- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mtuhumiwa mmoja aliyeuawa na wananchi wenye hasira baada ya
kukutwa akichimbua kaburi la marehemu Sisala Simwali huko Mbeya.
WATU wasiofahamika wamefukua kaburi la Bandusamile Mwalyebe
'Kanjanja' (65) mlemavu wa ngozi (albino) aliyefariki mwaka 2012 katika Kitongoji
cha Mbande, Kijiji cha na Kata ya Ngonga wilayani Kyela mkoani Mbeya, kisha
kuondoka na mifupa na baadhi ya viungo
kwa kile kilichodaiwa ni imani za kishirikina kwa lengo la kupata
utajiri.
Mashuhuda wa tukio hilo juzi walilieleza gazeti hili kuwa
imani za kishirikina ndiyo chanzo cha kufanya unyama huyo kwa watu hao ambao
bado hawajafahamika wakiwa na lengo la kusaka utajiri baada ya kwenda kwa
mganga wa kienyeji (Sangoma) aliyepiga ramli katika nchi jirahi ya Malawi.
Hatua hiyo ya kufukuliwa kaburi la mtu mwenye ualbino
limezua taharuki kwa wakazi wa wa eneo hilo huku wakidai kuwa tukio hilo halijawahi
kutokea katika kijiji hicho toka dunia ianze, huku wakieleza kuwa watafanya
msako ili kuwatambua wahusika wa tukio hilo.
Betina Buruma, mtoto wa kaka wa marehemu, alisema alipoamka
asubuhi, aliona kaburi limefukuliwa alipokuwa akichuma majani ya mchaichai,
hivyo akatoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji ambaye naye alitoa taarifa
kituo cha polisi wilaya ambao walifika eneo la tukio.
Alisema polisi walipofika walifanya upekuzi na kugundua kuwa
jeneza (sanduku) limevunjwa huku mifupa ikichukuliwa na watu hao wasiojulikana
na kuwa baba yake alikuwa muasisi wa kucheza ngoma za asili aina ya Mang'oma.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Malima Mwaisango, alisema
kuwa baada ya kupokea ttaarifa hiyo alipiga simu polisi ambao walifika eneo la
tukio kujionea hali halisi na kusema kuwa kitendo kilichofanyika ni chukizo kwa
mungu kwani imetokana na imani za kishirikina.
Mmoja wa walemavu wa ngozi katika kata hiyo, aliyejitajwa
kwa jina la Gwantwa Mwalyaje, alisema imani za kishirikina zimewafanya waishi
kwa hofu kwani maeneo mbalimbali amesikia wenye ualbino wakikatwa viungo na kuuawa
kinyama.
''Hali hii inatufanya tuishi kwa hofu na kutokuwa na uhakika
na maisha yetu,kutokana na watu wenye imani za kishirikina wamekuwa wakisema
Albino ni dili,wamekuwa wakituua kinyama huku wengine wakiwa hawana viungo
baada ya kukatwa na watu hao kisha kutokomea navyo," alisema Mwalyaje.
Mwalyaje alizungumza kwa taabu huku akibubujikwa na
machozi,aliiomba serikali kuwachukuliwa hatua watu hao pindi watakapobainika
huku akiomba waongezewe ulinzi ili waweze kuishi kwa uhakika akieleza kuwa
wanalazimika kurudi nyumba mapema pindi waendapo kwenye shughuri mbalimbali
wakihofu kutekwa.
Akizungumza na wananchi mara baada ya kubaini kuchukuliwa
kwa mifupa ya mremavu wa ngozi,mkuu wa upepelezi wa jeshi la pilisi wilayani
humo, Modestus Chambu, alithibitisha tukio hilo,na kusema kuwa wamefungua
jarada la uchunguzi ili kuwabaini watu waliousika na tukio hilo ili wachukuliwe
hatua za kisheria.
Aidha amewaomba wananchi kutoa ushirikiano na jeshi la
polisi kuwasaka wathusika na kudai kuwa vitendo kama hivyo havipaswi kufanyika
kwani ni aibu kwa kijiji na wilaya nzima kwa tukio hilo la kuwawinda kama
wanyama watu wenye ulemavu wa ngozi.
Alisema vitendo kama hivyo ni chukizo kwa mungu havipaswi
kufanywa, kwani watu hao ni sawa na watu wengine ''hii dunia inakoelekea si
kuzuri watu wanapaswa kuwa waungwana kuacha kutegemea imani hizo za hovyo
wakidhani kufanya hivyo watapata mafanikio ya kimaisha," alisema.
Imebainika kuwa matukio kama hayo ya ufukuaji wa makaburi ya
watu wenye ulemavu wa ngozi (ALBINO) ni muendelezo wa matukio baada ya mwaka 2017
katika Wilaya ya Mbeya Vijijini baadhi ya watu walikamatwa wakituhumiwa kufukua
kaburi la Sisala Simwali, mwenye ulemavu wa ngozi, ambapo walifikishwa mahakamani huku mmoja akiuawa na wananchi wenye hasira katika eneo la tukio.
Na pia mwaka huo huo katika Kata ya Miyovizi, wilaya ya
Mbozi, kaburi la mtu mwenye ulemavu wa ngozi aliyekufa miaka sita iliyopita pia
lilifukuliwa na kuchukuliwa mifupa na watu wasiofahamika ambapo hadi leo hakuna
mtu ama watu waliokamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
Machungaji wa Kanisa la Temple of Pray For All Nations,
Nabii Charles Mkuvasa, wilayani Kyela alisema kutokana na kuwepo kwa matukio
haya ipo haja ya viongozi wa dini mbalimbali kuongeza maombezi kuliombea Taifa
hili ili watu wenye imani za kishirikina waache kufanya ukatili huo.
Nabii Mkuvasa alisema Watanzania baadhi wenye tabia kama
hizo waache kwani mambo hayo ni chukizo kwa Mungu, badala ya kutegemea kupata
mali kwa njia za kishirikina kwa kudhuru wenzao, badala yake wamshirikishe
mungu na wafanye kazi za kihalali na kuachana na ushirikina ambao hauna tija.
Comments
Post a Comment