- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
KILA mwaka
katika kipindi kama hiki cha Majirio, yaani kuelekea siku ya kuzaliwa Yesu
Kristo (Krismas), kote duniani huwa kuna furaha kubwa mitaani na makanisani,
majumba yakiwa yamepambwa kwa miti ya Krismas inayonukia, maua na vikorombwezo
anuai kuikaribisha siku hiyo muhimu kwa wanadamu wote.
Zawadi
mbalimbali huandaliwa kwa ajili ya kuwapatia ndugu na jamaa, Father Christmas
naye akiwaandalia watoto zawadi, huku muziki mwororo ukitawala anga zote
kupitia kwenye redio au televisheni.
Ni wakati
huu ambapo muziki unaotawala huwa ni wa yule mkongwe wa muziki laini, marehemu
Jim Reeves wa Marekani, ambaye vibao vyake 12 kikiwemo cha Jingle Bells pamoja na kundi la Boney M vibao vyao vinatamba
duniani kote ikiwa ni pamoja na hapa Tanzania, ambako pia hukolezwa na kibao
cha Komandoo Hamza Kalala kisemacho Noel-Krimas.
Lakini
mbali na vibao hivyo, kwa ukanda mzima wa Afrika kibao ambacho hutamba zaidi na
kuchukua chati ya juu ni kile kinachojulikana kama Kakoele, ama Viva Christmas
au Noel Krismas, kwa vyovyote
utakavyokiita.
Blogu ya MaendeleoVijijini kwa
kuwatakia heri na baraka za kusherehekea sikukuu hiyo ya Krismas pamoja na
Mwaka Mpya, kwa nia njema kabisa, leo tumeamua kuwaletea kibao hicho ambacho
kimeimbwa kwa lugha ya Kilingala.
Wimbo huo
umetungwa na kuimbwa na Baba Gaston Ilunga wa Ilunga, mwanamuziki kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (zamani ikiitwa Zaire) ambaye alikuwa maarufu
katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.
Kibao
hicho kilichomo kwenye albamu yake ijulikanayo kwa majina niliyoyasema hapo juu
kilifyatuliwa takriban miaka 40 iliyopita nchini Kenya, lakini bado kinaendelea
kutamba na kitaendelea kutamba kwa mashabiki na wafuasi wote wa dini ya
Kikristo kutokana na ujumbe uliomo ndani.
Wimbo huo
unaosikika kila ikaribiapo sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya uliweza kumjengea
jina na sifa kubwa mkongwe huyo ingawa hakuwa mashuhuri kama walivyokuwa akina
Joseph Kabasele 'Le Grand Kalle', Dk. Nico, Franco na wengineo kutoka Zaire.
Aliifyatua
albamu hiyo kwa ajili ya nyimbo za Krismas tu kama alivyofanya Jimmy Reeves,
ambapo ina jumla ya nyimbo tano ukiwemo huo wa Kakoele au Krismas.
Nyingine ni Nakumbuka Krismas, Bewela
Krismas, Super Krismas na Topele
Krismas.
Kakoele
anayeimbwa na Baba Gaston ni msichana wa kileo, yaani 'Sister Duu', mkorofi na
mchoyo wa mapenzi, lakini ni mzuri ajabu. Baba Gaston kwa kuwa anafahamu
Krismas ni siku ya kuzaliwa Masihi aliyekuja kufundisha pendo la kweli kwa
wanadamu wote, anamwendea Kakoele siku hiyo hiyo kumkumbusha kwamba Krismas ni
siku ya 'Mfalme wa Pendo' (Yesu Kristo).
Kwa hiyo
anamtaka ajaribu kujivua uchoyo wake na kuwa mkarimu siku hiyo kisha amwonyeshe
angalau pendo linalotakiwa kwa binadamu badala ya lile la 'Chuna Buzi'.
Hali
kadhalika, katika ushauri huo kwa Kakoele, anatukumbusha wanadamu wote kuwa
tunawajibika wakati huu kushinda udhaifu wetu na kudhihirisha pendo la kweli
ambalo limeletwa na Bwana Yesu Kristo.
