Featured Post

MLONGE NI ZAO LA AJABU LENYE FAIDA KIAFYA NA KIBIASHARA

Mlonge ukiwa umechanua maua.

MILONGE ama kwa lugha ya kisayansi moringa oleifera, ni miti inayostawi vizuri nchini Tanzania ambapo wengi huita ‘zao la ajabu’ kutokana na kuwa na faida nyingi za kiafya na kibiashara.

Kwa kawaida miti hii huwa haiwi mikubwa sana, inakuwa na maua meupe na kisha hutoa mbegu ndogo zinazokuwa kwenye magamba marefu kama kunde japokuwa yenyewe makubwa.
Miti hii hustawi zaidi ukanda wa pwani wenye mvua kiasi na joto, hustawi zaidi kwenye udongo usiotuamisha maji na inaweza kustawi kwenye udongo usio na rutuba nyingi na inahimili ukame kwa kiasi kikubwa.
Ni zao la ajabu kwa sababu hata kiangazi miti hii inaweza kutoa maua ambayo yana faida kubwa kwa jamii.
Wakulima wengi hawafahamu kama mlonge ni zao la biashara linaloweza kuwaongezea tija pia licha ya kuwa na faida nyingine nyingi.
Kwa sasa zao hilo limeanza kupata umaarufu nchini Tanzania ingawa si zao geni kwa sababu limekuwepo nchini kwa miaka mingi japokuwa watu hawakujua kama lina manufaa ya kijamii na kiuchumi pamoja na kimazingira.
Miti ya milonge inaweza kupandwa shambani kwenye mipaka au katikati na ikamfanya mkulima akapata faida ya ziada mbali na kupanda mazao mengine.
Zao hili ni muhimu kwa matumizi ya nyumbani na katika soko la kimataifa.
Mlonge unaweza kudumu kwa miaka hata 20 kama utatunzwa vyema.
Zao hili linalimwa zaidi katika nchi za India, Misri, Ufilipino, Ethiopia, Senegal, Kenya, Uganda, Ujerumani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Rwanda.

MATUMIZI YAKE

Majani ya mlonge yanaweza kupikwa kama mboga na kuliwa, pia yanaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu bila ya kuathiri ubora wake wa virutubisho (nutritional value).
Kwa kawaida, majani ya mlonge yana virutubisho vingi kuliko vyakula vingi tulivyozoea mfano:
Ina vitamin A nyingi zaidi ya karoti
Ina Calcium nyingi zaidi ya Maziwa
Ina madini ya chuma zaidi ya spinach
Ina vitamin C nyingi zaidi ya Machungwa
Ina madini ya potassium zaidi ya Ndizi
Ina protein nyingi zaidi ya nyama na mayai

MATUMIZI MENGINE

Maganda ya mbegu zake yanaweza kutumika kutibu maji (water treatment). Unaweza kuchukua maji ambayo unahisi si salama, unachanganya na maganda ya mbegu zilizopondwa pondwa kiasi, unayaacha kwa muda yatuame kisha unayachuja na yanakuwa salama kwa matumizi.
Mbegu za milonge zinaweza kutumika kama dawa ya kupunguza sukari mwilini kwa wagonjwa wa kisukari.
Unachukua mbegu mbili au tatu unazipasua na kuchukua kokwa ya ndani na kutafuna mara 3 kwa siku, matumizi yanaweza kuongezeka au kuzidi kutegemeana na hali ya mgonjwa.
Sehemu yoyote ya mmea kama majani, magamba, mizizi, au maua yakipondwa pondwa na kupakwa kwenye sehemu yenye uvimbe ni dawa tosha ya kupunguza hali hiyo, pia dawa hii ina uwezo mkubwa wa kupunguza sumu kama umeng'atwa na wadudu kama nyuki, manyigu/dondola, siafu, tandu, nge na kadhalika.
Mbegu zake zinatoa mafuta (40%) yanayojulikana kama BEN OIL, ambayo hutumika kulainishia mitambo maalum kama saa za ukutani, pia mafuta haya ni dawa ya upele na harara.



Comments