- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Sanamu ya Baphomet inayotumiwa na Satanic Temple
CALIFORNIA, MAREKANI
BINADAMU tangu zama za kale amekuwa akijenga, kuchonga na
kuweka sanamu za aina nyingi kwa sababu mbalimbali.
Baadhi hutumiwa kuwaenzi watu maarufu na kuwakumbuka, na
nyingine huabudiwa kama miungu.
Kwa muda mrefu hata hivyo, imekuwa ni nadra kuona sanamu
ambayo moja kwa moja inahusishwa na shetani au ibilisi.
Lakini ukifika Marekani, mambo ni tofauti.
Kuna sanamu moja kubwa ya shaba ambayo inahusishwa na
ushetani.
Ni sanamu ya Baphomet, kiumbe mwenye kichwa kinachofanana na
cha mbuzi lakini ameongezwa maungo ya ajabu.
Ni kiumbe huntha mwenye mabawa, na kwenye sanamu hiyo
inayotumiwa kwa sasa huoneshwa akiwa na watoto wawili wanaotabasamu.
Sanamu inayotumiwa kwa sasa ina urefu wa karibu futi 9, na
iligharimu $100,000 (takriban shilingi za Kitanzania milioni 230) kuitengeneza.
Sanamu hii imekuwa ikitumiwa kuwapiga vita wale walio na
imani za Kikristo na imani nyingine zenye kumcha Mungu mmoja. Ni sanamu hii
ambayo imekuwa ikitumiwa kuendesha vita dhidi ya kuwekwa kwa sanamu za Kikristo
na dini nyingine katika majengo maarufu, bustani na maeneo ya umma nchini
Marekani.
Agosti 17, 2018 sanamu hiyo ya kiumbe anayefahamika kama
Baphomet ilipelekwa katika Jimbo la Arkansas anakotoka rais wa zamani wa
Marekani, Bill Clinton.
Wanaotumia sanamu hiyo ni watu wa kundi linalofahamika kama
Satanic Temple (Hekalu la Shetani) ambalo ni kundi la 'kidini' na kisiasa
ambalo hupinga kuingizwa kwa dini katika masuala ya serikali.
Kundi hilo liliandaa maandamano ya watu 150 waliyojumuisha
waabudu shetani, watu wasioamini Mungu yupo na Wakristo pia.
Maandamano hayo yalifanyika nje ya jengo lililo makao makuu
ya Jimbo la Arkansas katika Mji wa Little Rock.
Walikuwa wamekerwa na hatua ya kuweka sanamu ya Mnara wa
Amri Kumi za Mungu katika uwanja wa makao makuu hayo.
Satanic Temple walisema sanamu hiyo inakiuka Sheria ya
Kwanza ya Marekebisho ya Katiba nchini Marekani ambayo huzungumzia uhuru na
haki za kidini.
"Ikiwa utakubali kuwepo kwa sanamu ya dini moja basi kunafaa
kuwa na uhuru kwa wengine kuweka sanamu za kidini, na ukizuia basi kusiwe na
sanamu yoyote ile," mwanzilishi mwenza wa tawi la Satanic Temple katika Jimbo
la Arkansas, Ivy Forrester, alinukuliwa na wanahabari siku hiyo ya maandamano.
Ndoto yao ni kuwa na sanamu ya kudumu, lakini siku hiyo
hawakuruhusiwa na sheria kuiweka kwa muda mrefu. Kuna sheria ya Arkansas ya
mwaka 2017 inayohitaji sanamu ya kuwekwa maeneo ya serikali iwe na udhamini wa
mbunge ambaye atawasilisha muswada iidhinishwe kupitia Bunge.
Sanamu hiyo ya Mnara wa Amri Kumi za Mungu ilidhaminiwa na
mwanasiasa wa Republican, Seneta Jason Rapert. Hata hivyo, chini ya saa 24
baada ya kuwekwa, mwanamume mmoja alivurumisha gari na kuugonga mnara huo na
kuubomoa.
