- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Ofisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) Rose Mahendeka akitoa elimu juu ya msamaha wa riba na
adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi wakati wa semina elekezi kwa
wafanyabiashara na wadau mbalimbali (hawapo pichani) iliyofanyika mkoani Tabora
kwa lengo la kuwahamasisha wafanyabiashara hao kutuma maombi ya msamaha huo
kabla ya tarehe 30 Novemba, 2018.
Na Veronica Kazimoto, Tabora
29 Agosti, 2018
Wafanyabiashara wenye malimbikizo ya madeni ya kodi
wametakiwa kutuma maombi ya msamaha maalumu wa riba na adhabu kwenye
malimbikizo hayo mapema kabla ya tarehe 30 Novemba, 2018 ili waweze kunufaika
na msamaha huo ambao umetolewa kwa lengo la kutoa unafuu kwa kuwapa fursa ya
kulipa kodi ya msingi ndani ya mwaka wa
fedha wa 2018/19.
Wito huo umetolewa na Afisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi kutoka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Rose Mahendeka wakati wa semina elekezi kwa
wafanyabiashara, wadau na washauri wa wafanyabiashara kuhusu msamaha huo iliyofanyika
leo mkoani Tabora.
“Nachukua fursa hii kutoa wito kwenu wafanyabiashara kutuma
maombi ya msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi ambapo
mwisho wa kutuma maombi ya msamaha huu ni tarehe 30 Novemba, 2018,” alisema
Mahendeka.
Mahendeka aliongeza kuwa “Mara nyingi wafanyabiashara huwa
mnajitokeza mwishoni kabisa mwa tarehe zinazoonyesha mwisho wa kulipa,
kuwasilisha au kutuma maombi fulani suala linalosababisha foleni na msongamano
mkubwa katika kutoa huduma katika ofisi zetu. Nachukua fursa hii kuwaomba
msisubiri tarehe za mwisho kuleta barua za maombi ya msamaha huu wa riba na adhabu
ya madeni ya kodi na naomba mjue kwamba, huu ndio muda muafaka wa kila mwenye
malimbikizo ya madeni kutuma maombi Ofisi ya TRA katika mkoa wake kikodi.”
Naye, Afisa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka hiyo Chama Siriwa
alisema muombaji wa msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya kodi anapaswa
kutoa maelezo na vielelezo vya ukweli na uhakika wakati wa uwasilishaji wa
maombi yake.
“Kila muombaji anatakiwa kutoa taarifa za ukweli wakati
anaomba msamaha huu na endapo itabainika kuwa muombaji ametoa taarifa za
udanganyifu, Kamishna Mkuu anayo haki kisheria kubatilisha na hivyo kupelekea
muombaji kupoteza sifa za kufaidika na
msamaha huu, ” alifafanua Siriwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mihayo iliyopo
mkoani hapa inayomilikiwa na Taasisi ya Dini ya Kanisa Katoliki Padri Salvatory
Maganga, ameishukuru TRA kwa kutoa Elimu ya msamaha wa riba na adhabu ya madeni
ya malimbikizo ya kodi na kuomba elimu hii iendelee kutolewa kwa
wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini.
Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea kutoa elimu ya msamaha
huu hususani kwa wafanyabiashara, wadau na washauri wa wafanyabiashara kwa
lengo la kuwahamasisha kutuma maombi ya msamaha huu kabla ya muda uliopangwa
haujamalizika ambao ni tarehe 30 Novemba, mwaka huu.
Comments
Post a Comment