Featured Post

WAIRAQW - 2: WAMBULU NI WAIRAQW WALIOBAGULIWA


Na Innocent Nganywagwa
KARIBUNI kwa mara nyingine tena kwenye kona hii ya Asili na Fasili. Leo tunaingia sehemu ya pili ya ziara kwa ndugu zetu Wairaqw, kabila tuliloanza kulitembelea jana na kuona baadhi ya mambo yao ya Kikushi yanayovutia.
Wajadi ambao hamkubahatika kusoma simulizi hiyo, nitawaelezea japo kwa ufupi juu ya yale tuliyoyachambua kuhusiana na ndugu zetu hawa. Wairaqw kama lilivyo jina lao, ni kabila lililotokana na jamii zilizotoka nchini Iraq siku nyingi zilizopita.

Walitoka huko karne za mwanzoni, wakasafiri kwa mwendo mrefu hadi kufika mahali wanakopatikana kwa sasa.
Safari za aina hii ni mwendo wa miaka mingi wenye vituo vya makazi ambayo wahusika huzaliana kabla ya kuondoka tena kutokana na sababu mbalimbali za kijamii.
Tulipowapigia hodi Wairaqw kwa mara ya kwanza jana, niliwagusia kidogo juu ya njia za kung’amua asili ya mahali yanakotokea makabila ambayo jamii zake zinatokea mbali na mahali walipo.
Kwa wewe uliyeikosa simulizi hiyo, si vibaya nikikumegea kidogo elimu hiyo ya utambuzi wa chanzo cha kabila husika. Mathalan, maandiko yanaweza kukusaidia kupata ufumbuzi wa udadisi wa chanzo cha kabila unapokabiliwa na hali kama hiyo.
Nilitoa mfano wa watoto wa Nuhu ambao ni Sham, Ham na Japhet, naye Ham alizaa watoto wake wakiwemo Egypt (Misri), Cush (Abyssinia, Ethiopia) na Libya. Sina shaka kuwa, Mjadi unatambua majina ya watoto wa Ham kuwa ni majina ya nchi zilizoko maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa bara letu la Afrika.
Zamani kulikuwa na mifumo mingi ya kupata majina ya maeneo, mojawapo ukiwa ni kurithi jina la mwanzilishi wa kizazi kinachopatikana kwa wingi kwenye eneo husika.
Jambo hili huwa muafaka zaidi, hasa kama mwanzilishi huyo amewafanyia watu wake mambo makuu. Kuna mifano mingi tu ya aina hiyo kwa nchi nyingi duniani, mathalan, Israel ni jina la Jacob ambaye ni baba mwanzilishi wa taifa hilo.
Hiyo ilitokana na jina alilopewa, baada ya kutoshana nguvu na mtu aliyesadikika kutumwa na Mungu kwenye pambano la mieleka. Na kutoka nchi hiyo kuna jamii za watu waliokuja kulowea upande wa Afrika, baadaye wakawa sehemu ya baadhi ya makabila.
Niliwataja Wakurya wa Kinyabhasi ambao tuliona zile silika zao za Uyahudi weusi, kama tulivyoona mambo yao siku nyingi zilizopita tulipotembelea kabila hilo.
Kama ukibahatika kupitia historia ya kustaarabika mnamo karne za awali, utagundua thamani kubwa ya bara letu inayopotoshwa na watu wa mabara pinzani ili tusijitambue.
Kwa bahati mbaya viongozi wetu wa kisiasa hawalioni jambo hilo, japo kuna uthibitisho rahisi usiohitaji maarifa makubwa kuutambua. Hata ukitazama ramani ya eneo la Mashariki ya Kati zilipo Israel na Iraq ambapo zamani paliitwa Messopotamia, panawiana sana na upande wa kaskazini mwa Afrika.
Hata simulizi za imani za kigeni tulizoletewa, zinajaribu kupotosha ukweli wa kuhusika kwa watu weusi kwenye matendo makuu.
