Featured Post

BITEKO AELEKEZA TUME YA MADINI KUPELEKA TIMU YA WAKAGUZI WA MADINI WILAYANI ULANGA



Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko akiongea na wananchi wa kijiji cha Ipanko juu ya changamoto ambazo wanakabiliwa nazo na kuunda timu maalum ya wataalam kwa ajili ya kuchunguza migodi yote na aina ya madini yanayopatika katika migodi iliyopo halmashauri ya wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania haiendelei kuibiwa na wawekezaji katika seckta ya madini. 

Baadhi ya wananchi wakimsikiliza kwa umakini Naibu waziri wa madini mheshimiwa Doto Bitoke alifanya ziara ya kutatua mgogoro baina ya wawekezaji na wananchi kwenye sekta ya madini
NA FREDY MGUNDA,MOROGORO.

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amesema kuwa ataunda timu maalum ya wataalam kwa ajili ya kuchunguza migodi yote nchini ikiwa ni pamoja na utambuzi wa aina ya madini yanayopatika katika migodi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania haiendelei kuibiwa na wawekezaji katika sekta ya madini.

Akizungumza wakati wa ziara ya siku mbili Mkoani Morogoro Mh Biteko alisema kuwa madini yote yaliyopo katika ardhi ya Tanzania ni mali ya watanzania hivyo yanapaswa kuwanufaisha watanzania kwanza ndipo watu wengine wafuate.

“Naombeni watanzania wote mjue kuwa madini haya ni mali ya watanzania wote hivyo tunapaswa kuyalinda na kutoa taarifa sahihi kwa serikali kama kuna mtu anaiibia serikali kwa namna moja au nyingine ili serikali iweze kuchukua hatua za kisheria dhidi yake, Na mimi nawaambieni watanzania tuache uoga tuseme ukweli kama Rais wetu Mhe Dkt John Pombe Magufuli anavyosisitiza utendaji wa uwazi na uwajibikaji katika serikali” Alikaririwa Mhe Biteko

Biteko amepiga marufuku wawekezaji kutumia fedha zao kuwanyanyasa wananchi waliopo kwenye maeneo ambayo kuna migodi kwa ajili ya kuwaibia watanzania ambao bado wana kipato cha chini katika maeneo yanapopatikana madini.
“Najua hawa wawekezaji wanapesa nyingi sana hivyo isiwe sababu ya kuwarubuni baadhi ya wananchi na kuwatesa wananchi wengi hususani waliopo kwenye maeneo ya madini na leo nataka niwaambie ukweli wawekezaji wote nchini najua ambavyo mnatumia pesa zenu kuwanyanyasa wananchi, sasa ndio mwisho wenu maana serikali ya awamu ya tano inataka haki kwa kila mwananchi” Alisisitiza Biteko

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Bitoke alifanya ziara ya kikazi katika kijiji cha Ipanko kilichopo katika wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na kugundua kuwa kuna wawekezaji wanaidanganya serikali na wananchi kwa kutoweka wazi kiasi gani ambacho wanakipata kwenye migodi iliyopo katika kijiji hicho.

“Jamani wana Ipanko nchi hii tumeibiwa sana sasa ifike mwisho tusema hapana haiwezekani tena kwenye serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli tuendelee kuibiwa madini yetu na kuwanufaisha watanzania ambao wapo nje ya nchi yetu, Rais kashasema na sisi wasaidizi wake tunaungana naye kwamba iwe mwisho kuchezewa kwa rasilimali zetu”

“Chonde chonde nyie viongozi wetu wa ngazi za vijiji, kata, tarafa, wilaya na mkoa tunaomba msituangushe kwa kupokea rushwa kutoka kwa wawekezaji na kuisaliti nchi yako kuendelea kuibia kirahisi namna hii” alisema Biteko

Biteko alieleza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli inawapenda sana kuwa na wawekezaji wengi wenye tija ambao sio wababaisha na ambao wamekuja nchi kuiba rasilimali za watanzania.

Aidha, Biteko alisema kuwa haiwekani muwekezaji akawekeza Bilioni 42 halafu akachangia madawati na mifuko ya saruji katika jamii kama ndio mchango wake, haiwezekani wanapaswa kuchangia kulingana na kiasi ambacho wamewekaza kwa faida na manufaa ya wananchi.

“Mimi binafsi hainiingi akilini kuona muwekezaji amewekeza pesa nyingi kama hizo halafu kwenye shughuli za kimendeleo amechangia kiasi kidogo namna hiyo kwangu nasema haiwezekani na nchi hii kwa sasa sio yakuchezewa tena” alisema Biteko

Lakini pia Naibu waziri huyo alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mhe Goodluck Mlinga kwa kuwapigania wananchi wake kwa kuzifikisha kero mahali husika na kutafutiwa ufumbuzi.

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Pangarasi Kanyali, Cyprian Kanyali, Micky Sengo, Doedatus Moholeli, Hilda Linoma na Fredrick Kazimoto walimpongeza Naibu Waziri wa Madini Mhe Biteko kwa kufika kijiji hapo na kusiliza kero zao kwani wana amini zitatafutiwa ufumbuzi kwa kufuata sheria na katiba ya nchi.

“Toka sisi tuzaliwe hatujawahi kutembelewa na waziri na kusikiliza kero zetu kama ambavyo wewe umefika kijijini kwetu leo hii tunajisikia wenye amani na furaha kwa kuwa tunajua kero zetu tunazifikisha moja kwa moja kwa kwa Rais wetu kupitia wewe waziri” Walisema wananchi hao

Awali Mbunge wa Jimbo la Ulanga Goodluck Mlinga alisema kuwa lengo la waziri kufika katika kijiji hapo ni kujionea kero wanazokumbana nazo wananchi kupitia wawekezaji wa sekta ya madini na kuzitafutia ufumbuzi.

“Huku ni mbali sana Mheshimiwa Naibu Waziri lakini kuna madini mengi ambayo ndio utajiri wa nchi hii hivyo tunapaswa kuwa makini na hawa wawekezaji maana wamekuwa wakiibia sana serikali yetu” Alisema Mlinga

Comments