- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
KAMPALA, UGANDA
MBUNGE wa Uganda na msanii Bobi Wine hakuhudhuria kikao cha
mahakama hii leo kuhusiana na kesi ya uhaini iliyowasilishwa dhidi yake na
serikali.
Mmoja wa mawakili wake, Tonny Kitara, anasema kuwa Bobi Wine
bado amelazwa katika hospitali moja mjini Kampala kufuatia majeraha aliyopata
wakati alipokamatwa na wanajeshi.
Mwanamuziki huyo anatarajiwa kusafirishwa kwa matibabu
ijapokuwa haijulikani anatarajiwa kupelekwa wapi.
Watu 25 waliokuwa wameshtakiwa pamoja naye katika mahakama
ya hakimu mkuu mjini Gulu waliwasili mahakamani humo kaskazni mwa Uganda
kulingana na Kitara.
Jumla ya watu 33 wameshtakiwa na uhaini kufuatia madai
kwamba waliupiga mawe msafara wa rais Yoweri Museveni.
Baadhi ya washukiwa hao hawakuonekana mahakamani kwa sababu
ya hali mbaya ya kiafya ama mkanganyiko wa siku ya kusikizwa kwa kesi hiyo .
Stakhabadhi zao za dhamana kwa makosa zilisema kuwa
wanatarajiwa kuwasili mahakamani Septemba 30 na sio Agosti 30. Kesi hiyo
imeahirishwa hadi Oktoba Mosi.
Baadhi ya washtakiwa wanaendelea kupata matibabu hospitalini
na huenda wakashindwa kuhudhuria mahakamani ambapo watawakilishwa na mawakili
wao.
Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi ni
mwakilishi wa Jimbo la Kyadondo Mashariki na ni msanii maarufu wa muziki nchini
Uganda.
Alikamatwa wiki mbili zilizopita kwa tuhuma za uvamizi wa
msafara wa Rais Museveni mjini Arua na kupokea kipigo kikali yeye na wenzie 32
kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama. Dereva wa Bobi Wine alipigwa risasi na
kuuawa katika purukushani hizo.
Watuhumiwa hao waliwekwa chini ya ulinzi wa jeshi huku Bobi
Wine awali akipandishwa katika mahakama ya kijeshi kwa tuhuma za kumiliki
silaha kinyume cha sheria.
Rais Yoweri Museveni alijitokeza na kukanusha taarifa kuwa
Bobi Wine ameumizwa vibaya na kuvishutumu vyombo vya habari kwa kueneza taarifa
za uongo.
Baada ya kelele za upinzani kupazwa ndani na nje ya Uganda
pamoja na kwenye mitandao ya kijamii, kesi yake mbele ya mahakama ya kijeshi
ilifutwa na kuachiwa huru kabla ya kukamatwa tena na kufunguliwa mashtaka ya
uhaini katika mahakama ya kiraia.
Jumatatu wiki hii, Bobi Wine na washukiwa wengine wote
waliachiwa kwa dhamana.
Comments
Post a Comment