- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NEW YORK, MAREKANI
MHUBIRI mmoja wa Kiinjilisti nchini Marekani amewaomba
waumini wake kuchanga pesa za kumsaidia kununua ndege yake ya nne.
Amesema hata kama Yesu angekuwepo siku hizi, "asingekuwa
anapanda punda".
Jesse Duplantis amesema Mungu amemwambia anunue ndege aina
ya Falcoln 7X ambayo inagharimu Dola za Marekani milioni 54 (takriban shilingi
bilioni 124.2).
Ameongeza kwamba alikuwa na shaka pia kuhusu kuendelea na
ununuzi huo mwanzoni, lakini Mungu alimwambia: "Sikukwambia uilipie.
Nilikwambia uamini na utaipata."
Ingawa si jambo la ajabu kwa wahubiri kumiliki ndege zao
binafsi, ombi lake kwa waumini kuchangia limezua shutuma.
Watu kwenye Twitter wamepokea ombi hilo kwa mshangao, wengi
wakinukuu aya kwenye Biblia zinazotahadharisha dhidi ya ulafi na "manabii
wa uongo".
Wengine wanasema pesa hizo zingetumika vyema kuwasaidia
maskini.
Kwenye ujumbe wa video ambayo imepakiwa kwenye mtandao wake,
Duplantis mwenye umri wa miaka 68 alisema: "Mwajua, nimemiliki ndege tatu
maishani mwangu, na nimezitumia na kuchoma mafuta kwa ajili ya Bwana Yesu
Kristo.
"Sasa, baadhi ya watu wanaamini kwamba wahubiri hawafai
kuwa na ndege. Ninaamini kwamba wahubiri wanafaa kwenda kwenye kila redio (au
kipaza sauti), kwenye kila chombo (cha habari), kuwezesha Injili kuenezwa kote
duniani."
Huku akiwa amesimama karibu na picha za ndege zake
anazozimiliki sasa, mhubiri huyo alisema ndege aliyoinunua miaka 12 iliyopita
kwa sasa haitoshi kwa utumishi na matumizi ya kanisa lake.
Alisema ni kwa sababu ndege hiyo haiwezi kusafiri mbali bila
kutua, hiyo ikiwa na maana kwamba hulazimika kulipa pesa nyingi kutua ili
kuiongeza mafuta.
Picha nyingine iliyooneshwa kwenye video hiyo ilimuonyesha
mhubiri huyo akiwa amesimama na ndege hizo tatu, na juu ya picha hiyo maelezo:
"Si kuhusu vitu unavyomiliki, bali vitu unavyovipa kipaumbele."
Duplantis ametetea ombi lake la kutaka kununuliwa ndege
akisema Yesu aliwaambia wafuasi wake "nendeni kote duniani na mkahubiri
Injili kwa kila kiumbe, sasa tutawezaje kutimiza hilo? Siwezi kuishi muda mrefu
wa kutosha kusafiri kote kwa kutumia gari au meli au treni, lakini ninaweza
kusafiri mbali kwa kutumia ndege."
Mwaka 2015, Duplantis alitokea kwenye video na mhubiri
mwingine Kenneth Copeland, ambapo Copeland alieleza kusafiri kwenye ndege za
kibiashara, pamoja na watu wengine wa kawaida, kama kusafiri "katika mkebe
mkubwa uliojaa mashetani."
Comments
Post a Comment