Je, wajua kuwa katika ndoa za mitala upo uwezekano mume kuishi na wake zake hata watatu katika Nyumba moja?
Katika
maeneo mengi ya Pwani ya Afrika Mashariki, ndoa hizo zimeshamiri. Sababu kuu ikiwa suala la dini na utamaduni wa maeneo ya Pwani, huku
katika maeneo mengine likibaki kuwa mjadala mkali hasa kwa wanawake. Katika Kisiwa cha Mafia, Mkoa wa Pwani nchini Tanzania, ndoa za mitala zimejaa
karibu kila nyumba, jambo ambalo husababisha wake wenza kukaa nyumba
moja. Kutokana na hali hii kuwa ya kawaida katika kisiwa hiki cha
Mafia, niliweza kuzungumza na watu kadhaa, ambao wana wake zaidi ya
mmoja. Mmoja wao aliyenivuta zaidi ni Bwana Ally Khasim, ana wake
wawili ambao wanaishi katika nyumba moja lakini vyumba tofauti, na
hawajawahi kuwa na mgogoro wowote kati yao, jambo ambalo si mara nyingi kutokea. Mke mkubwa anaitwa Khadija, na wa pili anaitwa Nuru. Khadija anasema kuwa hakukubaliana na uamuzi wa mume wake wa kuongeza
mke wa pili lakini baada ya kumshawishi akaona ni jambo la kawaida, na
kwa upande wa Nuru mke wa pili alikubali kuingia katika ndoa ya wake
wengi kwa hiari yake. Ndoa hiyo ya Bwana Khasim na wake zake imedumu kwa miaka 14 bila migogoro na ugomvi baina ya wake zake, jambo ambalo ni nadra. "Hawajawahi kugombana kwa lolote lile labda mikwaruzano ya
kawaida baina yangu mimi na mmoja kati yao, ambapo ni jambo la kawaida
baina ya mume na mke,'' anasema Khasim. Nilipomuuliza Nuru, mke
mdogo kuwa alitarajia kukutana na mikasa ya uke wenza, alinambia kuwa
mwanzoni alidhani angekutana nayo lakini akakuta hali ni tofauti. ''Mwanzoni
nilitarajia kuwa nitakutana na visa, lakini nashukuru sana baada ya
kukaa na mke mwenzangu kwa muda hatujawahi kugombana tunafanya kila kitu
kwa ushirikiano,'' anasema Nuru. Naye mke mkubwa, Bi Khadija anasema kuwa yeye hana matatizo
yoyote na alipokuja mke mdogo na yeye hakuwa na matatizo hivyo wamekuwa
wakiishi kwa amani na upendo katika ndoa yao. Nilimuuliza pia Bwana Khasim kama anatarajia kuongeza mke wa tatu, akanambia akiwa sawa
kiuchumi basi ataongeza, na wake zake wanakubali kumkaribisha kukaa naye
kama huyo mke wa tatu atakua mpole na mtulivu kama wao. Kwa Bwana
Khasim, wake zake na watu wengine wa Pwani suala la ndoa za mitala si
ajabu, ni sehemu ya maisha yao, lakini mbali na dini niliambiwa pia
suala la chakula lina mchango mkubwa wao kuoa wake wengi kutokana na
kula samaki wa aina mbalimbali ambao wao wanaamini inawaongezea nguvu za
kiume. ''Mimi
nakubali kabisa sisi tunapenda kuoa wake wengi, mimi nina wake wawili
na ukiachana na dini sisi watu wa pwani bwana, tunakula vyakula vya
kuleta nguvu mke mmoja pekee hatoshi, kwani ana mambo mengi, anaweza
akajifungua akaa miezi mitatu minne, sasa sisi uvumilivu huo hatuna ndio
mana tunaoa wanawake hata watatu na tunataka utulivu pia,'' anasema
Khamis Saburi mkazi wa kisiwa cha Jobondo, Mafia. Mbali na mitazamo hiyo wapo wachache ambao hawana mpango wa kuongeza mke, kama Bwana Ally Njenge, ''Kama
huwezi kuridhika na mke mmoja basi ni hulka yako tu, mimi nina mke mmoja
na siwezi kuongeza mwingine, kwanza ni kujiongezea gharama lakini pia
matatizo tu kwanini usiridhike na huyo mmoja?"
Katika maeneo mengine ya bara, bado suala hilo lina mjadala mkali, huku wanawake hawataki kusikia kabisa kuolewa uke wenza.
Comments
Post a Comment