Maandamano ya Satanic Temple Arkansas yalisababisha
kuandaliwa kwa maandamano mengine ya kuwapinga yaliyoandaliwa na makundi ya
Kikristo na wanachama wa Republican. Wakristo walikuwa wamebeba karatasi
zilizokuwa na ujumbe kutoka kwenye Biblia.
Satanic Temple waliwasilisha ombi la kushirikishwa kwenye
kesi ya kupinga mnara huo wa Amri Kumi za Mungu iliyowasilishwa na shirika la
haki za kiraia la American Civil Liberties Union, lakini kundi hilo
limewasilisha ombi kutaka wasishirikishwe kwenye kesi hiyo.
Sanamu ya Detroit
Sanamu hiyo ya Baphomet ilizinduliwa mara ya kwanza katika
mji wa Detroit, Michigan.
Mipango ya kuuweka nje ya makao makuu ya Jimbo la Oklahoma
ambapo kulikuwa kumewekwa mnara mwingine wa Amri Kumi za Mungu mwaka 2015.
Mnara huo ulizinduliwa Julai 25, 2012, ambapo kupitia taarifa,
SatanicTtemple walisema: "Tulichagua Baphomet kwa sababu ni kiumbe ambaye
huhusishwa na Shetani na maana inayohusishwa naye inafaa sana akiwekwa kando na
sanamu inayowakilisha dini nyingine."
Sherehe ya kuuzindua ilikuwa ya faragha, na ukumbi uliotumiwa
uliwekwa siri kubwa kwani Wakristo walikuwa wameandamana awali kuipinga mjini.
Picha zilizopakiwa kwenye Facebook zilionyesha uzinduzi wake ulifanyika karibu
na Mto wa Detroit.
Waliohudhuria sherehe ya uzinduzi walihudhuria kwa mwaliko
Kabla ya uzinduzi huo kufanyika, waumini takriban 200
walihudhuria ibada ya misa katika kanisa la St. Joseph mjini humo kupinga
sanamu hiyo. Wengine 50 walifanya maombi mjini katika eneo ambalo awali Satanic
Temple walikuwa wamepanga kuuzindulia mnara huo hapo.
Mwanamume yule yule aliyeuharibu mnara wa Arkansas anadaiwa
kufanya vivyo hivyo na kuubomoa mnara mwingine kama huo wa Amri Kumi za Mungu
nje ya makao makuu ya jimbo la Oklahoma.
Satanic Temple walisitisha juhudi zao za kutaka kuweka
sanamu ya Baphomet huko baada ya Mahakama ya Juu ya Oklahoma kuamua kwamba
Sanamu ya Mnara wa Amri Kumi za Mungu ilikuwa imewekwa kinyume cha sheria,
hivyo wakawa wameshinda vita bila kupigana.
Mahakama ilisema ni kinyume cha sheria kutumia mali ya umma
kwa manufaa ya dini yoyote ile.
Jina Baphomet lilitoka wapi na asili yake wapi? Jina hili asili
yake ni enzi ya kukomesha uasi katika Kanisa Katoliki katika miaka ya 1100, kwa
Kiingereza Inquisition, na kuteswa kwa wapiganaji wa kidini kwa jina Knights
Templar waliokuwa wanateswa ili wafichue siri zao na wakubali kuifuata dini kwa
mujibu wa viongozi wa kanisa wa wakati huo.
Kwa mujibu wa waandishi wa enzi za vita vya kidini maarufu
kama Crusade, wapiganaji hao walikiri kumuabudu mungu wa wapagani kwa jina
Baphometh.
Baadhi ya wasomi hata hivyo huamini kwamba
"Baphometh" ni upotoshaji wa jina "Mahomet" - ambalo
hutumiwa kumrejelea Mtume Muhammad, jambo linalozua utata zaidi.
