- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
WAKAZI Jiji la Dar es Salaam wako hatarini
kuugua magonjwa ya akili kutokana na kukosa usingizi na msongo wa mawazo.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, pilika nyingi
za wakazi wa jiji hilo zinazowafanya wakose usingizi, pamoja na kuzidiwa na
majukumu ya kazi na ugumu wa maisha ni mambo yanayosababisha msongo wa mawazo
ambao hatimaye huleteleza magonjwa ya akili.
Wanajamii walioko hatarini kupata magonjwa
mbalimbali kutokana na kukosa usingizi ni wanafunzi ambao wanatumia muda mwingi
kujisomea hasa nyakati za usiku, wafanyakazi wa vyombo vya usafiri hasa
madaladala, watu wanaolinda nyakati za usiku kwa siku kadhaa mfululizo bila
kupokelewa pamoja na watumishi wa sekta ya afya, hususan madaktari na wauguzi.
“Tunakoelekea ni kubaya sana, siyo ajabu
machizi wakaongezeka jijini Dar es Salaam kuliko mahali pengine nchini Tanzania
na uchizi siyo lazima uokote makopo, kauli yako tu inaweza kukuonyesha kwamba
wewe hauko sawa,” anaeleza Dkt. Noel Peter, mtaalam wa mambo ya saikolojia.
Dkt. Noel anasema, msongo wa mawazo
unaosababishwa na ugumu wa maisha pamoja na kukosa usingizi, matatizo ambayo yanawakabili
wakazi wengi wa jijini humo.
Tafiti kadhaa zinaonyesha kwamba, watu
wanaolala kwa muda wa kati ya saa 6.5 hadi 7.5 kwa usiku mmoja wanaweza kuishi
muda mrefu na kwamba wanaolala kwa muda wa saa 8 au zaidi, au wanaopata
usingizi kwa chini ya saa 6.5, wanaishi muda mfupi.
Wataalam wamekuwa wakishauri kulala kwa
walau saa 8 ili kujenga afya, jambo ambalo linaepusha matatizo mengi ya kiafya.
Kukosa usingizi (Sleep deprivation)
ni hali ya kukosa usingizi kwa kiwango kinachotakiwa ambapo wakati mwingine
husababishwa na matatizo binafsi ya ukosefu wa usingizi (sleep disorders).
“Kondakta au dereva wa daladala anaamsha
gari alfajiri, halafu anachelewa kulala, akija barabarani ndani ya gari
anakutana na abiria wengine ambao nao wanakuwa na matatizo yao, hivyo utakuta
wanapishana kauli mara kwa mara," anasema Dkt. Noel.
Tanzanite imeshuhudia mara kadhaa abiria
wakigombana na hata kupigana na makondakta kutokana na ugomvi kwenye daladala.
Mapema mwezi Machi 2018, kondakta wa
daladala aina ya Nissan Civillian lenye namba za usajili T 247 DDT linalofanya
safari zake kati ya Temeke, Dar es Salaam na Vikindu, Pwani, Abdallah Kikoto
(36), anadaiwa kunyongwa na abiria wake hadi kufa kwa kile kilichoelezwa "kutofautiana
wakati abiria akidai chenji".
Inaelezwa
kwamba, abiria huyo alimkwida shati kondakta kwa umbali mrefu huku akitaka
arejeshewe chenji yake, ambapo juhudi za abiria wengine kuamulia zilishindwa
kuzaa matunda, hali iliyomlazimu dereva kulipeleka gari Kituo cha Polisi
Tandika.
Taarifa
zilibainisha kwamba, Polisi pia walilazimika kutumia nguvu kumnasua kondakta
huyo mikononi mwa abiria, na alipokimbizwa hospitali tayari alikuwa amekata
roho.
Dkt. Noel anasema, kutopata usingizi wa
kutosha kuna madhara makubwa kiafya na kunaweza kumfanya mtu yeyote kubadilika
kitabia hata ndani ya familia.
“Anaweza kuwa mkali bila sababu za msingi,
anaweza kutoa lugha chafu bila kutegemea ingawa baadaye anaweza kujutia na
matatizo mengine ya kiafya, hasa kiakili, tena basi kukosa usingizi kunafupisha
umri wa kuishi,” anasema.
