- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb) amesikitishwa
na kauli zilizotolewa na mwanamuziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul (Diamond) wakati akihojiwa na mtangazaji wa
kipindi cha PlayList Bw. Omary Tambwe
(Lily Ommy) wa kituo cha redio cha Times Fm ya Jijini Dar es Salaam.
Mwanamuziki Diamond alitoa maelezo
yaliyoshutumu hatua mbalimbali ambazo Serikali imezichukua katika kutunza na kulinda
maadili ya Kitanzania kwenye tasnia ya Sanaa za muziki.
Waziri
Mwakyembe amesema maamuzi ya kuzifungia
baadhi ya nyimbo na wasanii wawili kwa kukiuka maadili yalifanywa kwa mujibu wa
sheria, na siyo kwa utashi wa Mheshimiwa Naibu Waziri Shonza ambaye anamshutumu. Diamond atambue kuwa Serikali ina taratibu zake na maamuzi ya Naibu
Waziri ni maamuzi ya Wizara.
Aidha,
amesema kuwa vikao na wasanii vimefanywa mara nyingi sana lakini Diamond hakuwahi kuhudhuria vikao hivyo,
na si wajibu wa Serikali kumfanyia kikao cha peke yake.
“Sheria
ni ya watu wote bila kujali umaarufu au nafasi ya mtu katika jamii, hivyo msanii
Diamond anapaswa kutii Sheria na
mamlaka zilizowekwa” amesisitiza Dkt. Mwakyembe.
Dkt.
Mwakyembe ameeleza kuwa si busara kwa Diamond
kushindana na Serikali, endapo anaushauri wowote ni vyema akawasilisha kwa njia
sahihi lakini si kwa kumshambulia Naibu Waziri kwa dharau na kejeli kama
alivyofanya. Aidha, Dkt. Mwakyembe amesema kwamba Diamond kwa mafanikio aliyoyapata kwenye muziki, anatarajiwa kuwa
mfano bora kwa wanamuziki wenzake.
“Napenda
kuwakumbusha wasanii wote kwamba Sanaa ni kazi kama zilivyo kazi zingine, hivyo
pamoja na kuwa na kipaji hicho, wasanii wanatakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
Miongozo inayoisimamia tasnia ya Sanaa kama ilivyo kwa tasnia nyingine”,
amesisitiza Dkt. Mwakyembe.
Lorietha
Laurence,
Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
21/03/2018
Comments
Post a Comment