- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
nchini Marekani, Steve Dowd (wa pili kulia), wakikagua kituo cha kusambaza
umeme cha Zuzu jijini Dodoma, ikiwa ni moja ya miradi ya nishati inayofadhiliwa
na AfDB kwa kushirikiana na Serikali.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (
katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini
Marekani,Steve Dowd (wa pili kulia), wakikagua kituo cha kusambaza umeme cha
Zuzu jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (
katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Benki ya maendeleo ya
Afrika ( AfDB), watendaji wa Wizara ya Nishati, pamoja na Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) baada ya kufanya ziara katika kituo cha kusambaza umeme cha
Zuzu jijini Dodoma.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (
wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika( AfDB)
nchini Marekani,Steve Dowd (wa pili kulia), wakiwa katika picha ya pamoja
katika moja ya Transfoma zilizopo katika kituo cha kusambaza umeme cha Zuzu
jijini Dodoma.
………………….
AfDB yaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya nishati ya
umeme wanayoifadhili
Yaahidi kuendelea kutoa ufadhili utakaohusisha uondoaji wa
miundombinu mibovu ya umeme jijini Dodoma
Na Zuena Msuya, Dodoma
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeahidi kuendelea
kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika kuimarisha miundombinu ya
umeme nchini hususan katika Mkoa wa Dodoma ili kuboresha upatikanaji wa huduma
ya umeme kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uwekezaji.
Uboreshaji wa hali ya umeme mkoani Dodoma unahusisha uondoaji wa miundombinu mibovu na chakavu
zikiwepo takribani transifoma 75, kujenga njia ya kusafirisha umeme yenye urefu
wa kilometa 135 kuzunguka Jiji, pamoja na kujenga vituo viwili vya kupokea na
kupoza umeme katika eneo la Msalato na Kikombo vitakavyokuwa na uwezo wa kufua
umeme wa takribani Megawati 200.
Waziri wa Nishati, Dkt.
Medard Kalemani alisema hayo katika kituo cha kupokea na kupoza umeme
cha Zuzu jijini Dodoma,wakati wa ziara
ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini
Marekani, Steve Dowd, aliyekuwa akikagua utekelezaji wa baadhi ya miradi ya
nishati ya umeme inayofadhiliwa na Benki hiyo katika mikoa mbalimbali nchini.
“Katika mazungumzo yangu na AfDB kabla ya kufanyika kwa
ziara hii, pia wameonyesha nia ya kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa Jua wa
megawati 100 katika eneo la Zuzu jijini Dodoma katika kipindi cha miaka miwili
ili umeme huo uingizwe katika Gridi ya taifa,” alisema Dkt Kalemani.
Akizungumzia miradi ya nishati, Dkt. Kalemani aliutaja mradi
mkubwa wa umeme na wa kwanza nchini wa megawati 400 (National Backbone), kuwa
ni miongoni mwa miradi mikubwa iliyotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na
mashirika mbalimbali ikiwemo AfDB.
Alifafanua kuwa, katika utekelezaji wa mradi huo, Serikali
ya Tanzania ilitoa shilingi Bilioni 18, Benki ya Maendeleo Afrika ( AfDB)
ilitoa Dola za Marekani milioni 64.5 kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo
la Japan( JICA), Benki ya Uwekezaji Ulaya (EIB), Benki ya Dunia( WB) na Benki
ya Korea.
Aliongeza kuwa mradi huo wa Backbone unahusisha ujenzi wa
Kituo cha kupoza umeme cha Zuzu ambacho kitaongezwa uwezo wa kusambaza umeme
kutoka Megawati 48 za sasa hadi kufikia Megawati 200.
Alisema kuwa, baada ya kukamilika kwa miradi hiyo, mji wa
Dodoma utakuwa mahitaji ya umeme wa megawati 70 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo,
na megawati 108 kwa miaka kumi ijayo, huku Mpango wa serikali kwa miaka kumi na
mitano ijayo, ni kuwa na zaidi ya megawati 210, ili mkoa uweze kujitosheleza.
“Tunataka Mji wa Dodoma uwe ni mji wa mfano kwa kuwa na
umeme mwingi na wa kutosha,na wa uhakika kwa kuwa viwanda vingi sasa
vitaanzishwa katika Mkoa wa Dodoma, na uwekezaji mkubwa utafanyika kwa muda
mfupi, kutokana na mkoa huo sasa kuwa na hadhi ya Jiji na Makao Makuu ya nchi,
hivyo umeme ni lazima uwepo wa kutosha na wa uhakika,” alisisitiza Dkt.
Kalemani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo
Afrika (AfDB) nchini Marekani, Steve Dowd alisema kuwa ameridhishwa na
utekelezaji wa miundombinu ya umeme inayofadhiliwa na Benki hiyo hapa nchini
baada ya kukagua na kuona namna ambavyo inavyotekelezwa.
Dowd alisema kuwa, Benki hiyo itaendelea kushirikiana na
Tanzania katika kufadhili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati ya umeme
kwa kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea kiuchumi ambazo zinafanya vizuri katika
utekelezaji wa nishati hiyo kulingana mahitaji na ubora unaotakiwa na kwa
wakati.
“Nimefurahi kutembelea baadhi ya miradi hii ya nishati
inayofadhiliwa na AfDB ambayo inatumia fedha nyingi. Kwa kweli mnafanya vizuri,
nimeridhishwa na kasi ya kuwaletea wananchi wenu maendeleo kupitia sekta ya
nishati, AfDB itaendelea kuwaunga mkono katika hili, tuendelee kushirikiana,”
alisisitiza Dowd.
Akizungumzia namna ambavyo AfDB inashirikiana na Tanzania,
Dowd aliishauri serikali ya Tanzania, kuendelea kuomba fedha za kutekeleza
miradi ya maendeleo kutoka katika nyanja mbalimbali, kwa kuwa inatekeleza
miradi hiyo kama ilivyotarajiwa.
Comments
Post a Comment