Ni kibao
kilichopambwa na maneno ya kumweleza muhibu wako, lakini kikiwa kimelenga hasa
kuwataka wanadamu wote wapendane kama lilivyokuwa kusudi la Bwana Yesu, ambaye
wanadamu wote tunaamini kwamba hata wakati anapaa aliwaambia wanafunzi wake
kuwa, Wapendane, kama Mungu alivyowapenda wanadamu na kumtuma Yeye ili auokoe
ulimwengu na vilivyomo!
Kuzaliwa
Baba
Gaston alizaliwa Julai 5, 1936 katika mji mdogo wa Likasi, karibu na Lubumbashi
katika Jimbo la Shaba kusini-mashariki mwa Zaire na kujipatia elimu yake ya
msingi katika shule ya St. Gabriel, Kapolowe katika Jimbo la Shaba na baadaye
akafanikiwa kuendelea na masomo ya juu katika shule ya Benedict Catholic
Fathers ya mjini Likasi.
Alibadili jina
na kujiita Ilunga Chenji Kamanda wa Kamanda
Gaston Omer baada ya mtawala wa Zaire wa wakati huo, Mobutu Sese Seko (Joseph Desire Mobutu) kuwataka Wazaire
wote kubadili majina yao kutoka ya Ukristo na kuwa na majina ya Kibantu.
Alijitosa
katika ulimwengu wa muziki akiwa na miaka 18 katika Jiji la Kinshasa kwa kuanza
kuimba kwaya kanisani kabla ya kuingia kwenye muziki wa Jazz.
Hii ni baada ya kupata mafunzo ya awali ya muziki kutoka kwa
mpiga piano maarufu wa Kigiriki, Leonides Rapitis, na akafanikiwa kutunga kibao
cha "Barua kwa Mpenzi Gaston" wakati akiwa shule.
Mwaka 1956 akiwa na miaka 20 tu akaanzisha bendi yake ya Baba
National Orchestre, ambapo alifanya ziara ndefu katika nchi za Zambia, Zimbabwe
na baadhi ya nchi za Ulaya na kuwa miongoni mwa wanamuziki wa kwanza wa Congo
kuweka maskani Afrika Mashariki mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Evani Kabila Kabanze, ambaye baadaye alikuja kuwa nyota wa Les
Mangelepa, aliimba na bendi ya Orchestra Baba Nationale mjini
Lubumbashi. Bendi hiyo ilikuwa na kawaida ya kusafiri kwenda Kinshasa kurekodi.
Mnamo mwaka 1971, kwa sababu ya ubovu wa barabara nchini Congo
DR, waliamua kusafiri kwa njia ya Kisangani kupitia Kalemi mpakani mwa Congo na
Tanzania. Lakini badala ya kwenda Kinshasa, wakaamua kuingia Afrika Mashariki,
baada ya kusikia ubora wa studio zilizokuwepo huko.
Mwaka 1972
gwiji huyo alitua Dar es Salaam ambapo onyesho lake la kwanza lilikuwa katika
ukumbi maarufu wakati huo wa White House, Kimara jijini Dar es Salaam, ambako
pia ndiko kulikuwa maskani ya bendi ya Orchestra Marquiz du Zaire (OMACO).
Bendi hiyo ilikaa Dar es Salaam kwa miaka minne. Maisha yalikuwa
rahisi sana na wakapata mashabiki wengi. Hata hivyo, walikuwa wanakwenda
kurekodi Kenya katika Jiji la Nairobi.
Lakini mwaka 1975, Baba Gaston akiwa na mkewe na watoto
wake kadhaa aliamua kuchanja mbuga na kwenda Kenya kuweka maskani baada ya
kugundua kwamba walikuwa na mashabiki wengi zaidi, kabla ya kwenda Arusha
alikozindua kibao chake kingine maarufu cha Talaka
Mpakani Yanitoa Jasho na kuongeza raha pale alipozingua na kibao kingine
cha Mapendo Kizunguzungu.
