- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mkurugenzi wa Uchumi Jumla, Biashara na Uwekezaji,
Dkt. Felipe Jaramilo akifafanua jambo katika kikao na Waziri wa Fedha na
Mipango kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akizungumza
na ujumbe wa Mkurugenzi wa Uchumi jumla, Biashara na Uwekezaji (hawapo
pichani), katika kikao kilichofanyika Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es
Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto
James akisisitiza jambo katika kikao kati ya Waziri wa Fedha na Mipango na
Mkurugenzi wa Uchumi Jumla, Biashara na Uwekezaji wa Benki ya Dunia, Dkt.
Felipe Jaramilo, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango
akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bi.
Bella Bird na Mkurugenzi wa Uchumi, Biashara na Uwekezaji, Dkt. Felipe
Jaramilo, mara baada ya kikao kilichofanyika Wizara ya Fedha na Mipango Jijini
Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizaraya Fedha
na Mipango)
Na Benny Mwaipaja, WFM
Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa
Uchumi Mpana, Biashara na Uwekezaji wa Benki ya Dunia, Dkt. Felipe Jaramilo
katika ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Dar es Salaam.
Katika kikao hicho,
Waziri wa Fedha na Mipango aliishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kuisaidia
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk. John Pombe Joseph
Magufuli katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maedeleo hapa
nchini.
Dkt. Mpango ameeleza kuwa
uchumi wa nchi umeendelea kukua kwa kiwango cha kati ya asilimia 6-7
kwa muda na hivyo kuiwezesha Serikali kuendelea na utoaji wa huduma za jamii na
kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Mpango ameeleza
kuwa pomaja na nia ya kuendeleza mafanikio mazuri
yaliyopatikana katika awamu za Serikali zilizopita, Serikali ya Awamu ya Tano
ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria kwa dhati kujenga uchumi imara
kwa kuendeleza viwanda na kuweka mazingira mazuri ya biashara ili kuvutia
wawekezaji wa ndani na wale wa nje kuja kuwekeza nchini ,
kujenga miundombinu ya barabara, reli, umeme , viwanja vya ndege na
kuongeza uwekezaji katika utoaji wa huduma za jamii kama vile elimu, afya na
maji.
Aidha, ameeleza kuwa
katika kufikia malengo hayo , Serikali imefanya juhudi mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato, kusimamia vizuri matumizi ya
fedha za Serikali, kuongeza bajeti ya maendeleo hadi kufikia asilimia kati ya
35 na 40 ya bajeti nzimat, kuongeza ufanisi katika utendaji wa
umma na kupambana na rushwa pamoja na mambo mengine.
Pamoja na ukuaji mzuri wa
uchumi, Dkt. Mpango alisema kuwa Taifa bado linakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana, kiwango cha umasikini bado kiko
juu, ukuaji mdogo wa Sekta ya kilimo ambayo imeajiri takribani
asilimia 70 ya watanzania unaosababishwa na ukosefu wa mbegu bora, miundombinu
ya umwagiliaji na soko la uhakika, na kupungua kwa mikopo ya benki za biashara
kwa sekta binafsi pamoja na mambo mengine.
Katika kusaidi juhudi za
Serikali kupambana na changamoto mbalimbali , Dk. Mpango aliiomba Benki ya
Dunia kupitia kwa Dk. Felipe kuisadia Serikali mkopo wa Dola za Kimarekani
milioni 150 kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi na utoaji huduma
( Growth and Service Delivery) amabao uko katika hatua ya
maandalizi.
Mkurugenzi wa Uchumi
Mpana, Biashara na Uwekezaji wa Benki ya Dunia, Dkt. Felipe Jaramilo, kwa
upande wake aliipongeza Serikali ya awamu ya tano ya Dk. John Pombe
Joseph Magufuli kwa kazi nzuri inayofanya ya kusimamia uchumi mpana, kuongeza
makusanyo ya ndani ambayo yanasaidia upatikana fedha kwa ajili ya kugharamia
uwekezaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo, kupambana na rushwa, kusimamia
matumizi ya fedha za umma, na kuongeza ufanisi katika utendaji wa
kazi za umma.
Aidha, Dkt. Felipe
aliishauri Serikali kuwekeza zaidi katika rasilimali watu na
miundombinu ili kulifanya Taifa kuweza kuhimili
ushindani wa kimataifa dunia na kujenga uchumi
unaokua na endelevu.
Vile vile aliieleza kuwa
katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita uwekezaji kutoka nje
umekuwa zaidi katika Sekta ya madini, hivyo alishauri Serikali kuweka mazingira
mazuri ya biashara ili kuwavutia wawekezaji kutoka nje kuwekeza katika sekta za
viwanda na utoaji huduma ili kuongeza wigo wa shughuli za kiuchumi na kuchochea
ukuaji wake.
Comments
Post a Comment