Kwa bahati nzuri mwenzenu nina kisima cha ufahamu ambao kama wewe umetopea kwenye imani hizo za kigeni, nikikumegea elimu hiyo utaweza kubishana nami na kuhisi labda nakufuru. Lakini hivyo ‘ndivyo ilivyo’ na ushahidi upo mwingi tu.
Panapo fursa siku nyingine nitakuthibitishia kuwa hata manabii na mitume wengi walikuwa weusi ‘Waafrika’ kama mimi na wewe! Ili ufahamu thamani yako ya Kiafrika, nitawagusia Wamaasai ambao lugha yao mama ya ‘Maa’ ilizaa lugha za makabila mengi yaliyokuja huku kusini kupitia bonde la mto Nile.
Hao walitokea kwenye nchi iliyokuwa moja na sasa ni mbili, yaani Misri na Sudan. Baadhi ya jamii zao za awali ndizo zile zile walizotokea Mafaraoh wa Misri wa nyakati hizo.
Kwa hiyo, kuhamahama na kusafiri, kunatupatia moja ya vyanzo muhimu vya kijiografia vya kutambua yalikotokea makabila kama hawa Wairaqw.
Nikuambie ukweli kuwa Waarabu si wenyeji wa kwanza Misri, wala si waliojenga mapiramidi bali yalijengwa na Wanubi.
Hao ndiyo walioweka msingi mkubwa wa utamaduni wa huko, hata muundo mkubwa wa lugha yao umekopwa na kuingizwa kwenye lugha tanzu za Kiarabu.
Kwa hapa nchini, Wairaqw wanapatikana zaidi kwenye mikoa ya Manyara na Arusha katika wilaya za Mbulu, Babati, Hanang’ na Karatu.
Japokuwa wao ni moja ya makabila yaliyotapakaa kimafungu, kwenye uwanda unaotokea kaskazini mashariki hadi magharibi mwa nchi yetu. Kwa hiyo usishangae ukiwakuta hata Kondoa, lakini walipotoka kule Mesopotamia walivuka Bahari ya Sham na kulowea Ethiopia kwanza.
Vita ya mara kwa mara iliwaondoa mahali hapo, wakaenda kusini magharibi kupitia Bonde la Ufa hadi wakafika Iramba, Singida.
Wakataka kwenda ulipo mpaka wa Iringa na Dodoma, lakini wakati huo Wahehe walikuwa wanapigana na Wangoni.
Basi wakaogopa na wakaamua kwenda Guse Tulaway huko Kondoa, walikopata utulivu wa muda na kulowea kwa shughuli za kilimo na ufugaji. Vita ikafumuka tena na safari hii walipambana na Wabarbaig, wakaamua kuondoka kwenda Gallapo au kwa lugha yao wanapaita ‘Tsea Daaw,’.
Waliokwenda huko ni Wairaqw wa kundi ambalo baadaye lilisababisha kutokea kwa Wagorowa, kundi lingine lililoongozwa na Haymu Now Hatype lilienda Dabil na Gaangaru na kulowea huko.
Hao walikwenda hadi eneo la Mama Isara mahali walipoanzia kuishi mlimani, kutokana na sehemu kubwa ya eneo hilo kumezwa na ziwa.
Lakini kiongozi wao alitumia ujuzi wake wa uganga kulihamisha ziwa hilo, kwa mtupo mmoja wa mshale uliotupwa na mtumishi wake aliyeitwa Mooya na kuchoma katikati ya ziwa.
Lile ziwa lilisogea pembezoni baada ya ule mshale kuchoma katikati, hilo ndilo lile Ziwa Manyara ambalo wenyewe huliita ‘Tlawta Mooya’.
Baada ya ziwa kuhama na wao kupata sehemu ya kufanyia shughuli zao, baadaye walipoongezeka wengine wakahamia Muray, Kuta, Amoa, Kainam, Suum, Datlaa, Tsaayo na Mbulu.
Pia walisogea hadi maeneo mengine ya Babati, Karatu na Hanang’, wakawa wanapatikana kwa wingi maeneo hayo hata sasa.
