- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ameliomba radhi
Bunge kwa kitendo cha maofisa wake kuingia ndani ya mgahawa wa kisha kupima
samaki waliopikwa kwa ajili ya wabunge bila kuzingatia taratibu na kanuni za
afya.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya maofisa hao kuingia
kwenye mgahawa wa Bunge bila utaratibu na kupima samaki waliopikwa, hali ambayo
ilizua kizaazaa na ksuababisha wabunge kulijadili kwa nusu saa.
Hatua hiyo imetokana na Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson,
kuiagiza serikali kutoa kauli bungeni kabla ya kuchukua uamuzi kama jambo hilo
lipelekwe kwenye Kamati ya Kinga, Hadhi na Madaraka ya Bunge ama la.
Akitoa kauli hiyo ya radhi jana, Mpina alisema, Juni 19,
2018 alipokuwa kwenye mgahawa huo alibaini uwepo wa samaki aina ya Sato
wanaouzwa wasiokidhi viwango vya kisheria.
Alisema baada ya kuona hivyo alimuagiza Katibu wake kwenda
kujiridhisha kama ni kweli ama la ambapo baada ya kufanya hivyo waligundua kuwa
samaki hao walikuwa na urefu wa chini ya sentimeta 25.
"Nikamuagiza katibu wangu katika uhakiki unaoendelea
wakaguzi wajiridhishe katika mgahawa wa Bunge ambapo walibaini baadhi ya samaki
ni wachanga waliokuwa na urefu chini ya sentimeta 25.
"Baada ya kukiri kosa mmiliki wa mgahawa huo alitozwa
faini ya Shs. 300,000 na samaki hao wasioruhusiwa waliondolewa kwenye mgahawa
huo," alisema Mpina.
Mpina alikiri kuwa, watumishi hao katika kutekeleza wajibu
huo waliingia eneo la Bunge bila kibali cha kuwawezesha kufanya kazi hiyo na
kupima chakula kilichopikwa.
"Kwa sababu hiyo, wizara inaliomba radhi Bunge lako
tukufu na ninasisitiza kuwa wizara yangu haikuwa na lengo lolote la dharau kwa
Bunge lako tukufu na Ofisi ya Spika.
"Pia naliomba Bunge lako tukufu liendelee kuunga mkono
jitihada za wizara yangu katika kuendelea kulinda rasilimali za nchi,"
alieleza.
Baada ya kuomba radhi, Spika Job Ndugai, alisema licha ya
maelezo mazuri ya waziri, alimueleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa namna ambavyo
Bunge lilisikitishwa na kitendo hicho.
Alisema, endapo mabunge mengine yakisikia waziri amefanya
kitendo hicho ni dharau ya hali ya juu.
"Hata panapokuwa na kosa la jinai linafanyika katika
eneo la Bunge, RPC anapaswa kunifahamisha na sisi si kazi yetu kulinda jinai,
sisi hatulindi wahalifu, lakini lazima tutaarifiane,” alisema.
Spika aliongeza: "Mtu anaponunua samaki kilo 100, kwa
akili ya kawaida watu wananunua samaki kwa kilo si kwa futi. Halafu samaki
mwenyewe ameshakuwa kitoweo. Sasa hii sheria ya kupima vitoweo itabidi tuzisome
vizuri.
"Hivi tunataka watu wafunge milango ndiyo wale samaki? Yani
samaki mbichi aliyevuliwa atafika Dodoma kwa muda gani, afanyiwe process
(matayarisho) bado urefu wake huo huo wakati ameshapikwa?
"Halafu wapimaji wenyewe wanapima mikono haina hata
groves (mipira ya kuvaa mikononi), wanashikashika samaki na wamealika waandishi
wa habari, wamejaa zaidi ya 20 kwenye chumba kimoja na baada ya pale wamerusha
kwenye mitandao kama kuliweka Bunge mahali pasipostahili.
"Kwa kawaida ukikasirishwa sana na jambo lazima usamehe
kwa hiyo naomba waheshimiwa wabunge, tusamehe," alihitimisha.
Comments
Post a Comment