Lakini kadiri miaka ilivyosonga na mafumbo na siri kuwahusu
tata na Knights Templar kuzidi, ndivyo ufafanuzi wa neno hilo na maana yake
ulivyozidi kutofautiana.
Moja ya ufasiri wa neno hilo unapatikana katika kitabu cha
Da Vinci Code cha Dan Brown ambapo neno Baphomet limefafanuliwa na kutafsiriwa
kama "Sophia" au busara.
Baphomet kwa mujibu wa
Levi
Picha maarufu zaidi ya Baphomet ilichorwa na mwanamizungu wa
Ufaransa, Eliphas Levi, mwaka 1856 katika kitabu chake cha Transcendental Magic: Its Doctrine and Ritual.
Alichora kiumbe huntha mwenye mabawa na mwenye pembe na
mwenge ulio katikati ya pembe hizo kichwani.
Kuna mchoro pia wa pembe nane kwenye paji la uso.
Mikononi kumeandikwa maneno ya Kilatino SOLVE (tenganishwa) na COAGULA
(fungamanisha) - ambazo ni nguvu za kuunganisha na kutenganisha ambazo
zilitwaliwa kutoka kwa Mungu.
Mchoro wa Levi ulihamasisha zaidi sanamu inayotumiwa na
Satanic Temple.
Ni jinsia mbili kwa pamoja, nusu mnyama na nusu binadamu.
Saluti ya vidole
viwili
Sanamu hiyo ina vidole viwili vilivyoelekezwa juu mkono wa
kulia na viwili vinavyoelekezwa chini mkono wa kushoto, maana yake "kama
ilivyo juu, na chini iwe pia".
Maneno hayo na ishara hiyo ya vidole ni maarufu miongoni mwa
wenye kuamini katika mizungu na mafumbo.
Chanzo chake ni kazi za kale za msomi Hermes Trismegistus,
ambaye vitabu vyake vilikuwa maarufu sana enzi ya Kipindi mwamko-sanaa na
mageuzi ya kidini, maarufu kama Renaissance and Reformation barani Ulaya.
Maneno hayo pia hutumiwa kuhusiana na sayansi, vitu vyote na
Mungu, lakini Levi aliandika kwamba kwa kutumia ishara hiyo, Baphomet wake
alikuwa anaashiria kuwiana sawa kwa fadhila na haki.
Watoto wawili
Lucien Greaves, msemaji wa Satanic Temple anasema lengo lao
ni kwamba watoto watatazama kazi hiyo ya sanaa kama salama, isiyofaa kuzua
wasiwasi wowote.
"Sura ya mbuzi huyo haioneshi chochote. Si ya kishetani
wala ya kutisha - kama wanavyodai baadhi ya watu - ukiitazama bila kuongozwa na
mzigo wa utamaduni."
Lakini watoto hawafai kumuogopa Shetani?
"Sifikiri watoto wanaokutana na sanamu hii bila kutiwa
hofu na propaganda wanaweza kuona chochote cha kuwatia wasiwasi," anasema
Greaves.
"Lakini si kwamba tunapinga kuwaingiza watoto kwenye
mitazamo ya kidini. Mara nyingi watoto hulazimishwa kuingia kwenye dini. Hilo
ni jambo hatutaki kulifanya kamwe."
Caduceus
Kwenye tumbo la Baphomet kuna ishara ya kale ya Kigiriki ya
nyoka wawili walio kwenye fimbo - fimbo ambayo ilibebwa na Hermes na maafisa wa
kueneza matangazo au kutoa matangazo rasmi waliotumiwa kutoa matamko rasmi.
Ishara hiyo kwenye sanamu hiyo inaashiria biashara,
mashauriano na kutendeana, na iliingizwa kwenye Baphomet na Levi.
"Kwetu ni ishara ya maridhiano ya vitu viwili tofauti -
kwa mfano kuwa na sanamu ya Kishetani karibu na sanamu ya Kikristo,"
anasema Greaves.