Wanamuziki wa Congo walikuwa wakifanya vizuri zaidi nchini Kenya
tangu mwishoni mwa miaka ya 1950. Bendi ya OS Africa Band ndiyo
iliyofungua njia kwa bendi za Congo kuteka anga la muziki la Kenya katika
ukumbi maarufu wakati huo wa Starlight Club jijini Nairobi mwaka 1964. Lakini ilikuwa
hadi katikati ya miaka ya 1970, baada ya zama za muziki wa soul wa Marekani
kupita, ndipo muziki wa Zaire ulipoanza kutawala kwenye klabu za usiku za
Nairobi.
Akiwa mtunzi na kiongozi wa bendi, Baba Gaston alikuwa
maarufu katika tasnia ya muziki nchini Kenya kwa miongo mitatu, na hata leo hii
anatajwa kwamba ni gwiji wa muziki wa pop wa Kenya.
Nyimbo zake nyingi aliimba Kiswahili na vibao vyake vilipata
umaarufu mkubwa nab ado vinaendelea kutamba hhata sasa.
Kibao cha "Kakolele
Viva Christmas" (ambacho mwimbaji mkuu ni Kasongo Wakanema ambaye
baadaye alijiunga na Super Mazembe) kilimpatia tuzo ya dhahabu, kikiuza
nakala 60,000 kupitia kampuni ya Polygram.
Nyimbo nyingine kali zilikuwa "Ilunga wa Ilunga," "Kai Kai," na "Mayasa." Mara chache sana
aliimba kuhusu siasa, lakini bibao chake cha kumsifu Mobutu mwaka 1983 kilimpa
tuzo ya dhahabu kutoka kwa rais huyo.
Kuna kipindi Baba Gaston alitamba kwamba aliimba na
wanamuziki zaidi ya 700 kupitia bendi hiyo na kwamba bendi yake ilikuwa chuo
cha muziki.
Hata hivyo, kama alivyosema Hanz Kinzl, meneja wa studio ya Phonogram,
inaonekana bendi ya Baba Gaston ndiyo iliyoongoza kukimbiwa na wanamuziki
nchini Kenya, sababu ikiwa kuwapunja posho wanamuziki wake.
Julai 1976 wanamuziki kadhaa wakiwemo Bwami Walumona,
Kasongo Wakanema, Evani Kabila Kabanze (mwimbaji na mtunzi), Kalenga Nzaazi
Vivi (mwimbaji na mtunzi), Lutulu Kaniki Macky, na Twikale wa Twikale walijiengua
kwenye bendi ya Baba Nationale na kuanzisha bendi ya Orchestra Les
Mangelepa.
Wanamuziki wengine walitoka kwenye bendi hiyo walianzisha
bendi za Bwambe Bwambe, Pepelepe, na Viva Makale.
Majina maarufu ya wanamuziki waliopitia mikononi mwa Baba
Gaston ni pamoja na Starzo ya Esta (ambaye ndiye aliyekuwa nguzo ya bendi ya Festival
du Zaire), BadiBanga
wa Tshilumba Kaikai (mwimbaji na mtunzi, baadaye alikwenda Les Mangelepa
na kutunga kibao cha Nyako Konya), Mukala Kayinda
Coco, Jimmy Kanyinda, Aloni Vangu, Mukala wa Mulumba Bebe, Zainabu, Pepe Mato,
Yassa Bijouley (kwa sasa anaishi Mombasa, Kenya), Lisasi Ebale Mozindo, Zengele
Saida, William Tambwe Lokassa, Kasongo Fundi, Kazadi Mbiya Saleh wa Bambu,
Medico Bwala, Lukangika Maindusa Moustang, Lumwamga Mayombo Ambassedeur, Mukala
wa Mulumba, na Tshimanga Zadios.
