- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Kiongozi wa msafara wa wawakilishi wa kampuni ya Henan Juren Crane Group kutoka Jimbo la Henan nchini China, Wang Yuheng (wa pili kulia) akisisitiza jambo wakati alipokutana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Bw. Henry Mwatwinza Mwimbe (kulia). Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.
Na Daniel Mbega
WANANCHI
wa mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na Simiyu wanaweza kujikwamua
kiuchumi kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji ifikapo mwaka 2019 kutokana na
kuwepo kwa mpango wa uwekezaji unaolenga kuchimbia visima virefu pamoja na
mabwawa katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi
wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC Ltd),
Bw. Henry Mwatwinza Mwimbe, amesema hayo jana baada ya kukutana na wawakilishi
wa kampuni ya Henan Juren Group ya China, ambayo
imeonyesha nia ya kuwekeza kwa ubia nchini kwa kutengeneza zana mbalimbali za
kilimo ikiwa ni pamoja na kuchimba visima katika maeneo yaliyo kame.
Lengo la
uwekezaji huo, kwa mujibu wa Mwimbe, ni kuwakwamua wakulima kiuchumi kwa kuwa
na kilimo endelevu cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua, ambazo zimekuwa
hazina uhakika kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na uharibifu
wa mazingira.
“Wanachama
wetu karibu asilimia 80 wanajihusisha na kilimo, hivyo tunaona itakuwa ni vyema
kama tutabadilisha namna ya uendeshaji wa kilimo hiki ili kilete tija kwao na
kwa taifa kwa ujumla.
“Katika
maeneo mengi mvua zinanyesha mara moja kwa mwaka na wakati mwingine siyo za
kutosha, matokeo yake wananchi wanashindwa hata kupata mavuno yanayojidhi
matumizi ya nyumbani, achilia mbali ziada ya kuuza sokoni, lakini kilimo cha
umwagiliaji kina uhakika na kinaweza kuendeshwa wakati wote wa mwaka,” alieleza
Mwimbe.
Alisema
kwamba bado wapo katika hatua za awali kuhusu mchakato huo na akafafanua
kwamba, mradi huo utawahusisha wanachama wote nchini walio kwenye ushirika
ambao watashirikishwa.
Hata hivyo,
alisema mradi mama ni kuunganisha (assembling) zana za kilimo kutoka China kama
matrekta na mashine nyingine zinazoendana na kilimo watakazoziuza kwa wakulima
wa ndani pamoja na nchi jirani, lakini wanaona kwamba hilo litafanikiwa ikiwa
wakulima watajengewa uwezo hasa kwa kuwa na uhakika wa maji ili kuendesha
kilimo cha umwagiliaji.
Dkt. Chikira Ismail Msangi, akifasili kuhusu azma ya wawekezaji hao katika kuanzisha kampuni ya ubia itakayounganisha zana za kilimo kama matrekta na mitambo ya uchimbaji visima na umwagiliaji hapa nchini. Kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Bw. Henry Mwimbe. Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.
“Vijijini
watu wana matrekta lakini yanatumika mara moja tu kwa mwaka kwa sababu ya
kutegemea mvua, kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji ni wazi kwamba wakulima
watahitaji nyenzo zaidi ili kurahisisha kilimo chao, lakini lazima kwanza maji
yapatikane.
“Israel ni
nchi ya jangwa, lakini leo ukienda imebadilika kutokana na kuwepo kwa visima
vilivyochimbwa pamoja na mabwawa na wanalima mazao mengi yenye ubora na
kuyasafirisha duniani kote, sisi Tanzania tunayo ardhi ya kutosha ambayo
tunashindwa kuitumia kwa kuwa tu mahali pengi hakuna vyanzo vya uhakika vya
maji.
