- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Mhe. Luhaga
Joelson Mpina(Mb) mwenye miwani akimkabidhi uenyekiti wa Baraza
la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye Maji katika
nchi za Afrika Mashariki(FASCoM) Mhe. Ssempija Vicente Bamulangaki
ambaye ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Uganda hivi
karibuni.
Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na
Utunzaji
wa Viumbe Kwenye Maji katika nchi za Afrika Mashariki(FASCoM)
linaliwajumuisha
Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi wa Tanzania, Uganda na Kenya, Makatibu Wakuu
na Wakurugenzi katika picha ya pamoja baada ya kikao cha kwanza
cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni Entebbe nchini
Uganda.
Picha
ya pamoja ya ujumbe wa Tanzania ulioongozwa
na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina(mwenye
miwani) baada ya kikao cha kwanza cha Baraza la Mawaziri wa Sekta
ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye Maji katika nchi za Afrika
Mashariki(FASCoM)
kilichofanyika hivi karibuni Entebbe nchini Uganda.Kushoto kwake ni
Katibu Mkuu wa Uvuvi, Dkt Yohana Budeba.
Na Mwandishi Maalum, Entebbe
Zatenga bilioni 4 za kufanya
doria ya pamoja kunusuru kutoweka kwa Sangara.
NCHI za Tanzania,
Kenya na Uganda kwa pamoja zimeridhia
kufanya operesheni ya pamoja ya kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa
Victoria ili kuokoa samaki aina ya sangara walioko katika hatari kubwa
ya kutoweka .
Uamuzi huo
umefikiwa na Baraza la Mawaziri wa Sekta
ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria ( LVFO) ambapo wameidhinisha Dola za
Kimarekani 1,800,000 sawa na sh. Bilioni 4.1 za kitanzania kwa ajili
ya kufanya operesheni hiyo katika Ziwa Victoria.
Hivyo nchi za
Kenya, Uganda na Tanzania kila moja
itapata Dola za Kimarekani 600,000 sawa na Sh. Bilioni 1.3 ili kufanikisha
operesheni hiyo ya kuokoa samaki aina ya sangara walioko katika tishio
la kutoweka katika Ziwa Victoria kutokana na kushamiri uvuvi
haramu.
Kwa siku za
karibuni kulikuwa na malalamiko kuwa
operesheni hiyo inafanyika upande mmoja tu wa ziwa hilo kwa Tanzania
huku shughuli za uvuvi haramu zikidaiwa kufanyika katika nchi za Kenya
na Uganda hivyo uamuzi huo utasaidia kumaliza tatizo hilo lilidumu kwa
miaka mingi sasa.
Akizungumza katika
kikao kukabidhi madaraka kwa nchi
ya Uganda mjini Entebbe juzi, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Baraza
hilo ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Luhaga Mpina
alisema fedha hizo zitasaidia kuongeza kasi ya kupambana na uvuvi haramu
ambapo kwa Tanzania ilishaanza operesheni hiyo mwanzoni mwa mwaka huu
na kuleta mafanikio makubwa.
Mpina pia aliwaomba
viongozi wa nchi wanachama wanaozunguka
Ziwa Victoria kutekeleza kwa vitendo mapendekezo yaliyotolewa na Taasisi
za Utafiti za KMFRI, TAFIRI na NaFIRRI ikiwemo kanuni ya urefu wa samaki
aina ya sangara wanaoruhusiwa kuvuliwa (slot size regulations) kati
ya sentimita 50 hadi 85, Kanuni hii licha ya kuagizwa na Kikao cha Baraza
la Mawaziri 2016 kutumika kwa nchi zote lakini baadhi ya nchi
hazijatekeleza
sharti hili kikamilifu.
Aidha Waziri Mpina
pia aliwakumbusha viongozi wa
nchi zinazotumia Ziwa Victoria kuwaeleza ukweli wananchi wao wanaojishughulisha
na biashara ya uvuvi kuhusu Sheria za Uvuvi za nchi zingine ili kujiepusha
na adha watakazokumbana nazo pindi nchi husika inapochukua hatua kwa
mujibu wa sheria zake na kwamba Tanzania itaendelea kuheshimu sheria
za nchi nyingine ili kulinda rasimali za ziwa hilo.
“Ni imani yangu
kuwa itakuwa hivyo hivyo Kenya
na itakuwa hivyo hivyo Uganda kwani rasilimali hii ni mali yetu sote
hivyo tunajukumu kubwa la kuilinda kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho”alisema.