Hawa Wairaqw wanapendelea nyama kwa kuwa ni wafugaji pia huwinda, wakiwa na ujuzi tangu zama za mawe hadi chuma.
Hiyo ni tangu zama za uwashaji moto wa kupikicha kwa vijiti yaani ‘bui na daha’.
Moto huo walipikia vyakula vyao vilivyotokana na mazao ya mtama, ulezi na uwele ambapo unga wake ulitokana na kusagwa kwa nafaka hizo kwa mawe ya asili ya kusagia. Moja ya vyakula maarufu vinavyopikwa kwa unga wa nafaka hizo, ni ugali laini ulio maarufu kwenye kabila hilo uitwao Xwante.
Pia nafaka hizo zilitumika kutengenezea pombe za sherehe zao za kimila, kwa ufupi tuliishia hapo jumamosi iliyopita.
Katika hizo sherehe zao za kimila, ndugu zetu hawa wana ngoma kwa kila sherehe husika.
Mathalan, ngoma ya ndani huchezwa siku binti anapoolewa na ngoma ya nje iitwayo ‘gilo’ huchezwa wakati wa mavuno, ili kumshukuru Mungu kwa kuwapatia mazao.
Kwenye zile sherehe za harusi akina mama huimba nyimbo za kuwapongeza wanandoa wapya, nyimbo hizo ni kama ule uitwao ‘mudeli’.
Ndugu zetu hawa hupendelea kutumia nyimbo, kwa mambo muhimu ya jamii zao.
Wanapofanya sherehe ya shukrani kwa mwaka wao wa kijadi hufanya maombi ‘slufay’ na ‘giriyda’ yaani uimbaji nyimbo mahsusi za kuomba matukio mazuri na kuepushwa na mabaya, ni kama akina mama wanapoimba ‘sibeli’ kumshukuru Mungu.
Kadiri tutakavyoendelea na mambo yao nitakutafsiria baadhi ya nyimbo za hekaya za lugha zao, zenye mafunzo mbalimbali.
Japokuwa kazi hiyo si nyepesi kutokana na lugha ya ndugu zetu hawa kuwa ngumu, hasa ukiilinganisha na muundo wa baadhi ya lugha zetu.
Katika utamaduni wao kimavazi, Wairaqw huvaa nguo za ngozi zilizolainishwa kwa unadhifu na kushonwa kwa muundo wa mitindo kadhaa kwa kina mama.
Wanaume hujifunika vazi moja refu kiasi lakini wanawake pia hujifunika vazi kama hilo, japo si refu kwa juu maana kwa kuwa chini huvaa vazi lililoshonwa kama sketi.
Pia huvaa viatu vya asili vilivyotengenezwa kwa ngozi za wanyama, hakuna shaka wana ghafi nyingi kutokana na ufugaji na uwindaji. Ndugu zetu hawa ni mafundi wa mambo mbalimbali, licha ya kujitengenezea mavazi kama hayo tuliyoyaona awali. Utengenezaji wa zana mbalimbali uliwawezesha kujikimu kwa kufanya biashara za mabadilishano ya bidhaa.
Baadhi ya zana zao za asili zinazovutia kuziona ni miti iliyochongwa kama majembe ‘taqhwani’, inayotumika kulimia na kushindilia udongo wanapojenga nyumba zao, utifulia shamba jipya hutumia ‘dughsay’ ambapo tofauti ya zana hii na ile ya awali, ni kuwa hii hutengenezwa kwa kuchonga mti mgumu zaidi. Walizidisha ufundi wao waligundua zana mpya, zilizotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi kutoka nchi ya Wambugwe na kukaushwa kwa moto mkali.
Awali, walitumia miti kutengenezea zana za mapambano kama vile mishale na mikuki na mawe yenye ncha kali.
Ndugu zetu hawa ni mafundi wa kutumia mazingira halisi kukabili changamoto za maisha. Mathalan, mazao yanayovunwa huhifadhiwa kwenye ghala zao za asili ‘kuntay’ zinazotengenezwa kwa vinyesi vya ng’ombe.