Hamad Selemani ni kondakta wa daladala
linalofanya safari zake Mbagala-Kawe jijini Dar es Salaam ambaye anakiri huwa
hapati usingi wa kutosha na ambapo hulala kwa muda wa saa 2 au 3 tu kabla ya
kuamka tena.
“Ninawajibika kuamsha gari saa 9:30 alfajiri,
nakuja nalo kituoni ambako dereva ananifuata na kunikuta, tunafanya kazi mchana
kutwa, kama kupumzika basi ni wakati wa chakula cha mchana.
“Ili tutimize hesabu ya tajiri na sisi
tupate posho lazima tufanye kazi kwa bidii, lakini wakati mwingine foleni
zinakwamisha malengo yetu, hivyo tunalazimika kufanya kazi hadi saa 4 au saa 5
usiku.
“Tukitoka hapo inabidi tupeleke hesabu ya
tajiri, tukaegeshe gari kwenye kituo cha mafuta au popote pale, halafu
tuangalie ustaarabu wa kurejea makwetu. Nafika nyumbani saa 6:30 au 7, lakini
mpaka nioge, nile na usingizi unipitie itakuwa saa 8 tayari, naweka alarm kwenye simu yangu iniamshe saa
9:30, maana yake nitalala kwa saa 1:30 tu. Kweli, wakati mwingine tunatoa kauli
mbovu kwa abiria siyo kwa kupenda, unajikuta tu umeropoka,” anafafanua.
Hamad anaeleza kwamba, takriban mara mbili
amejikuta akifikishwa polisi kutokana na kauli hizo, ambazo huzijutia baada ya
kuzitoa.
“Mara ya kwanza nilikuwa naendesha gari
mwenyewe, kwa sababu pia ni dereva, wakati niko pale Buguruni Shell ninataka
kutoka, gari moja ndogo ikaja, sikuiona, nikaibana ubavuni. Lilikuwa ni suala
la kuzungumza kistaarabu, lakini nikajikuta nikimjibu yule jamaa kwa dharau,
akanipeleka polisi na kwa kuwa kosa lilikuwa langu, nikalipa,” anasema.
Mara ya pili, anasema, alimtolea lugha ya
kashfa mwalimu mmoja ambaye alionyesha kitambulisho katika utaratibu wa
kusafiri bure, badala yake yeye akaanza kumtukana na kumwita ‘mzigo, mpenda
dezo’ na maneno mengineyo ya dharau, hivyo akapelekwa polisi ambako alishinda
tangu asubuhi hadi saa 4 usiku.
Maelezo ya Dkt. Peter hayana tofauti na
utafiti uliofanywa na Daniel Kripke na wenzake katika Kituo cha Scripps Clinic
Sleep Center mjini La Jolla, California nchini Marekani mwaka 2002, ambaye
anasema zaidi ya vifo milioni moja vya watu wazima vilivyotokea nchini
Marekani, vilisababishwa na kukosa usingizi.
Dkt. Peter anasema kwamba, kukosa usingizi
kunaweza kusababisha matatizo ya kimaumbile, kisaikolojia na kadhalika.
“Ukosefu wa usingizi kwa ujumla unaweza
kusababisha maumivu ya misuli, uoni hafifu, msongo wa mawazo, upofu usio rasmi
(colour blindness), kusinzia mchana,
uwezo mdogo wa kufikiri na kutafakari na hata kutojitambua,” anasema Dk. Peter.
Aidha, anasema hali hiyo husababisha pia
kudhoofisha kwa kinga ya mwili, kuzimia, kuchanganyikiwa, kuona mauzauza,
kuvimba mikono, kuumwa kichwa, hyperactivity,
hypertension, kutokutulia, kuwashwa,
kuota ndoto za kutisha kama za majinamizi, kupoteza kumbukumbu, kichefuchefu,
kushindwa kutoa uamuzi kwa haraka, kutoa kauli mbovu, kuvimba koo, kupungua ama
kuongezeka uzito kusiko kwa kawaida, na kuongezeka kwa hamu ya kufanya tendo la
ndoa.
