- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
SHIRIKISHO
la Vyama vya Ushirika nchini (TFC) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali lina
mpango wa kuwachimbia visima virefu wananchi ili kuwawezesha kuendesha kilimo
cha umwagiliaji nchini.
Kaimu Mkurugenzi
wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC
Ltd), Bw. Henry Mwatwinza Mwimbe, ameieleza MaendeleoVijijini kwamba,
lengo la mpango huo ni kuwafanya wakulima kote nchini kuendesha kilimo cha
uhakika na endelevu badala ya kutegemea mvua za msimu peke yake.
“Kilimo
ndio uti wa mgongo wa uchumi wa taifa letu na katika kutekeleza kauli mbiu ya
Tanzania ya Viwanda ni lazima malighafi zipatikane kupitia kilimo, hivyo tumeona
ni vyema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tuanzishe mpango huu ambao siyo
tu utamkomboa mkulima, bali utaongeza hata pato la taifa kutokana na uzalishaji
wake,” alisema Mwimbe.
MaendeleoVijijini
inatambua kwamba, kupitia mpango huo hata mikoa inayotajwa kuwa ni nusu-jangwa
hasa ya Dodoma,
Singida, Tabora, Shinyanga na Simiyu inaweza kugeuka kijani kibichi kupitia
kilimo cha umwagiliaji.
Uchunguzi wa
MaendeleoVijijini
umebaini kwamba, vyanzo vya maji vipo vya kutosha, yakiwemo maji ya ardhini,
lakini wakulima wengi hawana uwezo na nyenzo za kuchima visima ama mabwawa ili
kuwawezesha kuwa na maji ya uhakika ya kuendeshea kilimo hicho.
“Mpango
huu ukifanikiwa maeneo mengi nchini, hata yale ambayo yametelekezwa kwa sababu
ya ukame, yatatumika kwa kilimo na kwa maana hiyo hali ya uchumi ya kaya, jamii
na taifa itakua ili kutekeleza Malengo Endelevu ya Dunia pamoja na Mpango wa
Taifa wa Maendeleo kuelekea mwaka 2025,” aliongeza Mwimbe.
Hata hivyo,
amesema kwamba, ikiwa mipango itakwenda vyema, wanakusudia uchimbaji wa visima
hivyo uanze mwaka 2018 ili hadi kufikia mwaka 2019 wananchi waanze kujikita
kwenye kilimo hicho cha umwagiliaji.
Mwimbe amesema
kwamba, anaamini mikoa mingi inaweza kushughulika na kilimo cha mazao ya kila
aina ikiwa tu uhakika wa maji utakuwepo.
MaendeleoVijijini
inatambua kwamba, eneo la Kardesh-barnea katika Israel, ambalo lilikuwa jangwa,
kame na lililojaa mawe, hivi sasa ndilo linalobeba uchumi wa kilimo wa taifa
hilo katika Mashariki ya Kati kutokana na kilimo cha umwagiliaji, teknolojia
ambayo kama itatumika nchini Tanzania inaweza kubadili taswira ya mikoa kama Tabora,
Shinyanga, Simiyu, Singida, Dodoma na Manyara ambayo ni nusu-jangwa.
Nani wanastahili?
Ili wakulima
hao waweze kuchimbiwa visima, kwa mujibu wa Mwimbe, ni lazima wazingatie
masharti haya yafuatayo:
MASHARTI YA KUCHIMBIWA KISIMA
KWA MKOPO KWA AJILI YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI KWA VYAMA VYA USHIRIKA TANZANIA
BARA.
1. Muombaji ni lazima awe Chama
cha Ushirika kilichosajiliwa Tanzania Bara.
·
Kwa
sheria ya vyama vya ushirika iliyopo.
·
Kina
wanachama wanaojishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali ya muda mfupi (mwezi
1 hadi miezi 6).
·
Kiwe
na ardhi inayomilikiwa na chama (kwa ushahidi wa maandishi mfano Hati ya
Ardhi(Kiserikali au kimila).
·
Wanachama
wote wakubaliane kudhaminiana mkopo huu miongoni mwao ili ikitokea mmojawapo
anashindwa kurejesha basi wanaobaki watabeba mzigo huo.
2. Chama hicho lazima kiwe
mwanachama hai wa TFC au kiwe mwanachama wa chama cha upili (UNION) ambacho ni
mwanachama hai wa TFC.
3. Wanachama wakubali
kulipa 15% ya gharama za kisima
kabla ya kazi ya kuchimba kuanza.
· Hii itajumlishwa katika
marejesho ya mkopo yatakayofanywa.
4. Uchimbaji utafanyika
baada ya kupatikana kwa taarifa inayohusu upatikanaji wa maji katika eneo
husika (Itakayofanywa na TFC kwa gharama
za chama husika).
5. Udongo wa shamba husika
utapimwa ili kujua aina ya mazao yanayoweza kustawi na kushauri ipasavyo juu ya
nini cha kufanya ili kuiwezesha ardhi kustawisha zao au mazao yanayotakiwa
kulimwa.
6. Mazao yanayotakiwa
kulimwa ni ya muda mfupi (miezi 1-4) tangu kupandwa hadi
kuvunwa kwa kipindi chote cha mkataba ambapo mkopo unaendelea kurejeshwa. Mabadiliko
ya mazao ya kulimwa yanaweza kufanyika wakati wowote baada ya deni kulipwa.
7. Marejesho ya mkopo yatafanyika
kupitia mauzo ya mavuno yanayopatikana katika kila msimu wa mavuno.
8. Muda wa marejesho ya
mkopo hautazidi miaka mitatu (miezi 36) tangu kuanza kwa msimu wa kilimo.
9. Marejesho ya mkopo yatakuwa
kupitia benki ya NMB au Mitandao ya Simu kwa utaratibu utakaotolewa baada ya
kuingia mkataba wa kuchimbiwa kisima.
·
(Kuna
uwezekano wa kupata mkopo kutoka benki kwa chama ambacho kinaendesha kilimo cha
umwagiliaji hasa ikiwa tayari kina kisima cha maji).
Kwa taarifa zaidi:
Wasiliana: +255 656 331974 au +255 716 775334.
Barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.
Comments
Post a Comment