“Shinyanga,
Simiyu, Tabora, Singida, Dodoma na Manyara ni mikoa ambayo ina shida kubwa ya
maji japo ina ardhi kubwa, lakini kama watachimbiwa visima wanaweza kufanya
kilimo kwa uhakika na kuwavutia hata vijana wanaokimbilia mijini kutafuta
ajira,” alisema.
Mwimbe alisema
kwamba, katika maeneo ambayo yana mito na vijito kama ya mikoa ya Mtwara,
Lindi, Ruvuma, Rukwa, Katavi na mingineyo, wanaweza kuchimbiwa mabwawa makubwa
ya kuvuna maji ya mvua ambayo yatatumika kwenye kilimo cha umwagiliaji wakati
wa kiangazi.
Wachina wako tayari
Hii ni mitambo itakayounganishwa hapa nchini ambayo ni maalum kwa shughuli za ujenzi na uchimbaji wa mabwawa ya maji.
Bw. Henry Mwimbe (kulia) Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC akionyesha kufurahishwa na picha za mitambo ya uchimbaji mabwawa. Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwimbe (kulia), alitazama zana na mitambo mbalimbali ambayo itaunganishwa hapa nchini katika uwekezaji wa pamoja baina ya TFC na kampuni ya Henan Juren Cranes Group kutoka China. Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi wa
MaendeleoVijijini unaonyesha
kwamba, wawekezaji hao kutoka China wako tayari kwa mradi huo na kwamba
wanaweza kukaa chini na TFC kuangalia namna gani utakavyoendeshwa.
Mmoja wa wawakilishi
hao, Wang Yuheng, alisema lengo kubwa ni kuleta teknolojia ya wakulima wa chini
ili kuinua kilimo chao kilete tija na ikiwezekana wazalishe bidhaa wanazoweza
kuzisafirisha nje ya nchi.
“Tunataka
kuja kuwaletea teknolojia wakulima wa hali ya chini, tunajua zana za kilimo
zinaweza kurahisisha kilimo chao, lakini tutazungumza na TFC ili kuona vipaumbele
vyao vingine katika kilimo ni nini, mbali ya upatikanaji wa maji,” alisema
Wang.
Wang alisema
kwamba, zana zote hizo zitakuja kuunganishwa hapa hapa Tanzania badala ya
kuziingiza zikiwa tayari, hali ambayo itasaidia pia taifa kuingiza fedha za
kigeni pamoja na kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania pamoja na kujifunza ujuzi
mbalimbali.
Maofisa wengine
walioongozana na Wang ni Si Yongbin, Si Guanlei na Zhai Qinwu ambao kila mmoja
ni mtaalam wa teknolojia mbalimbali.
Watembelea EPZA
Wawakilishi
hao wa kampuni ya Henan Juren Group, jana walitembelea
Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZA) jijini Dar es Salaam ambapo
walionyesha kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na maelezo waliyopewa kuhusu fursa
za uwekezaji zilizopo nchini.
Mkuu wa
Mawasiliano ya Umma wa EPZA, Nyanda Shuli, aliwatoa mashaka kwamba hakuna
urasimu wowote kwa wawekezaji, wawe wa ndani au wa nje, na kuwahakikishia
kwamba mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania ni rafiki.
“Tunayo
maeneo mengi ya uwekezaji hapa nchini na kilimo kinapewa kipaumbele kikubwa kwa
sababu ndicho kinachozalisha malighafi za viwanda, ardhi inayofaa kwa kilimo
imetumika kwa asilimia 35 tu, hivyo bado kama taifa tunahitaji kuwekeza zaidi
ili tuzalishe bidhaa za kuuza nje,” alisema Nyanda.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Henry Mwimbe (wa pili kushoto) akijadiliana jambo na baadhi ya wadau katika makao makuu ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji Tanzania (EPZA) jijini Dar es Salaam jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017.
Bw. Nyanda Shuli (wa pili kulia mwenye miwani), Mkuu wa Mawasiliano ya Umma wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji Tanzania (EPZA), akifafanua jambo kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwimbe (wa tatu kushoto) pamoja na ujumbe wa kampuni ya Henan Juren Cranes Group kutoka China walipotembelea makao makuu ya EPZA jana Alhamisi, Novemba 16, 2017.
