- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI
RAIS mstaafu wa Marekani Barack Obama amesema ulimwengu umo
kwenye njia panda na kwamba kuna mitazamo miwili tofauti kuhusu ubinadamu.
Amesema hayo akihutubu katika mhadhara wa kila mwaka wa
Nelson Mandela nchini Afrika Kusini ambao huandaliwa kila mwaka kama sehemu ya
maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa kwa kiongozi huyo wa zamani wa Afrika Kusini.
Obama amesema enzi hizi ni za watawala walio na ubabe na
kwamba demokrasia haitiliwi uzito sana.
Huku akionekana kumkosoa mrithi wake Donald Trump, Obama
amesema watawala wenye nguvu wanahujumu karibu kila taasisi ya serikali ambayo
huleta maana kwa demokrasia.
Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 na mwaka huu ni karne moja
tangu kuzaliwa kwake.
Obama amesema kiongozi huyo aliyepambana dhidi ya utawala wa
ubaguzi wa rangi Afrika Kusini alikuwa mtu shujaa kweli na anayefaa kukumbukwa
katika historia.
Ametoa wito kwa watu kujifunza mengi zaidi kutoka kwa
uongozi wake na kujenga jamii ya kuvumiliana ambapo demokrasia na tofauti baina
ya jamii tofauti vinathaminiwa na kusema kwamba vijana wanafaa kutekeleza
mchango muhimu katika kuangusha watawala wa kiimla.
Obama amesema kuna kizazi kizima cha watu ambao wamekulia na
kulelewa katika ulimwengu uliojaa uhuru zaidi na wa kuvumiliana.
"Hili linafaa kutupatia matumaini," ameongeza.
"Lakini ulimwengu unakabiliwa na tishio la kurejea
katika mtindo wa zamani na hatari zaidi na katili wa kufanya mambo.
"Ni lazima tuanze kwa kukubali kwamba sheria zote
ambazo huenda zilikuwepo kwenye vitabu …. Miundo ya zamani ya hadhi na mamlaka
na unyanyasaji vyote viliangamizwa, lakini havikuangamizwa kabisa,"
amesema.
Uongozi wa kiimla
Obama amesema kwamba Marekani changamoto dhidi ya utandawazi
mwanzoni zilitoka kwa wanasiasa wa mrengo wa kushoto na kisha zikaanza kutokea
kwa wanasiasa wa mrengo wa kulia.
Amesema madhara ya kudorora kwa uchumi wa dunia mwaka 2008 -
na kutomakinika kwa wasomi na watawala - vilizifanya ahadi zilizotolewa kwa
watu kuwa hewa tu.
"Siasa za kuwatia watu hofu na kutoridhika na kuwa na
misimamo mikali zilianza kuwavutia watu. Na siasa za aina hiyo sasa zinashika
kasi," Bw Obama amesema.
Ameongeza kwamba hawatii watu wasiwasi lakini anaeleza
ukweli uliopo.
Amesema katika enzi za viongozi wa kisiasa wenye mamlaka
makuu, demokrasia huwa ni kivuli tu.
"Viongozi wenye nguvu kuu kisiasa wameanza
kuchipuka...wale walio mamlakani hujaribu kuhujumu kila taasisi au utamaduni
unaoipatia demokrasia maana," ameongeza.
Obama pia amesema watu wanafaa kuondoka kwa mtazamo wa
kusaidiwa tu na badala yake walio na mali na mamlaka wafikirie kuwekeza zaidi
katika jamii zilizotengwa.
"Ni lazima tuwekeze katika maeneo hayo ya dunia
yasiyobahatika. Kuna vipaji kila pahali," ameongeza.
Ubaguzi
Obama amesema hushangaa sana kwamba wakati huu ni lazima
kwake kuwakumbusha watu kuhusu kuwaheshimu watu wa rangi, asili, dini na
wapenzi wa jinsia moja.
Amesema anashangazwa na hilo kwamba linafanyika miaka mingi
baada ya Nelson Mandela kuondoka gerezani.
"Inaonekana ni kama tunaelekea kwa siasa za
kukaripiana, mapambano ya kuhakikisha haki za msingi bado hayakamilika kwa
kweli. Ni lazima tuwe macho dhidi ya watu wanaojaribu kujitukuza kwa kuwashusha
hadhi wengine," amesema.
Mandela aliachiwa kutoka gerezani mwaka 1990 na kuwa raia wa
kwanza mweusi Afrika Kusini mwaka 1994.
Itazame timu ya
Ufaransa
Barack Obama amesema usawa katika jamii huwezesha vipaji vya
kila mmoja kuifaa jamii.
"Itazame timu ya taifa ya kandanda ya Ufaransa,"
amesema. "Si wote walionekana kama wa asili ya zamani ya Ufaransa, lakini
wote ni Wafaransa - ni Wafaransa."
Ufaransa walishinda Kombe la Dunia Jumapili kwa mara ya pili
katika miaka 20, wakiwa na kikosi ambacho wengi wa wachezaji ni wahamiaji au
wazazi wao walikuwa wahamiaji.
BBC
Comments
Post a Comment