Katika nchi nyingi duniani, kukosa usingizi
miongoni mwa wanafunzi ni matatizo ya kawaida ingawa kitaalam wanapaswa kulala
kati ya saa 8.5 hadi 9.25.
“Watumishi wa sekta ya afya nao wako
hatarini kupata matatizo ya akili, hasa msongo wa mawazo,” anasema Dkt. Luhaja
Nginila.
Dkt. Nginila anasema, watumishi wengi
katika sekta ya afya hasa madaktari na wauguzi, ambao kutokana na uhaba wa
wafanyakazi, wengi wanatumia muda mwingi wakiwa kazini kwa siku kadhaa na hata
nyakati za usiku wanalazimika kuwa macho ili kuwahudumia wagonjwa – waliolazwa
ama wanaokuja nyakati hizo.
“Unaweza kukuta daktari au muuguzi anakaa
wodini kwa saa 72 bila kupokelewa, maana yake hata wakati wa usiku mtumishi
huyu inabidi ‘aufukuze usingizi’ ili awahudumie wagonjwa, hali ambayo inamfanya
hata tabia yake ibadilike.
“Anaweza kuwa na msongo wa mawazo, mkali
bila sababu za msingi, anaweza kufanya makosa ambayo katika hali ya kawaida
angeweza kuyaepuka, yote ni kwamba kichwa chake hakiko sawa,” anasema Dkt. Nginila.
Kwa mujibu wa Dkt. Nginila, hali hiyo ndiyo
wakati mwingine huwafanya baadhi ya watumishi, hasa wauguzi, wanakuwa na kauli
mbovu na za kuudhi kwa wagonjwa kutokana na kukumbwa na msongo wa mawazo na
fadhaa kwa kukosa usingizi muda mrefu.
“Kukosa usingizi ni tatizo sugu ambalo
linasababisha hata kubadilika kwa tabia, kupunguza utashi hata katika shughuli
za kawaida na kunaondoa ile hali ya kufurahia jambo lolote, unaweza kuwa mkali,
hasira za mara kwa mara, unachukia bila sababu na unaweza kujichukia hata wewe
mwenyewe,” anasema.
Utafiti wa mwaka 1996 wa Chuo Kikuu cha
Tiba cha Chicago unaonyesha kwamba, ukosefu wa usingizi unaathiri kwa kiasi
kikubwa mwili wa binadamu kwa kushinda kumeng’enya sukari hasa glucose, hali
ambayo inaweza kusababisha hatua za awali za Saratani Type 2.
Utafiti uliofanywa mwaka 2000 na UCSD School of
Medicine na Veterans Affairs Healthcare System jijini San Diego
ulibaini kwamba kukosa usingizi kunaweza kusababisha madhara makubwa kwenye
ubongo, ambao unaweza kushindwa kufanya kazi vizuri.
Aidha, utafiti uliofanywa na Taasisi ya
Tiba ya Chicago mwaka 2001 ulionyesha kwamba, kukosa usingizi kunasababisha
madhara makubwa kiafya, yakiwemo magonjwa ya moyo na uchizi.
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 1999
unaonyesha kwamba, kukosa usingizi kunachangia kuzidiwa nguvu kwa muhimili
mfumo wa tezi mbalimbali maarufu kama Hypothalamic-pituitary-adrenal
axis (ambao ndio unaodhibiti hali kama fadhaa, msongo wa mawazo na
kudhibiti shughuli za mwili kama mmeng’enyo wa chakula, mfumo wa kinga, hali ya
fikra, masuala ya ngono, au matumizi ya nishati mwilini) na wakati huo
unapunguza homoni za ukuaji na kusababisha udumavu.
Kwa mujibu wa utafiti
uliochapishwa mwaka 2000 na Jarida la Tiba la Uingereza (British Medical Journal), watafiti
nchini Australia na New Zealand waliripoti kwamba, kukosa usingizi kunaweza
kusababisha madhara makubwa kama ilivyo kwa ulevi wa kupindukia.
