- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
MKOA wa Mwanza umefanya Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji ambao umeandaliwa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF).
Mwongozo huo ni sehemu ya ripoti tatu zilizotokana na agizo la mkoa wa Mwanza la kutaka kuwekewa pamoja taarifa sahihi zinazogusa uwekezaji mkoani humo ili kurahisisha na kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.
Ripoti nyingine ni Fursafiche katika Viwanda (Industrialization Potentials Report), na Ripoti ya Fursa za Uwekezaji (Investment Opportunities Report) .
Akizungumza katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, Mashirika ya Umma, Sekta binafsi na mashirika ya kimataifa, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mh. John Mongella, alisema walilazimika kuwatafuta wataalamu wa ESRF, kuwasaidia kuweka pamoja fursa zote za mkoa katika mpangilio mmoja unaobainisha fursa zilipo.
Alisema katika kukabiliana na changamoto hizo waliiomba Taasisi hiyo kufanya utafiti na uchambuzi wa kina ili kubaini fursa za uwekezaji zilizopo katika Mkoa huo na ndio wakatoka na ripoti tatu ikiwa Mwongozo huo.
Alisema kazi hiyo ilifanyika kwa miezi 4 kwa msaada wa kifedha kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuanzia mwezi Julai 2017 hadi Novemba 2017.
Mongela alisema: wawekezaji wamekuwa wakipata taabu namna ya uoanishaji wa taarifa zinazotolewa kwao kutoka mamlaka moja hadi nyingine.
Alisisitiza katika hotuba yake kuwa wawekezaji walikuwa wanapata majibu tofauti katika maswali yao walipofika katika mkoa huo kutoka kwa watendaji tofauti ambao ilikuwa lazima kuwaona ili kukamilisha nia yao ya kuwekeza .
Alisema kutokana na hali hiyo waliomba ESRF kuwasaidia kuweka pamoja takwimu zote na kuwavutia wawekezaji kwa kuwa na majibu ya maswali muhimu wanayotakiwa kuyajua kabla ya kuwekeza.
Mongela alisema kwamba mwongozo uliotengenezwa unakwenda sanjari na dira ya maendeleo ya Tanzania na kuwataka wawekezaji wa kigeni na nchini kuwekeza katika mkoa huo.
Alisema wakiwa katikati ya nchi za Afrika Mashariki, zenye soko la watu wapatao milioni 230, Mwanza ni sehemu muhimu na njema kabisa kwa uwekezaji.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi waliyopewa Dkt. Tausi Kida, Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) alisema pamoja na kukabidhi mwongozo huo, Ripoti zote zilithibitishwa na Mkoa Septemba 15, 2017 katika warsha maalum iliyoandaliwa na Mkoa (Validation Workshop).
Tayari ESRF imeshandaa na kuzindua Mwongozo kama huo Mkoani Simiyu mwanzoni mwa mwaka huu.
ESRF imeshakamilisha kuandaa Miongozo ya Uwekezaji katika Mikoa ya Mara na Kilimanjaro ambayo inatarajiwa kuzinduliwa ndani ya wiki mbili zijazo. Miongozo hii itasaidia sana katika kupata Mwongozo wa Uwekezaji wa Taifa utakaoonyesha fursa zilizopo nchini na katika kila mkoa.” Alisema Dkt Kida.
Miongozo hiyo ya Uwekezaji, alisema Dkt. Kida inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016 – 2021) unaosisitiza ujenzi wa Tanzania ya Viwanda ili kuifikisha nchi katika uchumi wa kati ifikapo 2025.
Pamoja na kutoa maelezo ya kazi Dk Kida alishukuru uongozi wa mkoa wa Mwanza na taasisi zake mbalimbali kwa kuwezesha ukusanyaji wa takwimu na kuandaa muongozo huo.
“Kwa namna ya pekee napenda kuushukuru Uongozi wa Mkoa wa Mwanza chini ya Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa John Mongella, Katibu Tawala wa Mkoa – Kamishna wa Jeshi la Polisi Bw. Clodwing Mtweve na viongozi wengine wa mkoa na wilaya zote kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalamu wetu wakati wanapita kutafuta maoni, taarifa na takwimu mbalimbali za kutayarishia Mwongozo huu.” Alisema Dkt. Kida na kuwashukuru pia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ufadhili wa fedha.
“Napenda kuishukuru timu yangu ya ESRF ikiongozwa na Bi. Margareth Nzuki, Mkuu wa Idara ya Maarifa na Ubunifu kwa kuratibu na kuongoza zoezi zima, watafiti washiriki kuanzia na Dkt. Hoseana Lunogelo, Prof. Haidari Amani na Prof. Samuel Wangwe kwa kupitia mwongozo huu.” Alisema na kuwashukuru watafiti vijana waliojitoa kwa nguvu zote kufanikisha kazi hiyo.
Aliwataja vijana hao kuwa ni Bw. Mussa Martine, Bw. Joseph Nyampepela Ngonyani pamoja na Bw. Hafidhi Kabanda .
“Aidha, natambua mchango mkubwa aliotoa marehemu Abdallah Hassan katika uandaaji wa Mwongozo huu.” Alisema.
Aidha alisema kazi hiyo ilifanyika kwa kushirikisha wadau kutoka Sekretarieti ya Mkoa; Halmashauri zote za mkoa wa Mwanza, yaani Mwanza Mjini, Magu, Kwimba, Sengerema, Buchosa, Ukerewe, Ilemela na Misungwi; pamoja na wadau kutoka Sekta binafsi.
Aidha Mkurugenzi huyo aliutaka mkoa kutosita kuwatumia pale wanapohitaji msaada wa kitaalam katika utekelezaji wa Mwongozo na hata kusaidia katika kufanya upembuzi yakinifu (Feasibilty Study) na kuandaa Business Plans kwa baadhi ya fursa ambazo Mkoa utapenda kuwekeza.
Naye Amon Manyama, Mkuu na Mtaalamu wa Miradi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania akizungumza alipopewa nafasi aliwahimiza wananchi wa mwanza kutumia fursa zilizopo kuwekeza badala ya kuwaachia wageni pekee.
Alisema kwamba shirika lake litaendelea kushirikiana na Mwanza katika kuhakikisha kwamba Jiji hilo linaipiku Dar Es Salaam katika uchumi kwa kusaidia kupata wawekezaji wenye uhakika kutoka hata ughaibuni.
Alisema Mwanza ikiwa katikati ya Afrika Mashariki ina kila nafasi ya kukua kwa kasi na wao kama UNDP watahakikisha kwamba wanatoa ushauri wa namna ya kujenga uchumi kwa kutumia sekta binafsi na namna ya kushirikiana na taasisi za kitafiti kama ESRF.
Comments
Post a Comment