli lake liliiwezesha kufuzu fainali ya Michuano ya Soka
Barani Afrika (AFCON). Kushoto ni Afisa
wa Benki hiyo Bi. Gloria Kaale
Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania
(Taifa Stars) Peter Tino akikabidhiwa kadi yake ya ATM kutoka kwa Meneja Biashara wa Tawi la CRDB la Azikiwe,
Bw. George Yatera baada ya kukamilisha kufungua
akaunti ili aweke shilingi Milioni 5 alizopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua mchango wake kwa Timu ya
Taifa ya mwaka 1980 ambapo goli lake liliiwezesha kufuzu fainali ya Michuano ya
Soka Barani Afrika (AFCON). Wanaoshihudia ni Afisa kutoka kutoka TFF Bw. John Michael Mashaka na Afisa wa
Benki hiyo Bi. Gloria Kaale ambaye ndiye
Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa
Stars) Peter Tino akionesha kadi yake ya ATM
baada ya kukamilisha kufungua akaunti ili aweke shilingi Milioni 5 alizopewa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa
kutambua mchango wake kwa Timu ya Taifa ya mwaka 1980 ambapo goli lake liliiwezesha
kufuzu fainali ya Michuano ya Soka Barani Afrika (AFCON).
Comments
Post a Comment