Nafaka hizo huchanganywa na dawa ya asili ili zisiliwe na wadudu, dawa hiyo hutengenezwa kwa majivu ya kinyesi cha ng’ombe na majani ya miti.
Bado kuna mambo mengi yanayowahusu ndugu zetu hawa, lakini kuna mawili ambayo ningependa kuyaweka sawa katika kukamilishia simulizi ya leo.
Jana niliitaja Mbulu kuwa moja ya maeneo wanakopatikana kwa wingi ndugu zetu hawa, sanjari na kueleza kuwa hapo baadaye tutaona jinsi Wambulu walivyotokana na Wairaqw.
Mara nyingi Wairaqw ukiwatajia kuwa kuna Wambulu, hakika unawakwaza sana maana wanahisi huo ni upotoshaji wa utambulisho wa kabila lao.
Usishangae kama utaamsha hisia kali kidogo kutokana na jambo hilo, maana kuna ukweli kuwa hata kwenye baadhi ya nyaraka muhimu za kimamlaka mara nyingi wakiulizwa kabila na kutaja Wairaqw, wahusika hawawaelewi.
Kuna rafiki yangu Muiraqw aliwahi kukumbwa na matatizo, yaliyomsababisha afike mbele ya vyombo vya sheria. Katika kuandikisha maelezo yake alipoulizwa kabila na kutaja Muiraqw hakueleweka, wakamwandika kuwa Mmbulu.
Hakika hakuwa na jinsi, laiti wale wahusika wangejua kuwa walimkwaza sana kwa kutofahamu Wambulu ni hao hao Wairaqw! Wairaqw mara nyingi hawapendi kusikia jina hilo (Wambulu), kutajwa kuwa ni kabila maana inapotosha ukweli.
Mbulu ni moja ya maeneo yanayokaliwa na Wairaqw, lakini katika historia yao kuna Wairaqw waliotengwa kutokana na imani zao na kupelekea baadhi yao kujiita Wambulu.
Muiraqw mmoja alifiwa na mkewe katika umri usiotarajiwa, bila kufahamika hasa sababu ya kifo hicho. Akahisiwa kuwa na ‘mitiman’ yaani mkosi, basi kwa taratibu zao ikabidi abaguliwe na kutengwa, naye akaenda kuanzisha makazi ya mji wake eneo la Mbulu ya sasa. Utaratibu huo ukaendelea kwa wengine nao waliofiwa na wake na waume zao.
Mbulu ni jina la huyo mtengwa wa kwanza kabisa aliyefiwa na mkewe, japo inawezekana jina hilo ni kwa matamshi ya kawaida yaliyopindishwa kwa silabi za Kiswahili. Maana ndugu zetu hawa wana majina magumu kuyatamka kama ilivyo lugha yao, hakuna shaka ni kutokana na yale matamshi yao ya Kimesopotamia!
Wakati Wairaqw wakati wanaishi kwa muda maeneo ya Kondoa, walipoondoka pale kukwepa vita waliacha mabaki ya jamii zao.
Mabaki hayo ya jamii ndiyo yaliyosababisha kuwepo kwa Waalawa na Waburunge.
Baadaye walisababisha kuwepo kwa Wagorowa, waliotokana na binti wa Kiiraqw aliyeitwa Gorti. Hiyo ilitokea baada ya vita, ambapo binti huyo alihamia pembezoni kwenye eneo lenye bonde katika usawa wa Bonde la Ufa.
Mara kadhaa Wairaqw huchanganywa kiutambulisho na makabila mengine yanayowazunguka, kama wale Wabarbaig waliopigana nao ambao pia wanatangamana nao kwenye baadhi ya maeneo.
Wabarbaig ni sehemu ya Watatooga ambao ni mkusanyiko wa jamii kadhaa wakiwemo Wayaqod, Wasimjeck, Wataturu na Waburadick.
Tukutane kesho.


Makala haya yamehaririwa na yalichapishwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Tanzania Daima Aprili 11, 2009.

Comments