- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini ,Silvestry Koka na Naibu waziri wa nishati Subira Mgalu wakibonyeza kiwashio ikiwa ni sehemu ya kuuwasha umeme umeme mtaa wa Mbwawa Mkoleni,wilayani Kibaha. Picha na Mwamvua Mwinyi
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
SERIKALI imetoa tahadhari kwa watumishi ,wakandarasi na wadau wa sekta ya Nishati wanao husika na miradi wasitikise kiberiti kwa kuhamasisha maandamano kupitia shida za wananchi.
Aidha wizara ya Nishati imesema itatumia kiasi cha shilingi trilioni sita kwa ajili ya kuyafikia maeneo 7,873 nchi nzima ili yaunganishwe na huduma ya umeme kupitia miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Hayo yalisemwa kwenye mtaa wa Sagale Magengeni kata ya Viziwaziwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alipokuwa akitembelea maeneo yaliyoko kwenye miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Alisema kuwa ole wake anayetumia tumia shida za wananchi kuhamasisha maandamano kwani akibainika chamoto atakiona.
Mgalu alieleza hayo baada ya kauli ya mwananchi mmoja ambaye alikuwa akitaka umeme na kuambiwa kama anataka umeme aandamane maandamano ya Mange Kimambi.
“Serikali imeshtushwa tena inatokea maeneo haya kwa watu waliopewa dhamana mkandarasi ni dhamana huwezi kuleta jeuri kama unazo fedha usingeomba kazi hizi ni fedha za Rais Dk. Magufuli usilete jeuri,” alisema Mgalu.
Alisema kuwa, hawezi kuamini kama ni watumishi wa serikali wanaweza kufanya hivyo lakini kutokana na kauli hiyo ya mwananchi kujibiwa hivyo watavituma vyombo vinavyohusika vifanye kazi kumbana aliyetoa kauli hiyo kwani watawatafuta kwa udi na uvumba hadi wapatikane.
“Kama hatapatikana itabidi tuitishe gwaride la utambulisho kuweza kumbaini mtumishi aliyetoa kauli hiyo mbaya ambayo inawakatisha tamaa wananchi wakati kupata huduma ni haki yao ndo maana sisi tuko huku ingukuwa hivyo tusingekuja tungekaa lakini tunawatumikia wananchi hivyo hao wakamatwe wajieleze,” alisema Mgalu.
Alisema kuwa tanesco mkoa wa Pwani itabidi wahakikishe mtu au watu waliohusika na kutoa kauli hiyo wanabainika ambao walikuwa wakifuatilia masuala ya mita huko eneo la Viziwaziwa.
Alibainisha kuwa maandamano hayo hayapo na hakuna mtu atakayethubutu kufanya hivyo wananchi hawapaswi kushughulika na suala hilo watu waendelee na kazi zao waachane na watu wasiyoitakia nchi mema.
Akizungumza mbele ya naibu Waziri mwananchi huyo jina tunalo alisema kuwa waliambiwa waweke mfumo wa umeme kwenye nyumba zao ili waunganishiwe umeme.
Alisema kuwa walijibana lakini chaajabu nguzo za umeme zikapelekwa watu ambao wanaviwanja tu hakuna hata nyumba wao waliojenga na kuweka mfumo wa umeme hawakuwekewa nguzo.
“Tuliambiwa kuwa huu ni umeme wa msaada umefikia kilometa moja tu tukafuatilia hadi tanesco kwani tunajua umuhimu wa umeme lakini wakati wale wasomaji wa mita walivyokuja tulipouliza majibu yalikuwa kama tunataka tuandamane na maandamano ya Mange Kimambi,” alisema kwa masikitiko mwananchi huyo.
Aidha mwananchi huyo alisema kuwa kama umeme huo wa REA hautakuwepo basi wapewe wa Tanesco ambapo naibu Waziri alisema kuwa atafuatilia suala hilo ili waliohusika wachukuliwe hatua kama ni wa Tanesco au ni upande wa mkandarasi.
Wakati huo huo Mgalu akiwa Mbwawa alieleza kwenye awamu ya kwanza kupitia REA awamu ya kwanza waliyafikia maeneo 3,559 awamu ya pili wameyafikia 4,314 na kwa sasa bado maeneo 7,873 nchi nzima ili kufikisha huduma hiyo kwa wananchi wengi ambapo kwa mkoa wa Pwani kwa miradi hiyo imetumia kiasi cha shilingi bilioni sita.
“Tunatarajia kuhakikisha watu wanahiotaji umeme kwa wale wa vijijini ambapo zinatakiwa trilioni sita kuhakikisha tunawafikia wananchi pia tunataka kutekeleza agizo la Rais ifikapo Juni 2021 nchi nzima watu wawe wamepata huduma ya umeme,” alisema Mgalu.
Suala la ujazilizi tumeomba awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza na tayari tumeomba fedha kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kutotimia kwenye maeneo
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema serikali iko pamoja na wananchi katika kuhakikisha wanapata huduma hiyo muhimu ya nishati ya umeme kwani ni sehemu ya maendeleo ya nchi.
Alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kama ilivyoahidi ambapo inaendelea kutekeleza ahadi zake na kumshukuru Rais kwa jitihada zake za utekelezaji miradi ya umeme.
Koka alibainisha kutokana na umuhimu wa suala la nishati rais aliamua kuifanya wizara hiyo kujitegemea na imeonyesha matumaini kwani sasa mawaziri wanashuka hadi kwa wananchi.
Comments
Post a Comment