Bw. Nyanda Shuli akifafanua jambo katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwimbe (kulia) na ujumbe wa wawekezaji kutoka China wakimsikiliza kwa makini Bw. Nyanda Shuli wa EPZA (hayupo pichani).
Ofisa Mwandamizi wa Promosheni wa EPZA, Bi. Nakadongo Fares (kulia) akisisitiza jambo kwa ujumbe wa wawekezaji kutoka China na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) wakati walipotembelea makao makuu ya EPZA, Ubungo External, jijini Dar es Salaam, jana Alhamisi, Novemba 16, 2017.
Nyanda aliongeza
kwamba, kuna maeneo ya kutosha kwa uwekezaji huko Bagamoyo ambayo yako chini ya
EPZA hasa kutokana na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo itakayokuwa mkombozi kwa
Watanzania kiuchumi.
“Pale
zitakuja meli kubwa na mizigo, lakini tunataka zikipakua mizigo hiyo ziondoke
na mizigo mingine kutoka hapa, kama Watanzania watakuwa wamezalisha bidhaa hata
zitokanazo na mazao ya kilimo itakuwa fursa kubwa kupeleka nje,” alisema.
Kwa upande
wake, Ofisa Mkuu wa Promosheni, Bi. Nakadongo Fares, alisema kuna unafuu mkubwa
kwa wawekezaji kutoka nje wanaopitia EPZA kuliko kama wakija wenyewe moja kwa
moja, kwani mamlaka hiyo inayo maeneo tayari yaliyotengwa kwa ajili ya
uwekezaji wa kila aina.
“Uunganishaji
wa matrekta unafanyika hapa pamoja na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao
ambayo yanasafirishwa nje kwa ubora wa hali ya juu, tunashauri hata mitambo na
zana zenu mje mziunganishie hapa hapa ili kutoa na ujuzi kwa Watanzania,”
alisema Bi. Fares.
Kuhusu Henan Juren Group
Kampuni ya
Henan
Juren Crane Group ipo katika Mtaa wa Weizhuang Industrial Park, katika
kitongoji cha Changyuan, jijini Xinxiang katika Jimbo la Henan katika Bara
China, na inaongozwa na Bw. Jason Zhang.
Kampuni hiyo,
ambayo awali ilijulikana kama Henan Juren Crane Co., Ltd, ilianzishwa mwaka 1987
ikijihusisha zaidi na utengenezaji wa crane, lakini sasa inazo kampuni tanzu
kama Henan Juren Crane Services Co., Ltd., Henan Juren Advertisement Co., Ltd. na
Hexin Machinery & Electronic Co., Ltd ambayo inajihusisha zaidi na
utengenezaji na zana mbalimbali zikiwemo za kilimo na umeme.
Kampuni hiyo
ina mtaji wa Yuan za Kichina RMB120,000,000 (takriban Dola za Kimarekani 18,108,561.60),
na rasilimali zenye thamani ya Yuan 200,000,000 (sawa na Dola 30,180,936.00) ambapo
inazo karakana tatu katika wilaya ya kusini, wilaya ya kaskazini na wilaya mpya
huku ikimiliki eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 460,000 na wafanyakazi zaidi
ya 1,200.
Kwa mujibu
wa rekodi za mwaka 2001, uchunguzi unaonyesha kwamba, mapato yalikuwa kati ya
Dola 2.5 milioni na Dola 5 milioni.
Hizi ni crane na madaraja maalum yanayoundwa
na kampuni ya Henan Juren Cranes Group inayotaka kuwekeza nchini.
Makao makuu ya kampuni ya Henan Juren
Cranes Group katika Jiji la Xinxiang katika Jimbo la Henan nchini China.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. +255 656 331974.
Comments
Post a Comment