- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA
EMMANUEL J. SHILATU
KANALI
mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Abdulrahman Omar Kinana, anatajwa
kuwa katika orodha ya safu za viongozi mibuyu na migude kwenye misitu minene ya
siasa yenye kuhimili tufani za kila aina.
Si hivyo
tu, pia anatajwa kuwa mwanasiasa anayependa kuheshimu utamaduni, utaratibu na
mwenye kuishi kwa misingi ya nidhamu .
Kinana
anatajwa kama zao miongoni mwa kunga zitokanazo na mazao katika medani za
siasa, utawala, uongozi na aliyeshiba ujuzi toshelezi wa masuala ya diplomasia
ya siasa pia anayejua uhusiano utokanao na historia, harakati za ukombozi na
Umoja wa Afrika.
Sauti yake
aghalabu huwa na mvumo wa mawimbi ya busara, fikara njema na hekima zenye wito pele aamuapo kusema,
kukosoa, kutetea, kukumbusha, kushauri au kuonya kutokana na tabia yake ya
kufanya yote hayo kwa hali ya kujiamini akiwa na nguvu ya hoja.
Ukimya wa mwanasiasa
huyo siku zote ni kama mfano wa simba hodari awindaye nyikani au mbugani akiwa
hana pupa wala kiherehere. Huyafanya yote kwa utulivu na umakini mkubwa ambao
baadaye haumletei majuto, athari wala taathira.
Ni mwanasiasa
wa aina yake aliyewahi kuhitajiwa na marais (wenyeviti) watatu awe katibu mkuu
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akakataa, huku akitoa madai mazito yenye msingi,
nguvu ya hoja na maana.
Amewahi
kutakiwa na Rais Ali Hassan Mwinyi awe Katibu Mkuu wa CCM akakataa huku akitoa hoja. Akasema alikuwa na mchakato wa kazi nyeti na
muhimu akishirikiana na wenzake kufanya
mabadiliko ya mfumo mpya wa Jeshi utakaokwenda sanjari na mahitaji ya wakati;
hivyo asingekuwa tayari kuiacha kabla kazi hiyo kukamilika.
Akatakiwa
tena na Rais Benjamin Mkapa ashike nafasi hiyo akasita kukubali huku akitoa
hoja za msingi na zenye mashiko yasiyo na shaka wala utata.
Kinana
mara ya kwanza alitakiwa na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete, akakataa
kubeba jukumu hilo kwa sababu kadhaa alizoona ni ngumu kwake kukitumikia chama
kwa wakati huo. Hata hivyo, mbinu za ushawishi zikafanyika akaafiki kuwa Katibu
Mkuu.
Bila shaka
Kinana aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wakati CCM ikiwa katika mgawanyiko mkubwa
uliohatarisha uhai na mustakabali wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010.
Kwa busara
zake, pengine na ziada ya maarifa au mbinu za kijeshi, uzoefu wa kisiasa,
uongozi na utawala, Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake ghafla wakashikamana
tena na kuzika yaliopita.
Amewahi
kusema mbele ya Mzee Mkapa kwa wakati ule amejiona mbele yake bado ipo hazina
ya viongozi wajuzi wa muda mrefu ndani ya chama, vingunge wenye weledi na
maarifa ya kisiasa kuliko yake, hivyo muda wa yeye kushika wadhifa si wakati
huo.
Akaachwa
na kuendelea kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM akiwa Meneja wa kampeni za
wagombea urais Mzee Mkapa na Dkt. Jakaya Kikwete.
Katika
safu ya Vijana wa TANU (TANU Youth League - TYL) na baadaye UVCCM waliolelewa
kwenye mikono ya wanasiasa kama akina Mwalimu Julius Nyerere, Sheikh Aboud
Jumbe Mwinyi, Sheikh Thabit Kombo Jecha, Mzee Rashid Kawawa, Mzee Saadan Abdul
Kandoro na Mzee Rajab Diwani, Kinana anaweza kusimama kati yao.
Ameshiriki
pamoja nao katika mbio za siasa, akichuma uzoefu huku mbele yake kukiwa na wanasiasa
kama Mzee Pius Msekwa, marehemu Kingunge Ngombare Mwiru, Mzee John Malecela,
Hayati Daudi Mwakawago, Hayati Moses Nnuye, Balozi Christopher Liundi, Ali
Ameir Mohamed na wengine kadhaa.
Vijana
wanasiasia wa hirimu yake na wanaopishana kwa umri kiasi kidogo ni akina Dkt.
Kikwete , Dkt. Mohamed Seif Khatib, Dkt. Salmin Amour Juma, Yusuf Makamba, Jaka
Mwambi, John Chiligati, marehenu Ukiwaona
Ditope Mzuzuri na wengine wengi.
Kanali mstaafu
Kinana kama atajigamba amezaliwa na kulelewa ndani ya TANU/ASP na maisha yake
yote amekulia CCM na serikali zake, hoja hiyo itajuzu na kuyakinika.
Kwa ufupi
ni mwanasiasa asiyebahatisha katika utambuzi wa mizungu ya siasa, mbinu za
utendaji, uelewa na upimaji kwenye viwango vya usemaji, ushauri au anapofanya
shambulizi la kisiasa dhidi ya hasimu wake.
Niliposikia
tetesi za kujiuzulu kwake kwa siku nzima ya juzi nilikuwa nikitafakari bila
kupata majibu ya haraka na kuona haikuwa wakati sahihi na muafaka sana kwa
kiongozi huyo wa CCM kuachia ngazi na kujiweka kando.
Hata hivyo,
CCM ni chama kikongwe chenye hazina kubwa ya wanasiasa hodari, hivyo lolote
linaweza kuwa ila muhimu ni kutega mingo na kusubiri wakati kwa kutega vyema
masikio yetu juu ya nani atakayeshika wadhifa wa Katibu Mkuu.
Comments
Post a Comment