- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Kaburi la Mtwa Munyigumba Kilonge Mwamuyinga lililopo katika Kijiji cha Lungemba.
Na Daniel Mbega, Iringa
Inaendelea kutoka jana...
KWA bahati
nzuri, binti huyo alijifungua mtoto wa kiume, hivyo akamwita jina la Muyinga Mufwimi
kama alivyokuwa ameelekezwa na Mufwimi mwenyewe.
“Kijana
huyo alipokua, kwa vile Chifu Mwamududa hakuwa na mtoto wa kiume, akaamua
kuukabidhi utawala wake kwa mjukuu ambaye ni Muyinga Mufwimi aliyekuwa hodari
wa vita. Kwa hiyo basi, uchifu huu wa Mkwawa ulitoka kikeni, na hapo ndipo
uchifu ulipoanzia pamoja na ukoo wote maarufu wa Muyinga,” anafafanua Malugila.
Muyinga
Mfwimi akaanza kutawala, akazaa watoto watatu wa kiume – Maliga, Nyenza na
Mpondwa.
Mtwa
Maliga naye akazaa watoto watano wa kiume ambao ni Kitova, Mudegela,
Mgayavanyi, Mkini na Kigwamumembe.
Inaelezwa
kwamba, katika watoto wake hao, alisema Kitova yeye atakuwa tabibu (mganga wa
tiba asilia) na Mudegela atakuwa mtawala, kwa maana hiyo Kitova alikuwa akitibu
maradhi mbalimbali, lakini hasa majeruhi wa vita na kizazi chake ndicho
kinachoendelea kutibu mifupa katika Kijiji cha Image mpaka sasa.
Mudegela
Maliga yeye aliwazaa Lalika, Kalongole, Mbelevele, Wisiko, Kipaule, Mkanumkole,
Lusoko na Mwakisonga.
Hata
hivyo, uchifu wake ulikwenda kwa mwanawe wa tano, ambaye ni Mtwa Kilonge.
Kilonge Mudegela alimuoa Maumba Sekindole aliyemzalia Ngawonalupembe
na Munyigumba, lakini pia akamuoa Sekindole mwingine aliyewazaa Gunyigutalamu,
mkewe wa tatu aliyeitwa pia Sekindole aliwazaa Magidanga, Mhalwike, Mupoma,
Magoyo na Magohaganzali.
“Kilonge alipofariki akazikwa katika eneo ambalo sasa ni
Kijiji cha Lupembe lwa Senga (maana yake Pembe ya Ng’ombe), ambapo kaburi lake
lilikuwa na pembe mbili za tembo, ingawa taarifa zinasema pembe zile ziliibwa na
kwamba walioiba
wote walikufa ukoo mzima. Nasikia serikali ilipeleka pembe nyingine na
kuzichimbia ili iwe kumbukumbu,” anasimulia Malugala.
Utawala una mambo yake, wakati mwingine unatumia njia halali
na haramu ili kuudumisha. Malugala anasema, Munyigumba, ambaye ni mtoto wa pili
wa Mtwa Kilonge, alihisi kwamba angeweza kuukosa uchifu kwa kumhofia kaka yake Ngawonalupembe.
“Kwa hiyo
akafanya hila na kumuua kaka yake Ngawonalupembe ili yeye atawale, halafu
akamchukua Sekinyaga, mke wa marehemu kaka yake kuwa mkewe, lakini wakati
anamchukua, kumbe tayari Sekinyaga alikuwa mjamzito.
“Baada ya
mtoto kuzaliwa, ambaye alikuwa wa kiume, Mama Sekinyaga akamwita Malangalila
Gamoto, pengine kwa maelekezo ya marehemu Ngawonalupembe mumewe. Kwa hiyo
Malangalila siyo mtoto wa Munyigumba, bali wa kaka yake ingawa yeye ndiye
aliyemlea,” anaeleza Malugala.
Malugala
anasimulia kwamba, ugomvi ulitokea baada ya mama huyo kujifungua ambapo
alimwambia Munyigumba kwamba huyu siyo mtoto wake. Hapo Munyigumba akakasirika
na kuamua kumfukuza Sekinyaga na mwanaye.
Inaelezwa
kwamba, alipofukuzwa, Sekinyaga akaelekea katika maeneo ya Sadani, lakini baadaye
Munyigumba akajirudi kwa kuhisi angepata aibu, hivyo ikabidi amrudishe.
“Sasa
wafuasi wake aliowatuma wakamchukue huyo mama wakaenda kumuua huko Sadani, hata
kaburi lake halijulikani liliko. Wao wakarudi na mtoto Malangalila Gamoto. Kwa
hiyo, Malangalila na Mkwawa ni mtu na mdogo wake kasoro baba zao,” anaeleza.
Munyigumba alikuwa na wake watano – Sengimba, Sendale,
Sekinyaga (aliyekuwa mke wa kaka yake), Sembame na Sengimba mdogo. Sengimba
mkubwa aliwazaa Kilemaganga, Mkwawa, Mpangile, Mulimbila na Wiyolitwe; Sendale
alimzaa Mgungihaka; Sengimba mdogo alimzaa Msengele Kilekamagana; Sekinyaga
alimzaa Malangalila Gamoto (kwa Ngawonalupembe); na Sembame alimzaa Mpugumoto.
Mmiliki wa blogu hii akiwa amesimama kwenye kaburi na mdogo wake Chifu Mkwawa, Mtwa Msengele Kilekamagana Munyigumba Mwamuyinga 'Msigawabena' ambalo liko pembeni mwa kaburi la Chifu Munyigumba katika Kijiji cha Rungemba.
JUMAPILI IJAYO:
‘Utawala wa Munyigumba wapinduliwa na mkwewe’.
Imetayarishwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Simu: +255 656 331974.
Comments
Post a Comment