- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Wananchi wakimsikiliza kwa makini, Mhe.
Jaji Mugeta (hayupo pichani) alipokuwa akizindua rasmi programu ya utoaji elimu
kwa wananchi/wateja wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam.
Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu,
Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga akizungumza na Wananchi
waliokuwepo wakati wa hafla hiyo, waliosimama nyuma ni baadhi ya Watumishi wa
Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Baadhi ya Maafisa wa Mahakama
walioshiriki katika hafla hiyo wakiwa wamejumuika pamoja na wananchi, wa pili
kulia ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu, Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Said Ding’ohi
na mwenye koti jeupe ni Bi. Wanyenda Kutta, Mkurugenzi Msaidizi-Utawala,
Mahakama ya Tanzania.
Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es
Salaam akisalimiana na wananchi mara baada ya kuzindua rasmi zoezi la utoaji
elimu kwa wananchi wanaofika kupata huduma katika Kanda hiyo. Mhe. Jaji Mugeta
alimuwakilisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe.
Beatrice Mutungi.
…………………………
Na Mary Gwera
Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam imezindua rasmi
programu maalum ya kuzungumza na wateja wake kwa lengo la kutoa elimu kuhusu
taratibu mbalimbali za Kimahakama na vilevile kuongeza uwazi katika utoaji wa
huduma zake.
Akizindua rasmi zoezi hilo mapema Agosti 29, kwa niaba ya
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu- Kanda ya Dar es Salaam; Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda
ya Dar es Salaam, Mhe. Ilvin Mugeta alisema kuwa zoezi hili ni miongoni mwa
maboresho ya Mahakama ikiwa ni mkakati wa kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi.
Katika maneno yake ya ufunguzi, Mhe. Jaji Mugeta alisema
kuwa zoezi hilo litakuwa likifanyika mara moja kwa juma, ambayo ni Jumatano ya
kila wiki kuanzia saa 02:00 asubuhi hadi saa 02:15 asubuhi.
“Sisi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, tumeona ni vyema
tukawa na muda mfupi angalau mara moja kwa wiki kuzungumza na wateja wetu na
Umma wote kwa ujumla kuhusu huduma zetu,” alisema Jaji Mugeta.
Kwa upande wake, Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda
ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga alisema kuwa lengo la kampeni hiyo si tu
kutoa elimu bali pia kupokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wateja kwa lengo
la kujiboresha zaidi katika utoaji wa huduma zake.
Tiganga alitoa wito kwa wananchi kutosita kutoa malalamiko
yao kwa Watumishi wa Kanda hiyo ikiwemo Manaibu Wasajili na Makarani ili waweze
kupatiwa ufumbuzi.
Aidha; mbali na kuwaona Wasajili na Makarani wa Kanda hiyo,
Mhe. Tiganga aliwataka wananchi pia kutuma Malalamiko yao kwa njia ya ujumbe
mfupi wa maandishi kupitia simu nambari 0735 501 400.
Nao baadhi ya Wananchi walioshiriki katika uzinduzi huo
waliipongeza Mahakama kwa uamuzi huo kwani itawasaidia kujua zaidi taratibu
mbalimbali za Mahakama na kuondoa baadhi ya maswali waliokuwa wakijiuliza.
Rajab Mwimi na Bi. Hamisa Chaurembo ni miongoni mwa wananchi
walioshiriki katika zoezi hilo, ambapo waliipongeza Mahakama Kanda ya Dar es
Salaam kwa kuanzisha huduma hiyo ambayo itawarahisishia katika kutafuta huduma
ya haki zao.
“Zoezi hili nimelipokea vizuri na nimelipenda, tunaishukuru
Mahakama kwa kusikiliza kero za wananchi na kutuelimisha, vilevile naiomba
iendelee kusukuma mashauri haraka na haki zitendeke bila upendeleo,” alieleza
Bi. Chaurembo.
Zoezi la utoaji elimu kwa wananchi na kuwasikiliza wateja
wanaofika katika Mahakama nchini tayari limeshaanza katika Kanda mbalimbali za
Mahakama, ikiwa ni pamoja na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Tabora, Dodoma na
kadhalika.
Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake imejiwekea
nguzo kuu tatu moja ya nguzo hizo ni ya Kurejesha imani ya jamii na
Ushirikishwaji wa Wadau ambapo kupitia nguzo hii Mahakama inafanya jitihada
mbalimbali ili wananchi waweze kujua
zaidi huduma na maboresho yanayojiri kwa manufaa ya wananchi kwa kuwa wao ndio
wadau wakubwa wa Mhimili huu.
Comments
Post a Comment