- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Doto James, akipokea kitabu cha maadhimisho ya miaka 10 ya Shirika la
la Maendeleo la Kimataifa la Ufaransa (AFD) nchini Tanzania, kutoka kwa
Mkurugenzi Mtendaji wa AFD, Remy Rioux, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Jijini Dodoma. (Picha na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)
NA BENNY
MWAIPAJA, WFM, DODOMA
SERIKALI ya Ufaransa kupitia
Shirika lake la Maendeleo (AFD), itaipatia Tanzania mkopo wenye
masharti nafuu wa Euro milioni 500, sawa na takriban Shilingi
trilioni 1.3, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji, nishati na usafirishaji,
kupitia Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo (2017-2021).
Hayo yamesemwa Jijini
Dodoma, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, alipokutana
na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa
(AFD), Remy Rioux, ambapo ujumbe wa Tanzania na Ufaransa umejadili namna ya
kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili uliodumu kwa zaidi ya
miaka 58.
"Kupitia makubaliano
hayo, AFD itakuwa inatoa Euro milioni 100 kila mwaka, sawa na karibu shilingi
bilioni 267 kwa kipindi cha miaka mitano, kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo
muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu," alisema James.
James amesema kuwa fedha
hizo ni tofauti na Euro milioni 600 ambazo shirika hilo limeipatia
Tanzania kama msaada na mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza
miradi mikubwa hapa nchini ukiwemo Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Ziwa
Victoria unaohusisha mikoa ya Mwanza, Bukoba na Musoma ambapo Serikali hiyo
ilitoa Euro milioni 45.
Miradi mingine
inayofadhiliwa na Shirika hilo ni pamoja na Mradi wa Kuendeleza Sekta ya Maji
Awamu ya Pili (WSDP II), Mradi wa Vituo vya kupoza umeme kupitia TANESCO,
na Ujenzi wa njia ya Umeme kutoka Geita hadi Nyakanazi na mingine mingi ambayo
kwa pamoja imefikia thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.055.
James ameishukuru Serikali
ya Ufaransa kupitia AFD kwa namna inavyoshiriki katika kuleta maendeleo ya nchi
na watu wake kupitia ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuiomba
iendelee kuangalia maeneo mengine ya vipaumbele vya taifa ikiwemo kilimo, elimu
na miundombinu mingine.
Akizungumza katika kikao
hicho kilichowashirikisha pia viongozi waandamizi wa pande zote mbili,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Remy Rioux, amesema
kuwa Shirika lake litaangalia namna ya kutoa fedha zingine kwa ajili ya miradi
mipya ya kipaumbele iliyoainishwa na Katibu Mkuu-Hazina, Doto James, ukiwemo
mradi mkubwa wa Bwawa la Maji wa Farkwa utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha lita
za ujazo 37,000 kwa siku kwa ajili ya wakazi wa Jiji la Dodoma, uliopangwa
kugharimu Dola la Marekani milioni 420.
"Tuko tayari pia
kufadhili ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme jua katika mkoa wa Shinyanga na
tutakamilisha majadiliano yetu na Wizara ya Nishati ili kufadhili mradi wa
kuunganisha umeme kati ya Tanzania na Zambia pamoja na kushiriki kwa kutoa
fedha katika Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza" aliongeza Rioux.
Alisema pia kuwa Shirika
lake liko tayari kuelekeza nguvu zake katika kukuza sekta zingine ikiwemo Sekta
ya utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa-TANAPA, Shirika la Simu
Tanzania-TTCL, na Taasisi nyingine ambazo serikali itaona zina umuhimu wa
kupata rasilimali fedha kutoka AFD kwa ajili ya kusukuma haraka gurudumu la
maendeleo ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema kuwa Shirika lake
ambalo juzi limesherehekea miaka kumi tangu lianze kufanya shughuli zake hapa
nchini, limeamua kuanzisha Ofisi yake ya Kudumu nchini Tanzania badala ya
kutegemea Ofisi yake iliyopo Nairobi Kenya, baada ya kuridhika na kutambua
jitihada kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano za kuleta mapinduzi makubwa ya
kiuchumi.
"Tumeamua kufanya hivyo
ili tuweze kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali katika azma hiyo ya
kuifanya Tanzania nchi yenye uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025"
alisisitiza Rioux.
Uhusiano wa Tanzania na
Ufaransa ulianza tangu miaka ya 1960 na ukaimarishwa zaidi mwaka 1979,
ambapo kwa mara ya kwanza, Serikali ya nchi hiyo iliipatia Tanzania mkopo wa
kiasi cha fedha za Ufaransa, faranga milioni 361, kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (Julius Nyerere).
Comments
Post a Comment