- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ukosefu wa uadilifu ni
moja ya eneo ambalo lilitia doa utendaji wa sekta binafsi hususan pale ambapo
ilishirikiana na Serikali.
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Agosti 28 ,2018) wakati
akifungua Mkutano Mkuu wa 18 wa mwaka wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania
(TPSF) kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Hoteli ya
Serena, jijini Dar Es Salaam, Waziri Mkuu amesema uadilifu ni changamoto kubwa
inayopaswa kufanyiwa kazi na Serikali na TPSF.
“Katika kusisitiza
suala la uadilifu, nitoe rai kwamba muwe na mfumo wa kujitathmini, kupeana
alama chanya na kuhimizana kuenenda katika misingi bora ya uendeshaji wa
shughuli zenu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ameitaka TPSF ijifunze kwa wenzao
walioendelea kwa kutokuwa na vitendo vya rushwa, kutoa adhabu kwa wanaoenda
kinyume na misingi ya uadilifu walijiwekea.
Amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wamejiongezea nguvu yao
kama taasisi lakini pia kupeleka ujumbe kwa wanachama wao kuwa wanathamini haki
na kuchukia rushwa.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa shughuli za sekta binafsi
zimeendelea kuongoza katika kuchangia pato la Taifa na ukuaji wa uchumi kwa
ujumla.
Amesema kwa mujibu wa takwimu sekta ya utalii inachangia
asilimia tisa, huduma asilimia 35, kilimo asilimia 26.6, madini asilimia 3.3 na
sekta ya viwanda inachangia takribani asilimia 10.
“Jukumu letu sote ni kuchochea uzalishaji na kufanya
wepesi kwa wajasiriamali wetu watoke nje ya mipaka yetu na kwenda
kuuza bidhaa zetu nchi jirani. TPSF mtusaidie katika hili.”
Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake itaendelea
kuweka mazingira wezeshi kwa kuboresha miundombinu, kutoa vivutio kwenye kodi,
kanuni na sheria ili kukuza sekta binafsi.
Hivyo, Waziri Mkuu amesema sekta binafsi nchini nayo haina
budi kutumia vema fursa hiyo ya uwepo wa mazingira wezeshi na rafiki kwa
kuwekeza kwenye uchumi wa nchi.
Amesema ni vema wakatambua kwamba wana jukumu kuliletea
Taifa maendeleo, hivyo wafanye kazi kwa ukaribu na ubia baina yao ili
kuhakikisha nchi inanufaika na fursa zilizopo.
Pia amewasihi waendelee kuwekeza zaidi kwenye uzalishaji wa
bidhaa za viwandani na wahakikishe kuwa wanajali maisha ya Watanzania ambao
ndio soko na wateja wa bidhaa zao.
Comments
Post a Comment