- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WACHEZAJI sita wa Simba, mabeki Shomari Kapombe, Erasto
Nyoni, viungo Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga na mshambuliaji na nahodha,
John Bocco, wameenguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa
Stars, kinachojiandaa na mechi dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini
Kampala kwa utovu wa nidhamu.
Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike amechukua hatua hiyo baada
ya wachezaji hao kushindwa kuripoti kambini juzi, hoteli ya Sea Scape, eneo la
Kunduchi jijini Dar es Salaam bila taarifa yoyote, huku mwenzao, kipa, Aishi
Salum Manula pekee akiripoti
Badala yake, Amunike, winga wa zamani wa kimataifa wa
Nigeria, amewachukua mabeki, Ally Sonso, Paul Ngalema wa Lipuli ya Iringa,
Salum Kimenya wa Tanzania Prisons ya Mbeya, David Mwantika, viungo Frank Domayo
wa Azam, Salum Kihimbwa na mshambuliaji Kelvin Sabato, wote wa Mtibwa Sugar.
Wachezaji walioripoti kambini hadi sasa ukiondoa
walioongezwa ni makipa Aishi Manula wa Simba na Mohammed Abdulrahman wa JKU, mabeki ni Aggrey Morris, viungo
Mudathir Yahya na mshambuliaji Yahya Zayed wa Azam.
Wachezaji wa Yanga, kipa Benno Kakolanya, mabeki Gardiel
Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’ na kiungo Feisal Salum ambao
wapo na timu yao mjini Kigali, Rwanda ambako jana walimenyana na wenyeji, Rayon
Sport katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, watajiunga na timu wakirejea
kuanzia kesho Iiumaa.
Nyota wanaocheza nje wanatarajiwa kuwasili kuanzia Septemba
1 ambao ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC
ya Afrika Kusini, Himid Mao wa Petrojet FC ya Misri, Simon Msuva wa Difaa
Hassan El-Jadida, Morocco, Farid Mussa, Shaaba Iddi wa CD Tenerife ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya
Botswana, Thomas Ulimwengu wa El HIlal ya Sudan na nahodha Mbwana Samatta wa
KRC Genk ya Ubelgiji.
Amunike aliyesaini mkataba wa kufundisha Taifa Stars mapema
mwezi huu, ambaye anasaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na Mzalendo,
Hemed Suleiman ‘Morocco’, baada ya mechi na Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini
Kampala, atawafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa
kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Comments
Post a Comment