- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema kuanzia sasa, visimbuzi vya Starmedia,
Digtek, Continental na TING vitaanza kuonyesha chaneli zote za ndani bila
kutoza gharama yoyote kwa mtazamaji.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya
Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema serikali
imefikia uamuzi huo baada ya visimbuzi vya Azama, Zuku na DSTV kuzuiwa kuonyesha chaneli za ndani kulingana na aina
ya leseni zao.
Akifafanua kuhusu mazungumzo kati ya Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, na wadau pamoja na
wamiliki wa vituo mbalimbali vya
televisheni nchini yaliyofanyika mapema
jana, Dkt. Abbasi alisema kuwa kuanzia
sasa chaneli zote za ndani zinapaswa kuonekana bila kutoza gharama yoyote kwa
mtazamaji.
“Ningependa Watanzania wafahamu kwamba kuanzia sasa
visimbuzi vya TING, Starmedia, Continental na Digtek vitaonyesha takriban
chaneli 34 za ndani bure, ili kutoa fursa ya kila mwananchi kuwa na haki ya
kupata taarifa,” alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, alielezea kuwa wadau hao pamoja na wamiliki wa vituo
vya televisheni wameonyesha kuridhishwa na hatua hiyo ya kwa vile Serikali
imetengeneza miundombinu itakayoruhusu chaneli zao kuonekana nchi nzima.
Dkt. Abbasi, alisisitiza kuwa “tayari nchi imeandaa mifumo
ya kuhakikisha kwamba bila kutegemea kampuni za nje, au zilizosajiliwa nje ya
nchi, tulishajenga mifumo ya ndani ya kusaidia kurusha matangazo nchi nzima”
Vilevile, aliwatoa hofu watazamaji kwa kusema kuwa kufikia Septemba
5, mwaka huu visimbuzi vyote vitakuwa na chaneli zote za ndani bila kutoza
gharama yoyote kwa mtazamaji.
Kuhusu baadhi ya wateja kulalamikia visimbuzi vya Starmedia,
kutoonyesha chaneli za ndani, Dkt. Abbasi alisema wameshaagizwa kuvifungua
vyote na zoezi hilo litaendelea hadi Septemba 5 ambapo wataonekana nchi nzima.
Dkt. Abbasi, alisema visimbuzi vya Azama, Zuku na DSTV hao
wataendelea kuonyesha maudhui mengine lakini siyo chaneli za ndani kama leseni
zinavyowataka.
Comments
Post a Comment