- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akiwa na Balozi
Getrude Mongella kabla ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda kidogo cha kuchakata
zao la muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani Kisarawe.
NA DANIEL MBEGA, KISARAWE
SPIKA wa zamani wa
Bunge la Afrika, Balozi Getrude Ibengwe Mongella, amemtabiria mambo makubwa
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akisema kwamba anaamini atafika
mbali katika uongozi wa nchi hii.
Balozi Mongella,
ambaye alipata umaarufu kimataifa alipoongoza Mkutano wa Wanawake uliofanyika
Beijing, China mwaka 1995 akiwa mwenyekiti, alisema mkuu huyo wa wilaya atafika
mbali katika uongozi na kinachotakiwa ni kuendelea kuchapa kazi bila kusikiliza
kelele za pembeni, kwani hata yeye alikumbana na vikwazo vingi.
“Nilifurahi sana
ulipoteuliwa, nami nilianza harakati za siasa nikiwa binti mdogo kama wewe,
nikakumbana na vikwazo vingi sana, lakini sikugeuka nyuma, kushoto wala kulia,
ndiyo maana niliweza kufika mbali.
“Hata wewe unayo
nafasi kubwa ya kufika mbali, unaweza kuwa rais wetu katika siku za mbele kwa
sababu naamini wanawake tunaweza,” alisema Balozi Mongella wakati wa uzinduzi
wa kiwanda kidogo cha kuchakata muhogo katika Kijiji cha Kitanga wilayani
Kisarawe hivi karibuni, ambapo DC Mwegelo alikuwa mgeni rasmi.
Mama Mongella
alipongeza jitihada zilizoanzishwa na DC Mwegelo wilayani Kisarawe za
kuhakikisha kwamba hakuna ‘sufuri’ katika elimu, huku akisema kwamba elimu ndio
msingi mkubwa unaoweza kulikomboa taifa.
“Unafanya kazi
nzuri sana, nimekuona mwenyewe siku moja unakimbia huku umevaa kombati,
nilifarijika sana kwa sababu hata mimi nilianza nikiwa binti kama wewe,
nakuombea uendelee na kasi hiyo hiyo ya kuwaletea watu maendeleo na ndiyo itakayoonyesha
ufanisi wa utendaji kazi wako,” alisema Mama Mongella.
Kwa upande wake,
DC Mwegelo alisema anashukuru kupata nasaha kutoka kwa Balozi Mongella, ambaye
kwake amekuwa mwanamke wa mfano katika uongozi kutokana na utendaji wake katika
ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Nimefarijika mno
kukutana na Mama Mongella ambaye kwangu amekuwa ‘role model’, binafsi
ninatamani sana walau kufikia hata nusu ya mafanikio uliyofikia, ingawa ni kazi
ngumu,” alisema.
Mkuu huyo wa
wilaya alitumia nafasi hiyo kujitambulisha katika Kijiji cha Kitanga, ambapo
aliwataka wananchi kubuni na kushiriki shughuli za maendeleo kwa kuzingatia
kwamba Serikali, chini ya Rais Dkt. John Magufuli, imedhamiria kwa dhati
kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Alisema kwamba,
wilaya hiyo ina ardhi kubwa yenye rutuba na kuwahamasisha wananchi kushiriki
kilimo ili kuzalisha malighafi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda ili
kwenda na falsafa ya Serikali ya kuifanya Tanzania ya Viwanda.
“Nawaombeni tushirikiane
katika maendeleo, tushiriki kilimo hasa cha mihogo na korosho na Serikali
inaendelea kuandaa mazingira bora zaidi kuboresha kilimo pamoja na kuwatafutia
masoko,” alisema.
Siku hiyo mkuu
huyo wa wilaya, akimwakilisha Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani
Jafo, ambaye ni Mbunge wa Kisarawe, aliweka jiwe la msingi la kiwanda kidogo
kinachomilikiwa na akinamama wakiongozwa na Abia Magembe, ofisa kilimo mstaafu
ambaye amejikita katika kilimo cha muhogo pamoja na kuchakata na kutengeneza
bidhaa mbalimbali.
Kiwanda hicho,
ambacho ni sehemu ya Mradi wa Green Voices unaofadhiliwa na taasisi ya Women
for Africa Foundation inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Maria
Thereza de la Vega, kinachakata muhogo ili kupata unga ambao unatumika
kuzalisha bidhaa mbalimbali.
DC Mwegelo aliwapongeza
akinamama hao na kuahidi kwamba, Serikali itakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha
wanasonga mbele katika kujiletea maendeleo.
“Nawapongeza sana
akinamama, pamoja na kiongozi wenu Mama Magembe, hakika hizi ni jitihada
zinazotakiwa kuungwa mkono na serikali yangu itafanya kila njia kuona kwamba
mnasimama,” alisema.
Aidha, aliwapongeza
wafadhili wa Mradi wa Green Voices waliotoa mafunzo kwa akinamama 15 huko
Hispania, ambapo akinamama 10 kati yao, akiwemo Mama Magembe, walianzisha
miradi ya aina hiyo baada ya kurejea nchini huku wakiwafundisha akinamama
wengine.
Miradi mingine ni
utengenezaji wa majiko banifu, ufugaji wa nyuki, kilimo cha uyoga, kilimo
nyumba (green house) cha mboga mboga, ukaushaji wa matunda na mbogamboga kwa
kutumia umeme-jua, kilimo cha matunda, kilimo cha viazi lishe pamoja na
utengenezaji wa majiko ya umeme-jua.
Miradi hiyo iko
katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Morogoro, Kigoma na Mwanza.
Balozi Getrude
Mongella ni Mjumbe wa Bosi ya taasisi ya Women for Africa
Foundation.
Comments
Post a Comment