"Tunafikiri ni ujumbe wenye nguvu sana kuwa na sanamu
hii ikiwa karibu na sanamu ya Amri Kumi za Mungu. Unaweza kuwa na mambo mawili
tofauti kwa pamoja bila mzozo."
Maziwa
Baphomet wa Levi alikuwa huntha mwenye maziwa, lakini
"tuliyaondoa maziwa hayo" anasema Greaves. Anasema hakutana wajipate
kwenye mdahalo kuhusu jinsia ya kiumbe huyo wao jambo ambalo lingewafanya watu
kupoteza maana halisi.
Badala yake anasema watoto wawili, mvulana na msichana, ndio
wanaowakilisha jinsia.
'Pentagram'
Kwenye paji la uso la Baphomet na kwenye kiti cha enzi
alichokikalia kuna mchoro wa nyota ya pembe tano, ishara ambayo mara nyingi
hutambuliwa kama ishara ya shetani.
Mara nyingi huonekana ikiwa imepinduliwa.
Msalaba wa Peter pia hupinduliwa.
Greaves anasema lengo lao ni kuwafanya watu wabadilishe
mtazamo wao na kuacha kuongozwa na waliyofunzwa na utamaduni wao. Waangazie
mambo kwa kuzingatia ushahidi uliopo.
Anasema mtazamo huo huwazuia watu kuchukua msimamo huru
kuhusu masuala kama vile ndoa za wapenzi wa jinsia moja na haki za kutoa mimba
pamoja na huduma nyingine za uzazi wa mpango.
Mwenge kati ya pembe
"Mwenge wa maarifa ndio kama upembe wa kati - na
inatukuza juhudi za kutafuta elimu na maarifa. Tunathamini hilo sana,"
anasema Greaves.
Levi mwenyewe aliandika kwamba mwenge wa maarifa uolikuwa
unawaka katikati ya pembe za Baphomet ni mwanga wa kusawazisha vitu vyote. Ni
taswira ya roho iliyo juu ya vitu vyote vinavyoonekana, kama zilivyo ndimi za
moto, ingawa bado imeunganishwa na vitu hivyo, mfano moto unavyoendelea kung'aa
juu ya mafuta au kijiti.
Maandiko
Kulikuwa na mpango wa kuongeza maandiko kwenye mchoro wa
nyota ya pembe tano ya moja ya nguzo saba kuu za Satanic Temple: "moyo wa
huruma, busara na haki unafaa daima kuongoza zaidi ya neno lililoandikwa au
kutamkwa."
Nyuma ya sanamu hiyo, kutakuwa na nukuu kutoka kwenye kitabu
cha Cain cha mwandishi Lord Byron
unaosema: "Kisha, nani alikuwa Ibilisi? Yule hangekuruhusu wewe uishi
milele, au yule ambaye angelikuumba uishi milele, katika raha na nguvu za elimu
na maarifa?"
Satanic Temple ndio
nani?
Kwa mujibu wa tovuti yao, Satanic Temple wanaamini kwamba
"kimsingi watu kuteseka au kuumia ni vibaya, na chochote kile
kinachopunguza madhila na mateso ni kizuri."
Hawaamini katika kutenda mabaya.
Wanasema: "Huwa tunakumbatia kukufuru kama njia halali
ya kujieleza na kuonyesha uhuru wa mtu binafsi dhidi ya imani za kitamaduni
zisizo na tija."
"Msimamo wa Satanic Temple ni kwamba dini inaweza, na inafaa
kutenganishwa na ushirikina. Hivyo basi, huwa hawaendelezi imani katika Shetani
binafsi.
"Kukumbatia jina la Shetani ni kukumbatia mtazamo wa
kutumia fikra na kujindoa kutoka kwenye mfumo wa kuamini katika nguvu za
kipekee za kutoka nje ya dunia na utamaduni uliopitwa na wakati wenye msingi
wake katika ushirikina."
CHANZO: BBC SWAHILI
Comments
Post a Comment