- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akiagana na mgeni wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Group Duniani kutoka Uingereza, Bill Winters, baada ya kumalizika mkutano kati yao ambapo Benki hiyo kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa Dola Bilioni 1.46 (trilioni 3.3) ili kutekeleza mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa kutoka Morogoro hadi Dodoma.
NA BENNY MWAIPAJA, WFM, DAR ES SALAAM
BENKI ya Standard Chartered Group ya Uingereza imekubali
kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa dola za Marekani bilioni 1.46 sawa na zaidi ya
shilingi trilioni 3.3 kwa ajili ya kujenga kipande cha Reli ya Kiwango cha
Kimataifa (SGR) kuanzia Morogoro hadi Makutupora, mkoani Dodoma.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Philip Mpango, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki hiyo, Bill Winters, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mpango ameishukuru Benki hiyo kwa kukubali
kugharamia ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa ambayo lengo lake ni kuimarisha
usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo kwenda bara na nchi jirani za
Maziwa Makuu na zile ambazo hazipakani na Bahari.
"Tunajenga Reli hiyo ya Kisasa kutoka Dar es
Salaam - Morogoro hadi Makutupora ambazo ni awamu mbili lakini pia tutajenga
reli hiyo kuelekea Isaka mpaka Mwanza na baadaye Rusumo ambapo wenzetu wa nchi
ya Rwanda, tutasaidiana, wao watajenga reli hiyo kutoka Rusumo hadi Kigali,"
aliongeza Dkt. Mpango.
Aidha, Dkt. Mpango alimweleza kiongozi huyo wa juu
kabisa wa Standard Chartered Group anayeongoza Benki hiyo kwenye nchi zaidi ya
60 duniani, kuhusu vipaumbele vikubwa vya nchi ikiwemo kuboresha Shirika la
Ndege la Taifa-ATCL, na Ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme wa Mto Rufiji,
Stiegiler's Gorge.
"Tunaimarisha Shirika letu la Ndege ili
kuimarisha sekta ya utalii kwa sababu tuna vivutio vingi na haipendezi wageni
wanao kuja nchini wanafikia nchi jirani, sasa ifike wakati tuwe na uwezo wa
kuwasafirisha moja kwa moja kuja nchini kwetu" Alisisitiza Dkt. Mpango.
Alisema Tanzania ni ya pili duniani kwa kuwa na
vivutio vingi vya utalii ikitanguliwa na Brazil lakini inapokea watalii
wasiozidi milioni 2 kwa mwaka jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka
ili sekta hiyo ichangie uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa kupitia fedha za
kigeni.
Alisema katika kulifufua Shirika hilo la Ndege,
tayari Serikali imenunua ndege nne ikiwemo ndege kubwa aina ya Boeing 787- 8
Dreamliner na kwamba ndege nyingine 3 zitakuwa zimewasili nchini ifikapo mwezi
Juni, mwakani, na kulifanya shirika hilo kuwa na ndege 7.
Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha
huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji na kuendeleza ujuzi kwa wananchi
ili waweze kufanyakazi kwenye viwanda na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa
ujumla kwa kuwa maendeleo yanahusu watu.
Akizungumza kwenye mkutano wake na Dkt. Mpango,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Group, Bill Winters,
ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kiuchumi na kwamba Benki yake
itatoa mkopo huo na kuahidi kuwa balozi wa kuelezea mafanikio makubwa ya
kiuchumi ya Tanzania kwa wadau wengine.
Aliahidi kuzishawishi taasisi nyingine za fedha
ulimwenguni kuangalia uwezekano wa kuunga mkono jitihada hizo ambazo mwisho
wake wanufaika wakubwa watakuwa ni wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla.
"Tunaimani kubwa na uwezo wa Tanzania pamoja
na fursa nyingi za kiuchumi ilizonazo na kwamba miradi mingi ya kipaumbele
iliyoainishwa itafikiwa na tunalo jukumu kama Benki kutoa fedha na kuiweka
miradi hiyo pia sokoni ili iweze kupata fedha" Alisisitiza Bill Winters.
Katika kikao hicho, Bill Winters aliambatana na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo nchini Kenya na nchi za Ukanda wa Afrika
Mashariki, Lamin Manjang na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo nchini Tanzania,
Sanjay Rughani, ambapo pia Benki hiyo inafanya shughuli zake hapa nchini kwa
kipindi cha miaka 101 sasa.
Comments
Post a Comment