Hivyo Waziri Mpina
alisisitiza kuwa biashara ya uvuvi
haramu itabaki historia katika nchi za Afrika Mashariki kama viongozi
watakuwa na dhamira safi na kujitoa kwa moyo wote kulinda rasilimali
hizo na kwamba vita hiyo haiwezi kufanikiwa kama viongozi hawatajitoa
mhanga kufanikisha kazi hiyo.
Hata hivyo chini ya
uenyekiti wake, Waziri Mpina
alijivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana ikiwemo kuanzishwa vya vikosi
kazi mtambuka vilivyoweza kongoza mapambano ya uvuvi haramu ikiwemo
Inter-Agency Unit ya Kenya, Multi-Agency Task Team(MATT) ya Tanzania
na Fisheries Protection Force(FPF) ya Uganda.
Alisema
Tanzania imepata mafanikio makubwa baada
ya kuendeshwa kwa operesheni Sangara 2018 ambayo ililenga kupambana
na uvuvi haramu kwa kuondoa zana zote haramu ndani ya ziwa, kudhibiti
wazalishaji zana haramu pamoja na wachakataji wa samaki
wasioruhusiwa.
Aidha Waziri Mpina
alimweleza Mwenyekiti mpya wa
Baraza hilo ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Uganda,
Ssempijja Vicent Bamulaki kutambua kuwa kupewa fursa ya kuongoza watu
ni kupewa fursa ya kuleta mageuzi na kwamba uongozi ni
vitendo sio nafasi.
Waziri Mpina
alieleza kuwa hali ya upatikanaji wa
samaki aina ya sangara ni mbaya katika Ziwa Victoria kwani kwa mujibu
wa taarifa kutoka Taasisi za Utafiti za Afrika Mashariki zinaonyesha
kuwa sangara wenye urefu wa sentimita 50 na kuendelea wamepungua na
kubakia asilimia 5 tu, hivyo juhudi za haraka zisipochukuliwa samaki
hao watatoweka na shughuli za uvuvi katika ziwa hilo zitakoma
.
Aidha, Waziri
alisema katika kipindi cha uongozi
wake kumekuwepo na changamoto mbalimbali zikiwemo uvuvi haramu,utoroshaji
wa mazao ya uvuvi,usimamizi dhaifu wa sheria, uvunaji holela,nguvu kubwa
ya uvuvi,ukwepaji wa mapato ya Serikali, nchi wanachama na nchi za nje
kuingia katika mipaka ya nchi nyingine na kufanya biashara ya uvuvi
bila vibali wala leseni.
Kwa upande wake,
Katibu Mtendaji wa LVFO anayemaliza
muda wake, Godfrey Monor alisema nafasi ya Katibu Mtendaji kwa kipindi
hiki ni ya Tanzania na nafasi na Katibu Mtendaji Msaidizi ni ya nchi
ya Uganda baada ya Sekretarieti iliyopo kumaliza muda wake Agosti mwaka
huu kwa mujibu wa mkataba wa LVFO kifungu cha X hivyo nchi husika zifanye
mchakato wa kujaza nafasi hizo kwa muda muafaka.
Monor alisema
miongoni mwa maazimio ya kikao hicho
ni pamoja na kuundwa kwa chombo kipya kitakachosimamia rasilimali za
uvuvi katika nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (East
Africa Fisheries Organizatin – EAFO) ili kusimamia shughuli zote za
uvuvi katika mito,maziwa na bahari badala ilivyokuwa awali kwa LVFO
kusimamia Ziwa Victoria pekee.
Waziri Mpina
alisema miongoni mwa ajenda
za kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi Kanda
ya Ziwa Victoria ( LVFO) ilikuwa ni kujadili utekelezaji wa maagizo
ya kikao cha awali cha tisa cha Baraza hilo kilichofanyika Nairobi
nchini Kenya Januari 29 mwaka 2016.
Baadhi maagizo
yaliyowasilishwa ni pamoja na
kuwasilisha taarifa za tafiti za kisayansi kutoka katika taasisi zenye
dhamana ya kufanya tafiti za uvuvi kwenye nchi wanachama ili kusaidia
usimamizi wa pamoja wa Ziwa Victoria ambapo taasisi hizo kwa
upande wa Tanzania ni TAFIRI, Kenya ni KMFRI na NaFIRRI kwa upande
wa Uganda.
Mheshimiwa Mpina
alisema kikao hiki kimekuwa ni kikao
cha kwanza baada ya mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika kikao
cha tisa cha Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria
( LVFO) kilichofanyika Nairobi nchini Kenya Januari 29 mwaka 2016 ambacho
kilifanya mabadiliko ambayo yanalifanya baraza hilo kuwa Baraza
la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi na Utunzaji wa Viumbe Kwenye
Maji katika nchi za Afrika Mashariki(FASCoM)
badala
ya (LVFO)
Comments
Post a Comment