Watu waliokuwa wakiendesha magari kwa muda
wa saa 17-19 mfululizo walifanya makosa mengi zaidi ya wale ambao kiwango chao
cha damu kilikuwa na ulevi wa asilimia .05, ambacho ndicho kiwango
kinachoruhusiwa kisheria kwa mtu anayekunywa na kuendesha gari katika Mataifa
ya Magharibi.
Hali hiyo inaelezwa ndiyo inachangia
kutokea kwa ajali nyingi za barabarani kwani madereva ambao wanaendesha muda
mrefu bila kupata usingizi wa kutosha huwa wanakumbwa na msongo wa mawazo,
fadhaa na hawawezi kuchukua tahadhari zozote.
Aidha, kukosa usingizi kwa muda mrefu
kumeripotiwa pia kusababisha madhara mengine ya kiafya ikiwemo matatizo ya hernia (ngiri maji), kuvimba kwa
mishipa, na matatizo mengineyo.
Taarifa za Idara ya Usalama Barabarani
nchini Marekani inaeleza kwamba, zaidi ya ajali 100,000 zinazotokea kila mwaka
zinasababishwa na uchovu wa madereva pamoja na kusinzia.
Ofisa mmoja wa Jeshi la Polisi nchini
Tanzania amethibitisha kwamba, hata ajali nyingi zinazotokea nchini kwenye
barabara kuu zinachangiwa na madereva kukosa usingizi pamoja na uchovu.
“Usingizi ni ugonjwa ama chanzo kikubwa cha
matatizo ya kiafya na kimwili, ndiyo maana huwa madereva wanashauriwa wakifika
mahali walale muda wa kutosha, tena walale kwenye vitanda badala ya kulala
kwenye magari ambako kunawaongezea uchovu na msongo wa mawazo,” amesema ofisa
huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa jeshi.
Hata hivyo, ofisa huyo amedokeza kwamba,
usingizi wakati mwingine hutumika kama silaha ya mahojiano kwa watuhumiwa,
ambapo wengi huwa wananyimwa usingizi kama njia ya kuwalazimisha kusema ukweli
kwa kile wanachotuhumiwa nacho.
“Katika nchi nyingine mtuhumiwa anaweza
hata akawekwa kwenye chumba chenye mwanga mkali usiozimwa, na akiwa huko hawezi
kujua kama ni mchana au usiku, tena wengine wanaweza kufungiwa spika na
kupigiwa muziki mfululizo,” amedokeza ofisa huyo.
Wakati wa utawala wa Pinochet nchini Chile,
na wakati wa Umoja wa Kisoviet, au hata katika Gereza la
Guantanamo la Marekani huko Cuba, kuwanyima usingizi imekuwa
silaha ambayo inatumika katika mahojiano maalum (interrogation).
Taarifa zinasema; “Watuhumiwa wanaofanyiwa
mahojiano hulazimishwa wakae macho kwa siku kadhaa; na wanaporuhusiwa kulala
tu, mara usingizi unapowapitia, huamshwa na kuhojiwa tena.
Menachem Begin, Waziri Mkuu wa Israeli kati
ya mwaka 1977-83 alielezea kuhusu uzoefu wake namna alivyonyimwa usingizi kwa
siku kadhaa wakati alipokuwa mateka wa KGB nchini Russia ambapo alisema:
“Kichwani mwa mfungwa anayehojiwa, hali
fulani huanza kujitokeza. Nafsi yake inakuwa na hofu ya kifo, miguu inalegea,
na anakuwa na hamu ya jambo moja tu: kulala...
Mtu yeyote ambaye amewahi kupatwa na hali hiyo anafahamu kwamba si njaa wala
kiu ambavyo vinaweza kukuzuia pindi usingizi unapokunyemelea.”
Nicole Bieske, msemaji
wa Amnesty
International Australia, aliwahi kukaririwa akisema: "Katika
hali yoyote, kumnyima mtu usingizi ni ukatili, kinyume na haki za binadamu na
kunashusha hadhi ya mtu. Kama hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu basi ni
mateso makubwa."
Comments
Post a Comment