Featured Post

MTANZANIA AIPATIA DENMARK USHINDI WA 1-0 KOMBE LA DUNIA HUKU NIGERIA IKINYUKWA 2-0 NA CROATIA


Yiusuf Poulsen akishangilia bao lake dhidi ya Peru.

YUFFUS POULSEN, mshambuliaji wa Denmark ambaye babake ni Mtanzania, amekuwa Mtanzania wa kwanza wa asili kushiriki fainali za Kombe la Dunia na leo hii amefanikiwa kuipatia Denmark ushindi muhimu.
·         Soma zaidi kumhusu Yiusuf Poulsen hapa: Mchezaji wa asili ya Tanzania kucheza Kombe la Dunia

Bao la dakika ya 59 alilofunga Poulsen lilitosha kuipa Denmark ushindi wa 1-0 dhidi ya Peru katika mchezo wa Kundi C.
Licha ya kupoteza mechi na fursa ya kuongoza kupitia penalti, kikosi cha Peru kiliweka historia kwa kuliwakilisha taifa hilo kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia tangu mwaka 1982.
Christian Cueva alipoteza mkwaju wake wa penalti dakika chache kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika. Shuti lake lilipaa angani.
Kocha wa Denmark, Age Hareide amemtaja kipa wake, Kasper Schmeichel na mabeki kwa kuchangia ushindi huo.
Vikosi vyao vilikuwa:
Peru: Gallese (Veracruz); Advincula (Tigres), Rodriguez (Atletico Junior)/Ruidiaz (Morella, 85), Ramos (Tiburones Rojos de Veracruz), Trauco (Flamengo), Tapia (Feyenoord)/Aquino (Leon, 87), Yotun (Orlando City), Carrillo (Benfica), Cueva (Sao Paulo), Flores (Aalborg)/Guerrero (Flamengo, 62), Farfan (Lokomotiv Moscow).
Kadi ya njano: Tapia.
Denmark: Schmeichel (Leicester); Dalsgaard (Brentford), Kjaer (Sevilla), Christensen (Chelsea)/Mathias Zanka Jorgensen (Feyenoord, 81), Larsen (Udinese), Kvist (Copenhagen)/Schone (Ajax, 36), Eriksen (Tottenham), Delaney (Werder Bremen), Poulsen (RB Leipzig), N Jorgensen (Feyenoord), Sisto (Celta Vigo)/Braithwaite (Middlesbrough, 67).
Kadi za njano: Delaney, Poulsen.
Mwamuzi alikuwa Bakary Gassama (Gambia).
Lakini leo imekuwa siku nyingine ya masikitiko kwa Afrika baada ya mwakilishi mwingine Nigeria kulazwa 2-0 na Croatia katika mechi ya Kundi D.
Misri na Morocco Ijumaa walikuwa wamechapwa 1-0 na Uruguay na Iran.
Matumaini sasa ni kwa Tunisia watakaokutana na England Jumatatu saa tatu usiku na Senegal watakaokutana na Poland Jumanne saa kumi na mbili jioni.
Misri watakuwa tena uwanjani saa tatu usiku siku hiyo dhidi ya wenyeji Urusi.
Siku ilianza kwa mechi za Kundi C katika ya Ufaransa na Australia. Pande zote zilikabidhiwa penalti baada ya refa kushauriana na waamuzi wenzake upande wa teknolojia wa VAR.
Pande zote zilifunga penalti zao, lakini mwishowe Ufaransa iliilaza Australia 2-1 baada ya bao la Paul Pogba kuvuka mstari.
Aidha, kwa mara ya kwanza katika kombe la dunia mwaka huu, Penalti tano zilitolewa huku mbili kati yao zikipotezwa na wachezaji katika muda wa kawaida wa mchezo.
Katika uwanja wa Spartak mjini Moscow, taifa ndogo la Iceland liliwashangaza wengi baada ya kujitetea dhidi ya Ajentina.
Lionel Messi alinyimwa bao la penalti na kipa wa Iceland Hannes Halldórsson ambaye aliishia kutuzwa mchezaji bora wa mechi. Refa kutoka Poland Szymon Marciniak aliipa Argentina penalti dakika ya 63 baada ya Maximiliano Meza kulazwa na Rurik Gislason.
Ingawa Aguero ailiiweka Argentina kifua mbele dakika ya 19, bao lake lilifutwa na Alfred Finnbogason dakika chache baadaye.
Siku iliisha na mechi ya Kundi D kati ya Croatia na Nigeria. Makosa ya mabeki yalipelekea Nigeria kulazwa 2-0 na kuninginia mkiani.
Timu hiyo imesalia na kibarua kigumu kwani ndio timu pekee bila alama katika kundi hilo.


Comments