Mwimbaji wa kike aliyeimba na Gaston alikuwa Nana Akumu wa
Kudu. Anakumbukwa pia kwa kuimba na bendi ya Pepelepe jijini Nairobi kabla
ya kujiunga na Franco
katika bendi ya TP
OK Jazz na kushiriki kibao cha "Mamou" kilichoimbwa
pia na Madilu System. Kwa sasa anaendelea kupiga muziki jijini Brussels, akiwa
pamoja na mumewe Djo Mali na mpiga gitaa wa zamani wa bendi ya Les Noirs,
Dieudos.
Wanamuziki wengine walliopitia kwenye bendi ya Baba
Nationale ni Mtanzania John Ngereza (aliyeimbia Les Wanyika hadi
alipofariki Februari 2000), Shoushou (Tchou Tchou), Lutulu Kaniki Macky (mwimbaji
na mtunzi), Bosho Kayembe Nyonga (aliyeongoza bendi ya Festival Libaku jijini
Nairobi hadi alipofariki), Tabu Nkotela Kiombwe (aliyefariki mjini Mombasa,
Kenya, wakati akiwa mahabusu kwa kosa la wizi).
Baba
Gaston aliachana na muziki mwaka 1989, lakini mwaka 1994 akiwa na familia yake
alihamishia maskani yake mjini Arusha akitokea Nairobi, Kenya, ambapo alikuwa akitegemea
zaidi biashara zake za duka la kuuza vyakula mbalimbali katika eneo la Majengo
katika Barabara ya Sokoine.
Mwanamuziki
huyo alifariki dunia Jumamosi Machi 18, 1997 katika Hospitali ya KCMC mjini
Moshi kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo. Alifariki akiwa anakaribia
kabisa kufikisha miaka 61 na Machi 25, 1997 akazikwa katika makaburi ya Lang’ata
jijini Nairobi, Kenya.
Katika
kibao hicho Baba Gaston amemwita Kakoele huku akitoa ushauri wake hivi:
1. Kako yeye ngai nakoloba likamboo
(Kakoele
neno nitakalokwambia)
Yo bomba na motema nayo
(lihifadhi
moyoni mwako)
Ezalaka makasi kokotana pamba boyee mama
(Ni vigumu
kukutana hivi kwa matatizo mama)
Bongo sima nagoo bolingana aa
(Halafu
baadaye waishi kwa upendo)
Mama lele bolingo motema pasii x2
(Mama ee
pendo linaumiza moyo x2)
2. Lokola ngai nayebanisee, Kako ee mama
(Kwa kuwa
mimi nafahamika sana, Kako ee mama)
Na basemeki na ngai
(Na
mashemeji zangu)
Ebingi tolingana
(Tunapaswa
tupendane)
Ezalaka makasi tokutana pamba boyee
(Ni vigumu
tukutane (maishani) hivi kwa matatizo)
Bongo sima nayoo tolingana aa
(Halafu
baadaye tuishi kwa upendo)
Mama lele bolingo motema pasii x2
(Mama ee
pendo linaumiza moyo x2)
Kiitikio:
Kakoele mama Kakoele x2
(Kakoele
mama Kakoele x2)
Kakoele mama Kakoele, Papy akolela
(Kakoele
mama Kakoele, Papy analia)
Mama yoka kooo
(Mama hebu
sikia)
Kakoele mama elingi yaye
(Kakoele
mama anataka pendo lako)
Papy akolela, yoka mama
(Papy
analia, sikia mama)
Kakoele mama Kakoele
Viva Krismas x2
(Kakoele
mama Kakoele,
Idumu
Krismas x2)
Noeli mama Yesu abotami - tolingana
(Ni
Krismas mama, Yesu amezaliwa - nasi tupendane)
Viva Krismas x2 Yesu abotami
(Idumu
Krismas x2 Yesu amezaliwa)
Kakoele mama Kakoele x3
Yoka ko! Yoka ko!
(Kakoele
mama Kakoele x3
Sikiliza!
Hebu sikia!).
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com
Simu: +255 656 331974.
Comments
Post a Comment